Hassan Mwakinyo amtamani Amir Khan baada ya kumchapa Eggington

Hassan Mwakinyo akimchapa Sam Eggington

Chanzo cha picha, Getty Images

Bondia kutoka Tanzania Hassan Mwakinyo ametangaza nia ya kutaka kupambana na bondia maarufu kutoka Uingereza Amir Khan.

Mwakinyo mwenye umri wa miaka 23 ambae usiku wa Jumamosi aliushangaza ulimwengu wa masumbwi kwa kumtandika Mwingereza Sam Eggington mwenye miaka 25 katika raundi ya pili amesema yupo tayari kupambana na Khan.

Pambano la Mwakinyo na Eggington la uzito wa kati lilikuwa la utangulizi kabla ya pambano kubwa la Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas. Khan alishinda kwa tofauti ya alama dhidi ya Vargas.

Mwakinyo aliingia katika uga wa Arena Birmingham, jijini Birmingham Uingereza kama mbadala wa bondia mengine aliyetakiwa kupambana na Eggington kushindwa kufikia vigezo.

Wachambuzi wengi wa masuala ya masumbwi waliliona pambano hilo kuwa rahisi kwa Eggignton ambaye alikuwa na rekodi bora zaidi.

Wakati Mwakinyo akiwa na rekodi shinda mapambano 11 na kupigwa mawili, mpinzania wake alikuwa ameshinda mapambano 24 na kupigwa manne. Eggignton pia ni bingwa wa zamani wa Uingereza, Ulaya na nchi za Jumuiya ya Madola.

Haikuchukua muda mrefu toka pambano lianza kwa Mwakinyo kufurumusha mvua ya makonde kwa Eggington. Mwakinyo alianza raundi ya pili kwa kasi aliyomaliza nayo raundi ya kwanza na baada ya kumsukumia makonde kadhaa bila majibu, mwamuzi wa mchezo huo Kevin Parker alilazimika kumnusuru Eggington kwa kumaliza pambano hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mara baada ya ushindi huo, Mwakinyo alisikika akiimba kuwa anata kupambana na bondia mwengine kutoka Uingereza, Kell Brook.

"Yeye (Eggington) aliingia ulingoni akiwa mwenye kujiamini sana. Nilitaka kuonesha uwezo wangu, sie wengine ni mabingwa pia lakini hatuonekani kutokana na mzingira tunayoishi," alisema Mwakinyo baada ya pambano hilo na kuongeza: "Nimefurahi sana kwa ushindi huu na nimeionesha dunia uwezo wangu halisi."

"Sasa nataka kupambana na Kell Brook, na na nikishamchapa namtaka Amir Khan." Alipoulizwa kama wataweza kustahmili nguvu za Brook akajibu kwa kujiamini: "Kwani wanionaje?"