Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 12.09.2018: Paul Pogba, Theo Walcott, Nacho Monreal, Mario Balotelli, John Terry

Didier Ndong Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Didier Ndong

Juventus watajaribu kumnunua tena nyota wa Ufaransa anayeichezea Manchester United Paul Pogba mwenye miaka 25 mwezi Agosti mwaka ujao. Mabingwa hao wa Italia pia wanataka kumnunua beki wa Brazil, Marcelo, mwenye miaka 30 ambaye kwa sasa huwachezea Real Madrid (Tuttosport)

Barcelona wanajiandaa kuwanunua mabeki kamili wa Uhispania Nacho Monreal, 32, na Alberto Moreno, 26, ambao huchezea Arsenal na Liverpool mtawalia. (Mundo Deportivo)

Kiungo wa kati wa Ujerumani anayechezea Manchester City Ilkay Gundogan, 27, yuko radhi kuwakataa Barcelona ambao wanataka kumnunua mwezi Januari na badala yake kuanzisha mazungumzo kuhusu mkataba mpya katika klabu hiyo ya Etihad. (Sun)

Mkabaji wa Arsenal na Uswizi Stephan Lichtsteiner, 34, amepuuzilia mbali taarifa kwamba anapanga kustaafu. Amedai kwamba anahisi mwili wake ni kama wa kijana wa miaka 28. Lichtsteiner amechezeshwa mara moja pekee kama nguvu mpya na Gunners tangu ajiunge nao kutoka Juventus mwezi Juni. (Daily Mail)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ilkay Gundogan akichezea Ujerumani

Mkurugenzi wa michezo wa Atletico Madrid Andrea Berta anaongoza miongoni mwa wanaotarajiwa kujaza nafasi mpya ya mkurugenzi wa uchezaji soka katika klabu ya Manchester United. (London Evening Standard)

Uwezekano wa John Terry kuhamia Spartak Moscow umeingia mashaka. Beki huyo wa zamani wa Chelsea na England mwenye miaka 37 alikuwa ameafikiana masharti ya mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, ambapo angekuwa analipwa £1.8m, kukiwa na uwezekano wake kuongezewa mwaka wa pili. Lakini sasa vyombo vya habari Urusi vinaripoti kwamba mpango wake umesimamishwa kwa muda huku familia yake ikiwa na wasiwasi kuhusu kuhamia Moscow. Kwa muda sasa kumekuwa na uhasama kati ya Urusi na Uingereza (Mirror)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption John Terry alichezea Aston Villa msimu uliopita lakini akaondoka waliposhindwa kurejea Ligi ya Premia

Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki inataka kumteua meneja wa zamani wa Sheffield Wednesday ya Uingereza Carlos Carvalhal kuchukua nafasi ya Mholanzi Phillipe Cocu, 47, ambaye amewaongoza kwa mechi tisa pekee. Mreno Carvalhal , 52, hajapata kazi tangu alipoondoka Swansea City baada yao kushushwa daraja kutoka Ligi ya Premia mwezi Mei. (Sky Sports)

Winga wa Liverpool kutoka Serbia Lazar Markovic, 24, ameshushwa hadhi na kulazimishwa kushiriki mazoezi na timu ya vijana wa chini ya miaka 23 katika klabu hiyo. Markovic amechezea Liverpool mechi 19 Ligi ya Premia tangu ajiunge nao kwa uhamisho wa £20m kutoka Benfica mwaka 2014. (Liverpool Echo)

Mshambuliaji wa zamani wa England na Tottenham Darren Bent, 34, kwa '100%' anataka kujiunga na Rangers ambao kwa sasa wako chini ya nyota wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard. (Talksport)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lazar Markovic akichezea Liverpool dhidi ya Swansea Desemba 2014

Mshambuliaji wa Everton na England Theo Walcott, 29, anatarajiwa kuikosa mechi ya Ligi ya Premia Jumapili dhidi ya West Ham baada ya kuumia ubavuni. Hata hivyo, Wacott anatarajiwa kuwa sawa kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani Arsenal mnamo 23 Septemba. (Telegraph)

Haki miliki ya picha BBC Sport
Image caption Theo Walcott

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester City na Liverpool Mario Balotelli, 28, alikuwa na uzani wa kilo 100 alipofika kwa mazoezi ya kujiandaa kwa msimu mpya katika klabu ya Nice ya Ufaransa. Uzani huo ni kilo 12 zaidi ya uzani wake rasmi. (L'Equipe)

Kipa wa Manchester United na Uhispania David de Gea, 27, bado anaongoza duniani licha yake kufanya makosa kadha, baadhi katika Kombe la Dunia, kwa mujibu wa meneja wa timu ya taifa ya Uhispania Luis Enrique. (Football Espana)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mario Balotelli alikuwa mfungaji mabao bora wa Nice msimu uliopita, ambapo aliwafungia mabao 18

Mshambuliaji wa Chelsea na Brazil Willian, 30, amesema kamwe hakutana kuihama klabu hiyo na kwamba anatumai atasalia katika klabu hiyo kwa miaka miano ijayo. Willian alikuwa anahusishwa na kuhamia Barcelona mwezi uliopita. (Sky Sports)

Kiungo wa kati Harry Arter yuko tayari kurejea katika kikosi cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland kitakachocheza msururu ujao wa mechi za kimataifa, hata baada yake kuzozana na Roy Keane. Mchezaji huyo mwenye miaka 28 kwa sasa yuko Cardiff City kwa mkopo kutoka Bournemouth. (Telegraph)

Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Didier Ndong

Sunderland wanakusudia kumshtaki mchezaji wao Didier Ndong, 24, wakimtaka alipe £13.6m baada yake kukosa kufika katika klabu hiyo msimu huu. Paka hao weusi wanakiri kwamba kufikia sasa hawafahamu mchezaji huyo wa Gabon yuko wapi. Beki wa Senegal Papy Djilobodji, 29, alirejea katika klabu hiyo wiki iliyopita tu. (Guardian)

Queens Park Rangers wanataka kumnunua winga wa zamani wa Tottenham Nathan Oduwa, ambaye amekuwa akichezeshwa katika kikosi cha kwanza Glasgow Rangers, baada ya mchezaji huyo wa miaka 22 kuwapendeza sana akifanyiwa majaribio. (West London Sport)

Klabu ya ligi ya Championship Preston North End imelazimika kutoshiriki mechi ya kombe la jimbo kwa sababu haikuwa na wachezaji wa kutosha kikosi kamili. Hii ni kutokana na kikosi chao kulemazwa na majeraha, marufuku na wachezaji wengine kuitwa kuchezea timu ya taifa. (Lancashire Post)

Wakufunzi na wafanyakazi wengine katika klabu ya Charlton Athletic inayocheza League One wameanza kupoteza matumaini kuhusu mpango wa kundi la matajiri wa Australia kuinunua, na sasa wanaamini huenda hilo lisifanyike. (London Evening Standard)

Bora kutoka Jumanne

Tottenham wanamfuatilia beki wa Leicester City mwenye miaka 21 Ben Chilwell, ambaye ameitwa kwenye kisosi cha England na ambaye amepangwa kwa ofa ya mchezaji wa Ajax raia wa uholanzi Frenkie de Jong, 21. (Telegraph)

Mshindi mara nne wa Ligi ya Premia Edwin van der Sar, 47, amesema hajiungi katika kikosi cha kiufundi huko Manchester United.(Sky Sports)

Chelsea ililipa zaidi kwa karibu pauni milioni 40 wakati ilitumia pauni milioni 71 kwa kipa wa Athletic Bilbao mwenye miaka 23 Kepa Arrizabalaga mwezi Agosti kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa kandanda CIES. (Football Italia)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kepa Arrizabalaga

Mlinzi wa Manchester United Luke Shaw, 23, huenda akakosa mechi mbili ya klabu chake baada ya kupata jeraha akiichezea England. United watacheza na Watford siku ya Jumapili kabla ya kusafiri kwenda Uswizi kukutana na Young Boys kwenye ligi ya mabingwa Jumatano ijayo. (Mirror)

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Luke Shaw

West Bromwich Albion hawawezi kumpoteza mshambuliaji Dwight Gayle, 28, msimu huu licha ya ripoti kuwa vilabu vya China vinanammezea mate mshambuliaji huyo. Gayle yuko kwenye mkopo wa msimu wote kutoka Newcastle United. (Express & Star)

Kiungo wa zamani wa kati wa Aston Villa Khalid Abdo, 21, amerudi nyumbani Sweden kufanya mazoezi na klabu ya Stockholm AIK. (Birmingham Mail)

Mada zinazohusiana