Eliud Kipchoge: Ni kwanini bingwa wa riadha Kenya anafananishwa na Usain Bolt?

Eliud Kipchoge Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Eliud Kipchoge

Bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge amedhihirisha uhodari wake wa mbio za marathon baada ya kuweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2, dakika 1 na sekunde 39 katika Berlin Marathon.

``Sijui niseme nini, najiona niko juu ya dunia, sina maneno ya kujieleza zaidi,'' alisema Kipchoge alipovunja rekodi a dunia kwa sekunde 78.

Mkenya mwenzake Dennis Kimeto aliyekuwa anashikilia rekodi ya dunia (2:0257) alimpongeza Kipchoge akisema kwenye mtandao wa twitter:

``Hongera Eliud Kipchoge. Wewe ni mfano wa kuigwa na wanariadha wote duniani.

Tangu aanze kukimbia marathon mwaka wa 2012, Kipchoge, mwenye umri wa miaka 33, ameshinda mara kumi kati ya marathon 11 alizokimbia.

Ameshindwa mara moja tu na mwenzake kutoka Kenya Wilson Kipsang mwaka wa 2013 wakati Kipsang aliweka rekodi mpya ya dunia ya 2:03:23 katika mbio za Berlin ambako jumla ya rekodi nane za dunia zimevunjwa.

Akieleza mbona rekodi nyingi za dunia za marathon zimevunjwa Berlin, Kipchoge anasema:

`` Napenda Berlin sana kwa sababu sehemu yote ya kukimbilia ni tambarare na mashabiki wanajua kushangilia wakimbiaji.''

Berlin marathon ni ya saba kwa malipo ya juu kwa washindi katika marathon kumi duniani, ya kwanza ikiwa ni Dubai marathon.

Mshindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake wa Berlin marathon hulipwa $55,000, mwanariadha akikimbia chini ya 2:04:30 kwa wanaume na 2:20:00 kwa wanawake analipwa $40,000 na $69,000 kwa kuweka rekodi mpya ya dunia.

Kipchoge alizaliwa Novemba tarehe 5 kijiji cha Kapsisiywa kaunti ya Nandi eneo la bonde la ufa.

Image caption Eliud Kipchoge katikati akikabiliana na wanariadha kutoka Ethiopia

Alianza kuwika mwaka wa 2003 aliposhinda taji la dunia katika mbio za nyika kwa upande wa wanariadha chipukizi, akaweka rekodi mpya ya dunia mbio za mita elfu tano na akashangaza wengi kwa kuangusha miamba Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Hicham El Guerrouj wa Algeria.

Kipchoge alishinda mbio hizo za dunia mwaka wa 2003 kwa dakika 12, sekunde 52 nukta saba-tisa huku Guerrouj akimaliza wa pili na Bekele wa tatu..

Kocha mkongwe nchini Kenya, Mike Kosgei, alikua na Kipchoge mjini Paris kama mkufunzi mkuu wa timu ya Kenya.

``Nilianza kuona kipaji chake kwenye mfululizo wa mbio za Eveready cross-country zilizokuwa zinafanyika hapa nchini Kenya,'' anasema Kosgei.

Mbali na Kipchoge, wanariadha wengine wa Kenya walioshiriki fainali ya mbio za mita elfu tano ni John Kibowen aliyemaliza wa pili, Abraham Chebii wa tano na bingwa wa dunia mwaka wa 2001 Richard Limo akamaliza wa saba.

``Siku hiyo ya fainali ya mbio za mita elfu tano nilimwambia Eliud akimbie nyuma ya Bekele (Kenenisa) wa Ethiopia na El Guerrouj (Hicham) wa Algeria.''

Bekele, ambaye alikua ameshinda dhahabu mbio za mita elfu kumi katika mashindano hayo ya Paris, aliongoza sehemu kubwa ya mbio hizo na hatimaye Kipchoge akachukua uongozi kwa muda kisha Guerrouj akafyatuka mzunguko wa mwisho lakini Kipchoge aliongeza kasi na kumpita mkimbiaji huyo wa Algeria kwenye msitari wa mwisho.

Kosgei anasema hajaona ushindani mkali kama huo:``Hapo ndio nilijua Eliud ana kipaji cha mbio na ataenda mbali.

Guerrouj hakuamini ameshindwa na Eliud (wakati huo akiwa na umri wa miaka 18).

Alikuja kwangu na kuniuliza huyu mtoto ni nani. Niliangua kicheko kwa jinsi Guerrouj alivyoulizia Kipchoge kwa hasira.

``Kutoka hapo Kipchoge akaanza kupanda juu. Paris ilikua mara yake ya kwanza kukimbia mbio za watu wazima.

Kabla ya hapo alikua anashiriki zile za chipukizi. Alipovunja rekodi ya dunia Berlin kwangu mimi sikuona ajabu kwa sababu nilijua siku moja ataivunja tu.

``Kinachomwezesha Eliud kufanya vyema ni nidhamu na kuskiza mawaidha ya makocha wake.

Ni mkimbiaji mtiifu sana na ana nidhamu ya hali ya juu. Sijaona mkimbiaji ana nidhamu kumshinda Eliud.

Hata Jumapili tukiwa kambini yeye peke yake ndiye anabaki na wenzake wengine wakiwa nje.

Hubakia kufanya usafi na kuosha vyoo akifua nguo zake mwenyewe.

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Wanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge na Vivian baada ya kushinda London Marathon mwaka 2018

Sitaona ajabu Eliud akikimbia chini ya saa mbili mbio za marathon.''

Mwaka jana Kipchoge alijaribu kukimbia chini ya saa mbili huko Italia lakini hakufanikiwa, akakimbia muda wa kasi zaidi duniani wa 2:00:25.

Hatahivyo muda huo haukutambuliwa rasmi kwa sababu Kipchoge alisaidiwa na wachochea kasi kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Bado Kipchoge ana imani ya kukimbia chini ya saa mbili katika mbio za marathon.

``Hakuna kitu kisichowezekani dunia hii mtu akijiamini. Nina uwezo wa kukimbia chini ya saa mbili.

Nani alijua kama siku moja binadamu atafika hadi kwa mwezi huko juu,'' anasema Kipchoge.

Mayweather kuzipiga tena na Pacquiao

Mourinho hawezi kuficha hisia zake - Lukaku

Kipchoge, mshindi mara tatu wa Berlin marathon, ni mkimbiaji wa 50 kuweka rekodi mpya ya dunia na mwanariadha wa tano wa Kenya kuweka rekodi mpya ya dunia ya marathon baada ya Paul Tergat 2003, Patrick Makau 2011, Wilson Kipsang 2013 na Dennis Metto 2014.

Amewahi pia kushinda London marathon mara tatu mwaka wa 2015, 2016 na 2018 na Chicago marathon mwaka wa 2014.

Kocha wa Kipchoge tangu akiwa chipukizi Patrick Sang alikua naye Berlin, na kwa maoni yake Kipchoge ana uwezo wa kufanya makubwa zaidi.

``Sote tumefurahia sana Kipchoge kuweka rekodi mpya ya dunia. Kilichomwezesha kufanya hivyo ni nidhamu yake.

Ni mkimbiaji hajanipa tatizo lolote tangu nianze kumfunza. Ni mtiifu na mcha Mungu hakosi kuomba kila asubuhi,'' anasema Sang..

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii