Cristiano Ronaldo aruhusiwa kucheza dhidi ya Man United, Ramsey atofautiana na Arsenal

Cristiano Roanldo baada ya kupewa kandi nyekundu Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa Juventus Cristiano Ronaldo atashiriki katika mechi ya vilabu bingwa dhidi ya klabu yake ya zamani Manchester United mwezi ujao baada ya Uefa kuamua kwamba lazima ahudumie marufuku ya mechi moja pekee kufuatia kadi nyekundu aliyopewa katika mechi ya kombe la vilabu bingwa.

Nahodha huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 33 alitolewa nje wakati Juve ilipopata ushindi wa 2-0 dhidi ya klabu ya Valencia wiki iliopita baada ya kuonekana kuzivuta nywele za beki Jeison Murillo.

Ilikuwa kadi nyekundu ya kwanza ya mechi za vilabu bingwa dhidi ya Ronaldo.

Juventus itacheza dhidi ya Man United katika kundi H katika uwanja wa Old Traford tarehe 23 Oktoba.

Marufuku ya mechi tatu ingemfanya Ronaldo kukosa mechi ya marudiano itakayochezwa mjini Turin tarehe 7 mwezi Novemba.

Atakosa mechi ya Juve ya vilabu bingwa dhidi ya klabu ya Uswizi ya Young Boys mnamo tarehe 2 Oktoba.

Ronaldo ambaye ni mshindi mara mara tano wa kombe la vilabu bingwa ambaye alijiunga na Juventus kutoka Real Madrid kwa dau la £99.2 msimu uliopita , alijaribu kufunga krosi lakini akazuiwa na Murillo ambaye alikuwa anaanguka.

Alimtaka Murillo kusimama na kuonekana akimvuta nywele zake kabla ya kuondoka akiwa na hasira.

Refa Felix Brych alishauriana na naibu wake nyuma ya goli kabla ya kutoa kadi nyekundu, na kumfanya Ronaldo kububujikwa na mchozi alipokuwa akitoka uwanjani.

Ikilinganishwa na ligi ya EPL ambapo angepigwa marufuku kushiriki mechi tatu, adhabu ya Uefa inategemea kisa baada ya kisa.

Marufuku ya mechi moja inamaanisha kwamba mtu hawezi kukata rufaa, lakini sheria za Uefa za michuano hiyo zinasema kuwa iwapo kutakuwa na makosa mabaya zaidi, shirika la Uefa linalosimamia maadili lina uwezo wa kuongeza adhabu hiyo.

Mazungumzo ya kandarasi ya Aaron Ramsey yagonga mwamba

Haki miliki ya picha Getty Images

Wakati huohuo mazungumzo kati ya Arsenal na kiungo wake wa kati yamegonga mwamba.

Kandarasi ya Ramsey inakamilika tarehe 30 mwezi Juni na Gunners walikuwa na matumaini ya kuongezea.

Na kwa sababu mazungumzo yamekwama huku kukiwa haijulikani iwapo yataendelea, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atauzwa mnamo mwezi Januari ama kuwa ajenti huru msimu ujao.

Kwa vile mambo yalivyo, raia huyo wa Wales ataweza kufanya makubaliano na klabu nyengine kutoka mwezi Januari.

Ramsey alijiunga na klabu ya Arsenal mwaka 2008 kwa dau la £4.8m kutoka klabu ya Cardiff City.

Ndiye mchezaji wa Arsenal aliyehudumu kipindi kirefu na kufunga bao la ushindi la kombe la FA 2017.

Ramsey alikuwa mchezaji wa ziada katika ushindi wa Brentford katika kombe la Carabao siku ya Jumatano.

Mada zinazohusiana