Kylian Mbappe atambuliwa na jarida maarufu la Time

France forward Kylian Mbappe Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kylian Mbappe alifungia Ufaransa dhidi ya Iceland Alhamisi

Mshambuliaji nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe ametajwa kama mtu mwenye matumaini makubwa katika soka siku za usoni.

Gazeti la Time limechapisha picha yake kwenye ukurasa wake wa mbele na kumtaja kama "siku za usoni za soka."

Mbappe alianza kugonga vichwa vya habari Septemba mwaka jana alipohamia PSG.

Mabingwa hao wa Ufaransa walilipa euro 180 milioni ($207 milioni) kumnunua kutoka klabu ya Monaco, wakati huo akiwa na miaka 18.

Mshahara wake baada ya kuhama ulikuwa ni euro 1.5m ($1.8m) kwa mwezi.

Sifa zake zilizidi katika Kombe la Dunia nchini Urusi alipofana sana akichezea timu ya taifa ya Ufaransa na kuwasaidia kushinda kombe hilo baada ya miaka 20.

Alisifiwa pia na mchezaji soka nguli wa Brazil Pele kutokana na uchezaji wake.

Katika michuano hiyo, aliibuka kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kufungia Ufaransa bao alipowafungia bao la pekee katika mechi waliyowalaza Peru 1-0 hatua ya makundi.

Kinda huyo kutoka mji wa Bondy viungani mwa Paris baadaye aliwapangua Argentina na kufunga maba mawili na kisha akawashindia mkwaju wa penalty.

Ufaransa waliwalaza Argentina 4-3 katika mechi hiyo ya hatua ya muondoano.

Kwa kufanya hivyo, Mbappe alikuwa mchezaji wa pili asiyetimiza miaka 20, baada ya Pele mwaka 1958, kufunga mabao mawili katika mechi ya Kombe la Dunia.

Mbappe alipofunga bao fainali kwa kombora kali akiwa hatua 25 kutoka kwenye goli katika mechi waliyowalaza Croatia 4-2 kwenye fainali, alikuwa kinda wa pili kufanya hivyo baada ya Pele mwaka 1958.

Mbappe alifunga jumla ya mabao manne michuano hiyo na akatunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Kombe la Dunia la Fifa katika michuano hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kylian Mbappe aliingia nafasi ya Antoine Griezmann dakika ya 60 dhidi ya Iceland

Pele mwenyewe, alisema: "Kylian akiendelea kufikia rekodi zangu hivi, huenda nikalazimika kuondoa vumbi kwenye buti zangu (na kuingia uwanjani)."

Mbappe atatizima miaka 20 mnamo tarehe 20 Desemba.

Alitekeleza mchango muhimu katika kuwaepushia Ufaransa aibu Alhamisi alipowafungia penalti katika mechi ambayo walitoka sare 2-2 dhidi ya Iceland.

Mada zinazohusiana