Hassan Wario: Aliyekuwa waziri wa michezo Kenya kushtakiwa kwa tuhuma za ufujaji wa fedha katika Olimpiki Rio

Balozi wa Kenya nchini Austria Hassan Wario ni miongoni mwa maafisa 7 wanaochunguzwa
Image caption Balozi wa Kenya nchini Austria Hassan Wario ni miongoni mwa maafisa 7 wanaochunguzwa

Balozi wa Kenya nchini Austria Hassan Wario ni miongoni mwa maafisa saba wanaochunguzwa upya na idara ya upelelezi kuhusu madai ya ufujaji wa $872,867 sawa na 88,000,000 za Kenya katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 iliyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Wario wakati huo alikua ni waziri wa michezo nchini Kenya. Pesa hizo inadaiwa zilikua ni tiketi za ndege za kikosi cha Kenya lakini maafisa walipandisha bei ya tiketi hizo kupita kiasi kwa manufaa yao wenyewe, kulingana na ripoti ya kamati ya kuchunguza kashfa hiyo.

Kamati hiyo iliongozwa na Paul Ochieng ambaye ni msimamizi wa wanafunzi katika chuo cha Strathmore mjini Nairobi. Baadhi ya wengine kwenye kamati hiyo walikua ni wakimbiaji wa zamani wa timu ya Kenya Ibrahim Hussein, Rose Tata-Muya na Elizabeth Olaba.

Mbali na Wario, wengine watakaochunguzwa ni mwenyekiti wa zamani wa chama cha Olimpiki cha Kenya na mkimbiaji hodari Kipchoge Keino, katibu wa zamani wa wizara inayosimamia michezo Richard Titus Ekai, mkurugenzi wa zamani wa usimamizi katika wizara hiyo Harun Komen, kiongozi wa kikosi cha Kenya katika michezo ya Olimpiki ya Rio Stephen arap Soi, Patrick Kimathi na katibu wa cha Olimpiki cha Kenya Francis Kinyili Paul.

Tayari Soi amekamatwa na Polisi Ijumaa ya tarehe Octoba 12 mwaka huu na kwa hivi sasa yuko katika kituo cha polisi cha Muthaiga. Hao wengine wanatakiwa kuripoti kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi kufikia Jumatatu ya Octoba tarehe 15.

Image caption Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji

Jitihada zetu za kuzungumza na Wario zimeambulia patupu na haijulikani kama naye pia ataripoti kwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi.

Baadhi ya maafisa hao wanakabiliwa na madai ya kutaifisha pesa za wakimbiaji walioshinda medali mjini Rio. Pesa hizo hutoka kwa kampuni ya Marekani ya kutengeza vifaa ya michezo Nike ambayo hutoa $15,000 kwa mshindi wa dhahabu, $7,500 kwa mshindi wa fedha na $5000 kwa wanaopata medali ya shaba.

Kwa miaka kadhaa sasa wanariadha wa Kenya wanaoshinda medali katika michezo ya Olimpiki na ya Jumuiya ya Madola wamekua wanalalamika hawapati pesa hizo kutoka Nike.

Image caption Mbunge Wesley Korir aliangazia katika mitandao ya kijamii hali duni inayowakabili wanariadha wakiwa katika mashindano hayo Rio 2016

Kamati ya Olimpiki Kenya yavunjiliwa mbali

Waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario alitangaza kuivunjilia mbali Kamati ya Taifa ya Olimpiki mnamo Agosti 2016 kuhusiana na maandalizi ya timu hiyo kwa michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Waziri alitangaza hatua hiyo kwenye kikao na wanahabari huku ikibainika kwamba bado kuna wachezaji kwa wakati huo ambao hawakuwa wameondoka Rio.

Bw Wario amesema majukumu ya kamati hiyo, maarufu kama NOCK, yatatekelezwa na Sports Kenya.

Waziri huyo pia alitangaza kuunda kamati ya kuchunguza yaliyojiri wakati wa maandalizi ya michezo hiyo na wakati wa michezo yenyewe.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii