Wilfried Zaha: Winga wa Crystal Palace asema ametumiwa vitisho baada ya sare na Arsenal

Wilfried Zaha

Chanzo cha picha, Reuters

Mshambuliaji wa klabu ya Crystal Palace Wilfried Zaha anasema ametumiwa ujumbe wa ubaguzi wa rangi na vitisho baada yake kujishindia penalti wakati wa mechi ambayo walitoka sare 2-2 na Arsenal.

Zaha aliangushwa na beki wa kushoto wa muda Granit Xhaka dakika za mwisho za mechi na kusababisha mkwaju wa penalti ambao kutoka kwake Luka Milivojevic alifunga bao la kusawazisha.

Zaha anasema amepokea ujumbe wenye vitisho vya kutaka kumuua.

"Kwa watu wale wanaozidisha hili na kuwa wabaguzi wa rangi na kuitakia familia yangu mauti, natawakia nyinyi na familia zenu pia kila la heri," amesema.

"Maisha yangu bado yanaendelea vyema sana licha ya chuki zenu.."

Baada ya mechi hiyo, kwenye mahojiano ya runinga ya moja kwa moja, Xhaka alikiri kwamba alifikiria hiyo ilikuwa "penalti ya wazi".

Tangu kuanza kwa msimu wa 2014-15, ni mshambuliaji wa Leicester Jamie Vardy (13) ambaye amejishindia penalti nyingi zaidi ya Zaha (11, aliye sawa na Raheem Sterling) katika Ligi ya Premia.

Tangu mwanzo wa msimu wa 2016-17, Arsenal ndiyo klabu iliyoadhibiwakwa wapinzani wake kupewa penalti nyingi zaidi (18) wakati wa mechi ligini. Kutoka kwa mikwaju hiyo, wamefungwa mabao 17.