Matokeo na Droo Kombe la Carabao: Arsenal wapewa Spurs baada ya kuwashinda Blackpool, Chelsea wawacharaza Derby wa Frank Lampard

Chanzo cha picha, Getty Images
Klabu hizo mbili za London kaskazini mara ya mwisho kukutana katika michuano hiyo ilikuwa mwaka 2015, ambapo Mathieu Flamini alifunga mabao mawili na kuwapa Gunners ushindi wa 2-1 raundi ya tatu
Arsenal wamepangwa kucheza dhidi ya mahasimu wao wa London kaskazini Tottenham Hotspur katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Carabao, ambalo zamani lilifahamika kama Kombe la Ligi.
Gunners, ambao walishindwa kwenye fainali msimu uliopita, watakuwa wenyeji wa majirani zao hao uwanjani Emirates katika mechi ambayo itachezwa wiki itakayoanzia 17 Desemba.
Klabu ya League One ya Burton Albion, ambao ndiyo ya chini sana kuorodheshwa iliyosalia bado kwenye michuano hiyo itakuwa mwenyeji wa klabu ya ligi ya Championship, Middlesbrough.
Chelsea watakuwa wenyeji wa Bournemouth, naye mshindi kati ya Leicester na Southampton akitarajiwa kukutana na mshindi wa mechi kati ya Manchester City na Fulham.
Matokeo ya mechi ya Kombe la Carabao zilizochezwa 31 Oktoba
- Arsenal 2 -1 Blackpool
- Chelsea3-2 Derby
- West Ham 1-3 Tottenham
- Middlesbrough 1-0 Crystal Palace
Tarehe mpya ya kuchezwa kwa mechi hiyo ya Leicester na Southampton uwanjani King Power Stadium, bado haijatangazwa.
Mechi hiyo, ambayo awali ilipangiwa kuchezwa Jumanne, iliahirishwa baada ya kifo cha mmiliki wa Leicester, bilionea wa Thailand Vichai Srivaddhanaprabha aliyefariki katika ajali ya helikopta Jumamosi.
Manchester City, waliowashinda Arsenal katika fainali msimu uliopita na kushinda kombe lao la kwanza chini ya Pep Guardiola, watakutana na Fulham uwanjani Etihad siku ya Alhamisi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Derby walijifunga mabao mawili katika kipindi cha dakika 16 kipindi cha kwanza
Arsenal na Spurs watakutana mara mbili uwanjani Emirates ndani ya muda wa wiki mbili hivi kwani mechi yao ya Ligi ya Premia imeratibiwa kuchezwa 2 Desemba.
Droo kamili:
Arsenal v Tottenham
Leicester/Southampton v Manchester City/Fulham
Middlesbrough v Burton
Chelsea v Bournemouth