Taifa Stars, Bafana Bafana, Harambee Stars, Chipolopolo, Amavubi, Cranes: Yafahamu maana na majina ya timu za taifa Afrika

Salum Abubakar wa Tanzania akikabiliana na Jean Jacques Gosso wa Ivory Coast jijini Dar es Salaam mnamo 16 Juni, 2013

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Salum Abubakar wa Tanzania akikabiliana na Jean Jacques Gosso wa Ivory Coast jijini Dar es Salaam mnamo 16 Juni, 2013

Mshambuliaji wa Benin, Steve Mounie, ameunga mkono pendekezo la kubadilisha jina la timu ya taifa kutoka The Squirrels (Kuchakuro) akisema huenda linachangia matokeo mabaya.

Shirikisho la soka la Benin (FBF) liko katika mchakato wa kubadilisha jina hilo la utani na badala yake kutumia jina lenye na hadhi zaidi.

Kiungo huyo wa kati wa klabu ya Huddersfield ya Uingereza amependekeza timu hiyo ipewe jina la The Pythons (Chatu).

"Chatu, nyoka ni alama muhimu sana nchini Benin," alielezea BBC.

"Kuna hata hekalu la Chatu nchini Benin, na kuna utamaduni mkubwa kuhusiana na chatu. Watu humuenzi sana chatu Benin."

Ameongeza kuwa atafurahia sana kusikia mapendekezo ya wengine pia.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Steve Mounie

Amesisitiza kuwa "Ni mnyama mzuri lakini wanaweza kuchagua jina jingine, sina neno kwa hilo. Kwa sababu hata hiyo haitabadilisha lolote kwangu uwanjani.".

Benin iliinyuka Algeria iliyokuwa na wachezaji wengi nyota katika mechi yao ya hivi majuzi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika na kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi D.

"Tumeicharaza Algeria, bila shaka sisi ni hatari, tuna wachezaji wazuri''.

Alisema kuwa "Kila mmoja anacheza Ulaya sasa kwa hivyo nahisi kuwa tuna timu nzuri, nina matumaini tutafuzu kwa michuano ijayo ya kombe la mataifa ya Afrika."

Les Ecureuils kwa tafsiri ya Kiingereza inamaanisha The Squirrels na jina hilo lilianza kutumiwa miaka ya 1960. Jina hilo lilikuwa la kuashiria taifa dogo lililokuwa linaania kufika kileleni.

Hata hiyo shirikisho la mchezo wa soka nchini Benin linasema muda umewadia kubalisha jina hilo kuambatana na matarajio makubwa ya timu ya taifa.

Hii ni mara ya kwanza Benin kutaka kubadilisha jina la timu ya taifa ya soka baada ya hatua sawia na hiyo kugonga mwamba mwaka 2008.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Benin walikusudia Kuchakuro iwe ishara ya taifa dogo linalopania kujiinua

Benin haijawahi kufuzu kwa kombbe la Dunia lakini imewahi kushiriki mara tatu katika mashindano ya Kombe mataifa ya Afrika miaka ya 2004, 2008 na 2010.

Mechi yao nyingine ya kufuzu kwa kmbe la mataifa itakuwa dhidi ya Gambia Novemba 17.

Taifa Stars na Harambee Stars

Benin haiko pekee katika kutaka kubadilisha jina la timu ya taifa. Nchini Tanzania mwaka 2014 kulikuwa na pendekezo la kubadilisha jina la taifa hilo kutoka Taifa Stars. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitaka pia kubadili rangi za jezi za timu ya taifa.

Rais wa TFF Jamal Malinzi alikuwa ameeleza mapendekezo hayo kama sehemu ya kubadili sura ya timu ya taifa na sifa zake.

Kwa mujibu wake, jina jipya lingeleta hamasa na mwamko mpya na jezi mpya kuonesha miaka 50 imepita sasa ni awamu ya pili ya miaka 50 mingine.

Baadhi wamekuwa wakidai jina Taifa Stars halitishi na limepooza, wakicheza na timu hakuna ule ujasiri tuseme kwa mfano timu zinapokutana na Simba wasioshindwa, yaani Indomitable Lions ya Cameroon.

Juhudi za wakati huo zilizimwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa wakati huo, Juma Nkamia aliyesema bungeni kwamba hakukuwa na haja ya kubadili jina hilo.

"Tumepokea maoni ya TFF kutaka kubadili jezi za timu ya taifa kwa kuwa rangi ya bluu kwenye TV inaleta matatizo. Pia wamependekeza kubadili jina la timu ya taifa. Serikali inaona hakuna haja ya kubadili jina badala yake wajikite katika kubadili mchezo wenyewe," alisema.

Nchini Kenya, kulikuwa na malalamiko sawa. Kwamba jina Harambee Stars halina mvuto. Jina Harambee linatokana na kauli mbiu ya mwanzilishi wa taifa hilo Mzee Jomo Kenyatta yenye maana ya 'Kuvuta Pamoja'.

Timu ya taifa ya Kenya ilianza kufahamika kama Harambee Stars kutokana na tamko la aliyekuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Kandanda Kenya (FKF) Kenneth Matiba mnamo 16 Desemba, 1976.

Baadhi husema kwamba jina hilo halina makali wala mashiko.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Kinayangi Whyvonne (kulia) wa Harambee Stars akishindania mpira na Feisal Salum wa Zanzibar mechi ya Cecafa Machakos nchini Kenya 17 Desemba, 2017

Mwaka jana kuna mhadhiri kwa jina Philip Zeal Chebunet aliwasilisha ombi kwa Bunge kutaka jina hilo libadilishwe akisema kwamba jina hilo limekuwa kwa muda mrefu sana linahusishwa na kushindwa.

Juhudi hizo hazikufua dafu.

Timu za mataifa mengine ya Afrika huitwaje?