Kombe la Carabao: Wasiwasi kuhusu Kevin de Bruyne licha ya ushindi wa Man City dhidi ya Fulham

Kevin de Bruyne sits on the turf after his injury

Chanzo cha picha, Getty Images

Manchester City walifanikiwa kuwalaza Fulham 2-0 kwenye mechi ya Kombe la Ligi iliyochezwa Alhamisi lakini wameingiwa na wasiwasi kuhusu kiungo wao nyota Kevin de Bruyne.

De Bruyne alichechemea na kuondoka uwanjani baada ya kuonekana kuumia dakika tatu kabla ya mechi kumalizika.

Nyota wa mechi hiyo alikuwa kinda Mhispania Brahim Diaz ambaye alifunga bao moja kila kipindi, dakika ya 18 na 65, hayo yakiwa mabao yake ya kwanza kufungia timu kubwa ya Manchester City.

City sasa watakutana na mshindi wa mechi kati ya Leicester na Southampton kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo hufahamika kama Kombe la Carabao.

Mbelgiji De Bruyne mwenye miaka 27 alikuwa ameanza mechi kwa mara yake ya pili pekee msimu huu tangu alipopata jeraha kwenye kano za goti lake la kulia mwezi Agosti.

"Anachunguzwa na madaktari," alisema meneja wa City Pep Guardiola baada ya mechi.

"Hatujafahamu kufikia sasa iwapo hakuna kitu chochote kibaya kimemtendekea au kama ni kitu kibaya."

De Bruyne alikuwa amecheza vyema sana na kuonekana kujituma uwanjani lakini aliondoka uwanjani akiwa anagusa goti lake la kushoto, na moja kwa moja akaelekea chumbani kupokea matibabu.

Viongozi hao wa Ligi ya Premia kwa sasa walikuwa wamefanya mabadiliko 10 kwenye kikosi chao kilicholaza Tottenham Jumatatu lakini bado waliwazidi nguvu Fulham waliotumia kikosi chao cha kwanza, walikuwa na makombora 27 yaliyolenga goli wakilinganishwa na wageni wao waliolenga goli mara tano pekee.

Debi ya Manchester

City watafahamu klabu watakayokutana nayo robo fainali mnamo 27 Novemba mechi kati ya Leicester na Southampton - iliyoahirishwa kutokana na ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha mmiliki wa Leicester Vichai Srivaddhanaprabha na watu wengine wanne wakiondoka uwanjani Jumamosi - itakapochezwa.

Ustadi wa De Bruyne na juhudi zake vilionekana wazi uwanani Etihad na alitamba safu ya kati na kwenye mashambulizi kuhakikisha City wanaidhibiti mechi.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kevin de Bruyne hakucheza kwa miezi miwili msimu huu kutokana na jeraha la goti

Alikuwa amecheza dakika 150 pekee kwa jumla msimu wa 2018-19 kabla ya mechi hiyo na hakuonekana kuwa na uchovu.

Alishambulia mara kwa mara na alionekana kujizatiti kuupata mpira tena kila City walipopokonywa.

Alikabili wapinzani na kushinda mpira mara saba, na akazuia mpira mara tatu.

"Ni kawaida kwa watu kusema mchezaji ameonyesha kiwango cha kuwa stadi zaidi duniani, lakini hautakuwa unaongeza chumvi ukisema kuhusu uchezaji wa De Bruyne," Pat Nevin aliyekuwa akichambua mpira katika BBC Radio 5 alisema.

Huku kukiwa na mechi nyingine tano za kuchezwa Novemba, ambapo miongoni mwake kuna mechi ya debi dhidi ya Manchester United uwanjani Etihad, Guardiola atatumai kwamba De Bruyne hakuumia sana.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Brahim Diaz alikuwa anachezea Manchester City mechi yake ya 14, lakini ilikuwa mara yake ya tatu kuanza mechi

Nini kinafuata?

Mkimbio wa City kucheza mechi tano katika kipindi cha siku 13 utaendelea kwa mechi ya nyumbani Ligi ya Premia dhidi ya Southampton Jumapili.

Watarejea tena uwanani Etihad Stadium Jumatano wakiwa wenyeji wa Shakhtar Donetsk katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Fulham, wanaotafuta ushindi wao wa kwanza ligini tangu 26 Agosti, watarejea kusaka ushindi watakapokuwa wageni wa Huddersfield wanaoshika mkia ligini Jumatatu. Fulham wanashikilia nafasi ya 18 kwenye jedwali.