Manchester United v Young Boys: Kwa nini Jose Mourinho huenda akatembea kwenda Old Trafford mechi ya UEFA

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho amesema atatembea kutoka hotelini kwenda uwanjani kwa mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Young Boys iwapo tatizo la foleni litajirudia.

United walitozwa faini ya euro 15,000 (£13,203) kutokana na kuchelewa kuanza kwa mechi yao na Valencia uwanjani Old Trafford mwezi Oktoba.

Kadhalika, walifika kuchelewa kwa mechi yao ya nyumbani dhidi ya Juventus, ambapo Mournho alilazimika kutembea.

"Taarifa tulizo nazo ni kwamba mambo ni mabaya kuliko wakati huo mwingine," amesema Mourinho.

"Tunakaa katika hoteli iliyo mita kadha tu kutoka uwanjani. Mambo [ya foleni] yasipoimarika, basi nitatembea [kwenda Old Trafford]."

Man Utd wanakabiliwa na shinikizo?

Kando na matatizo ya jinsi ya kufika uwanjani kwa mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, United wamekuwa wakiandikisha matokeo mseto wakiwa uwanja wao wa Old Trafford.

Wameshindwa mechi tatu katika mashindano yote msimu huu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jose Mourinho

Mourinho amepuuzilia mbali madai kwamba huenda wachezaji wanashindwa kuhimili shinikizo za kuchezea nyumbani.

"Kama waihisi presha, basi salia nyumbani utazame mechi kwenye TV," aliongeza.

"Iwapo unahisi presha ya kuchezea nyumbani ambapo watu hujitokeza kukuunga mkono, aisee. Huwa sihisi presha nikiwa nyumbani. Ukaniuliza mimi kama ningelipenda kurudi Bern (Uswizi) au kuchezea nyumbani, daima nitasema kwamba ningependa nyumbani zaidi.

"Ninachokitaka ni timu kuanza vyema mechi, sio kusubiri tu na baadaye kuanza kucheza baada ya kufungwa.

"Pengine mnafikiria kwamba Jose aliwaambia waanze kwa mwendo pole, wacheze bila kujisumbua sana na kutazama jinsi mechi itakavyoendelea. Ni kinyume kabisa. Ninawataka waanze kwa ukali na kushambulia tokea mwanzo."

Majeraha ya Lindelof

Mourinho amethibitisha kwamba mchezaji wa kimataifa wa Sweden Victor Lindelof anatarajiwa kutocheza kwa muda baada ya kuumia akicheza dhidi ya Crystal Palace Jumamosi, mechi ambayo ilimalizika kwa sare tasa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Victor Lindelof ameanza mechi katika mechi saba za karibuni zaidi Manchester United.

Eric Bailly na Luke Shaw wako sawa kucheza hata hivyo.

Beki wa Ivory Coast Bailly hajacheza tangu alipoondolewa uwanjani dakika ya 19 katika mechi ambayo mashetani hao wekundu waliwalaza Newcastle 3-2 mnamo 6 Oktoba.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Eric Bailly

Shaw amekuwa akitumikia marufuku kutokana na kulimbikiza kadi tano za manjano katika ligi za nyumbani.

Beki huyo wa England amekuwa kwenye kikosi cha kuanza mechi katika mechi zote walizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu.

United wakifanikiwa kuandikisha ushindi leo, basi watafuzu kwa hatua ya muondoano iwapo Valencia hawatafanikiwa kuwashinda Juventus mjini Turin.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii