Manchester United v Young Boys UEFA: Mourinho azua vituko tena Old Trafford

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Reuters

Manchester United kwa miezi mingi sasa wamekuwa wakishutumiwa kwa kucheza mchezo usiovutia, na kwa kuandikisha matokeo yasiyo ya kuridhisha sana.

Mashabiki hulalamika kwamba hakuna cha kufurahia, lakini meneja wao anaonekana kufidia hilo kwa vituko vyake.

Mreno huyo alisherehekea bao la ushindi lililofungwa na kiungo wa kati Marouane Fellaini dakika ya 91 kwa kunyanyua kreti ya maji na kuiangusha chini.

Kisha baadaye, alitumia kikao chake na wanahabari kutoa ujumbe kwa wanaompenda na kisha kumtawaza kipa wake "bora zaidi duniani."

Manchester United walikuwa wameonekana kuelekea kuandikisha sare nyingine tasa hadi pale Fellaini alipoufikia mpira wa Romelu Lukaku eneo la hatari uliokuwa umetokana na pasi ya Luke Shaw, akafanikiwa kumzuia mkabaji Loris Benito na kisha kutumbukiza mpira kwenye kona wavuni.

United wamefuzu kwa hatua ya makundi baada ya Juventus kuwalaza Valencia 1-0.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marouane Fellaini alifunga bao dakika ya 91

'Mwajua, niko sahihi'

Kusherehekea. Mwanachama wa bendi ya Nirvana, Kurt Cobain, alifahamika sana kwa kukamilisha matamasha yake wakati mwingine kwa kuvunja gitaa.

Mourinho alielekeza furaha yake na hisia zake kwa chupa za maji.

Haki miliki ya picha Reuters

Hakujawahi kuonekana mtu mwenye machungu hivi kwa chupa za maji Old Trafford tangu Eric Cantona alipoulizwa maoni yake kuhusu mchezaji mwenzake Didier Deschamps.

Mourinho alikosolewa na Rio Ferdinand kwa kituko chake hicho kwenye BT Sport. Ferdinand, ambaye ni beki wa zamani wa Manchester United alidai kwamba Mourinho alifanya hivyo katika jaribio la kufanya kitu cha kugonga vichwa vya habari.

Kama hilo lilikuwa ndilo kusudi, basi alifanikiwa.

Haki miliki ya picha Reuters

Lakini Jose hakubaliani na hilo.

"Wale wanaozungumzia kandanda, si wengi wao ambao wamekuwa uwanjani kama wakufunzi," alisema baada ya mechi.

Haki miliki ya picha Reuters

"Kwa wale wanaozungumzia mtu kuonyesha masikitiko yake akiwa kwenye basi, basi ninaweza kuwaalika waje waketi nami hapo kwenye benchi kama meneja.

"Pengine wanafurahia zaidi kuwa likizoni visiwa vya Barbvados na wanaweza kwenda kwenye runinga na kutumia vifaa hivyo vya kucheza kwenye skrini."

"Hilo halina presha ukilinganisha na kuwa kwenye benchi. Nina uhakika asilimia mia kwamba hakuna meneja yeyote mwenye akili zake anaweza kumkosoa mwenzake kwa vituko alivyovifanya akiwa uwanjani. Kwa wale ambao wanaishi maisha mazuri yasiyo ya presha, ni tofauti."

Mourinho si meneja wa kwanza kuelekeza hisia zake kwa chupa za maji.

Arsene Wenger alifukuzwa uwanjani kwa kupiga teke chupa za maji alipokuwa meneja wa Arsenal walipokuwa wanacheza Old Trafford mwaka 2009.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp naye aliomba radhi baada ya kuangusha chupa chini kwa hasira, baada ya sare ya msimu uliopita kati yao na Arsenal.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Arsene Wenger alipiga chupa teke wakicheza Ligi ya Premia dhidi ya Manchester United Agosti 2009

14 kutoka kwa 14

Mourinho hakuwa tayari kuzungumzia takwimu kuhusu uchezaji wa timu yake msimu huu.

United wanakaribia mkia kwenye Ligi ya Premia kuliko kileleni, na wamefungwa mabao zaidi ya mara nne ukilinganisha na wapinzani wao Manchester City na Liverpool.

Walishindwa kufunga dhidi ya Crystal palace nyumbani wikendi, na mchoro huu wa Michael Caley unaonesha mambo halisi.

Haki miliki ya picha Michael Caley

"Muhimu zaidi kwangu ni kufuzu na kwa baadhi ya watu wanaonipenda, na wanapenda takwimu hizo, nimekuwepo Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya misimu 14 na mara 14 timu zangu zimefuzu hadi hatua ya makundi," alisema Mourinho.

"Msimu ambao sikuwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, nilishinda Europa League."

Mreno huyo anaonekana kufahamu vyema zaidi takwimu kuhusu ufanisi wake.

Timu za Mourinho Jose Mourinho Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
Hatua Misimu
Washindi (x2) 2003-04 & 2009-10
Nusu fainali (x6) 2004-05, 2006-07, 2010-11, 2011-12, 2012-13 & 2013-14
Last 16 (x6) 2005-06, 2008-09, 2014-15, 2015-16, 2017-18 & 2018-19

'Najua anataka kusalia'

Mourinho alimsifia sana kipa wake David de Gea ambaye alitumia ustadi wa hali ya juu kuuzia United kufungwa.

De Gea, 28, mkataba wake Old Trafford unadumu hadi mwisho wa msimu, lakini klabu hiyo inaweza kuuongeza hadi mwaka 2020.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Fellaini amerejelea mtindo wake wa kufunga mabao muhimu mechi ikikaribia kumalizika

"Ni kipa wa kiwango cha juu zaidi duniani; kipa bora zaidi duniani," alisema Mourinho.

"Najua anataka kusalia na wakala wake anataka kufanya atakavyo mchezaji huyo. Bodi inamtaka asalie na tunalifanyia kazi hilo."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii