PSG vs Liverpool: Je, Mbappe na Neymar wataizamisha Liverpool leo?

SADIO MANE Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mshambuliaji hatari wa Liverpool Sadio Mane nae anatarajiwa kushuka dimbani baada ya kupona

Wachezaji wa Liverpool hawaogopi kupambana dhidi ya washambuliaji hatari Neymar na Kylian Mbappe kwa sababu "bila shaka wameshaangalia video zao 500,000 kupitia mtandao waYouTube" amesema kocha Jurgen Klopp.

Washambuliaji hao pacha wa Paris St-Germain (PSG) wanatarajiwa kushuka uwanjani kuwavaa Liverpool baadae leo katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.

Wote wawili waliumia walipokuwa wakizitumikia timu zao za taifa na walikosa mechi ya PSG jumamosi ambapo walishinda 1-0 dhidi ya Toulouse katika ligi kuu ya Ufaransa.

"Ni ngumu zaidi kujiandaa na mchezo ambao wachezaji wangu hawawajui wapinzani wao," amesema Klopp.

"Tunawapatia video lakini kizazi hiki yawezekana tayari wameshatazama video 500,000 YouTube za Mbappe, Neymar na (Edinson) Cavani na wanajua uwezo wao binafsi zaidi ya niwajuavyo mimi.

"Ni lazima wawe na mpira ili wang'are, hivyo itatulazimu tuwakabe."

'Salah ni binaadamu'

Klopp pia anamini mshambuliaji wake hatari raia wa Misri Mohammed Salah amerejea katika ubora wake ili kuwakabili PSG jijini Paris.

Salah, 26, alifunga magoli 42 msimu uliopita lakini hata hivyo amekuwa akijivuta kurejea kwenye makali yake mwanzoni mwa msimu huu baada ya kucheza Kombe la Dunia huku akiwa na maumivu ya bega aliloumia mwezi Mei kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya.

Tayari ameshafunga magoli tisa katika michezo 18 msimu huu, magoli sita kati ya hayo ameyafunga katika mechi saba zilizopita.

"Hata Mo Salah ni binaadamu na anahitaji muda. Kila kitu kipo sawa. Mwili wake umerejea, asilimia 100," amesema Klopp.

Mshambuliaji mwengine hatari wa Liverpool Sadio Mane nae anatarajiwa kushuka dimbani baada ya kuwepo na hofu ya kuwa mgonjwa.

PSG wapo nyuma ya vinara wa kundi hilo la C Liverpool na Napoli kwa alama moja.

Nafasi ya PSG kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza zitayeyuka kwa mwaka mwingine tena iwapo watafungwa na Liverpool na Napoli watashinda dhidi ya Red Star Belgrade.

Liverpool, amabo walifungwa katika fainali ya msimu uliopita na Real Madrid kwa upande wao watafuzu kwenye hatua ya mtoano iwapo watamfunga PSG na Red Star wakifungwa.

Timu zote nne zina nafasi ya kuendelea mbele kabla ya kuingia uwanjani leo, lakini ni timu mbili tu ndizo zitakazosonga mbele.

Liverpool ilishinda mechi ya awali dhidi ya PSG kwa goli la dakika ya 90 liliofungwa na Roberto Firmino katika ushindi wa goli 3-2 kwenye uwanja wa Anfield.

Mada zinazohusiana