AFOTY 2018: Mohammed Salah atwaa tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Mwaka 2018 wa Afrika wa BBC

Mo Salah Haki miliki ya picha Reuters

Mshambuliaji wa timu ya Liverpool na Misri, Mohamed Salah amenyakua kwa mara ya pili mfululizo tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Mwaka wa Afrika wa BBC.

Salah ameshinda tuzo hiyo kwa kuwapiku wachezaji nyota wengine wanne ambao ni Medhi Benatia, Kalidou Koulibaly, Sadio Mane na Thomas Partey.

"Najisikia furaha sana," Salah ameiambia BBC.

"Ningependa kushinda tena mwakani. Ninafuraha sana kunyakua tuzo hii."

Salah ambaye ndiye mchezaji bora wa ligi ya Premia alifunga magoli 44 katika mechi 52 alizocheza na timu ya Liverpool msimu uliopita na kuiwezesha timu hiyo kufika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya.

"Kila wakati najihisi kama nafunga magoli na kuisaidia timu kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi. Hizo ni hisia bora kabisa."

Mchezaji huyo aliifungia magoli mawili Misri katika michuano ya Kombe la Dunia lililofanyika Urusi katikati ya mwaka huu.

BBC ilipokea zaidi ya kura 650,000 mwaka huu kwa ajili ya tuzo hizo. Idadi hiyo ya kura ndiyo ya juu zaidi kuwahi kupatikana.

Salah atakuwa mchezaji wa kwanza kushinda mfululizo tuzo hiyo toka alipofanya hivyo mchezaji wa zamani wa Nigeria Jay-Jay Okocha.

Haki miliki ya picha Reuters

Salah amabaye alishawahi kukipiga na klabu ya Chelsea alisaini mkataba na Liverpool maarufu kama Majogoo ya Jiji kutoka kutoka klabu ya AS Roma ya Italia katika kipindi cha kiangazi cha mwaka 2017.

Salah aliifungia magoli 15 na kutengeneza nafasi kwa mengine 11 katika msimu wake wa mwisho na klabu hiyo yenye maskani yake jiji la Rome, ambapo walimaliza msimu katika nafasi ya pili. Matokeo hayo yalikuwa bora zaidi kwao katika kipindi cha miaka saba.

Alianza msimu wake na Liverpool kwa kuwashangaza wengi pale alipofunga magoli 19 katika mechi 24 za awali alizoshiriki.

Image caption Salah alinyakua tuzo hiyo kwa mwaka 2017 pia

Aliendelea kuvunja rekodi kwa kufunga magoli 31 katika mechi 38 za msimu wa Premia ligi na kufanya awe sawa na Luis Suarez aliyefikisha idadi hiyo mwaka 2013-14, Cristiano Ronaldo mwaka 2007-08 na Alan Shearer mwaka 1995-96.

Mohamed Barakat (2005) na Mohamed Aboutrika (2008) ni Wamisri wengine waliowahi kushinda tuzo.