Jose Mourinho: Manchester United wamfuta kazi meneja wao baada ya kushindwa na Liverpool Jumapili, kwa Paul Pogba kejeli

Jose Mourinho Haki miliki ya picha PA

Jose Mourinho amefutwa kazi wadhifa wake kama meneja wa Manchester United.

Klabu hiyo imetangaza kwamba ameondoka katika klabu hiyo mara moja.

"Klabu hii ingependa kumshukuru Jose kwa kazi yake kipindi ambacho amekuwepo Manchester United na inamtakia kila la heri siku za usoni."

Meneja mpya wa muda atateuliwa kuongoza klabu hiyo hadi mwisho wa msimu, huku klabu hiyo ikiendelea na mchakato wa kumtafuta meneja mpya wa kudumu."

Mourinho, 55, amekuwa Old Trafford kwa miaka miwili unusu pekee, baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Mholanzi Louis van Gaal mwezi Mei mwaka 2016.

Mreno huyo alikuwa ametia saini kandarasi mpya mnamo mwezi Januari ambayo iliimarisha mafao na mahitaji yake ya kikazi mbali na kumuongezea kandarasi yake hadi mwaka 2020.

Alishinda Kombe la Ligi na Europa League akiwa Manchester United lakini kwa sasa wamo alama 19 nyuma ya viongozi wa Ligi Kuu ya England kwa sasa, ambao ni Liverpool waliowachapa 3-1 Jumapili.

Hali ya United kwa sasa, ambapo wamezoa alama 26 pekee baada ya kucheza mechi 17 za msimu Ligi ya Premia ndiyo mbaya zaidi katika historia ya klabu hiyo hatua kama ya sasa tangu msimu wa 1990-91.

Haki miliki ya picha Reuters

Wamo alama 11 nyuma ya klabu nne za kwanza kwenye jedwali, ambazo hufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Wanakaribia zaidi eneo la kushushwa daraja kuliko kileleni.

Yamkini mwezi Desemba si wa bahati kwa Mreno huyo, alifutwa kazi tarehe 17 Desemba mwaka 2015 na klabu ya Chelsea baada ya klabu hiyo kuandikisha msururu wa matokeo mabaya.

The Blues walikuwa wameshinda Ligi ya Premia msimu uliotangulia lakini msimu huo mambo yakawaendea kinyume, na walikuwa alama moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja ligini.

Kejeli za Paul Pogba

Paul Pogba ambaye ameonekana kuzozana na Mourinho siku za karibuni na amekuwa hachezeshwi tena katika kikosi cha kuanza mechi ameandika ujumbe ulioonekana kuwa wa kejeli kwenye Twitter kisha akaufuta.

Haki miliki ya picha TWITTER
Image caption Pogba amepakia ujumbe huu Twitter kisha akaufuta muda mfupi baadaye

Mourinho amezozana kwa muda na Mfaransa huyo aliyenunuliwa kwa bei iliyovunja rekodi ya klabu hiyo ya £89m.

Pogba alikuwa benchi na hakuchezeshwa katika mechi hiyo ambayo walichapwa na Liverpool uwanjani Anfield Jumapili.

Baada ya kutoka sare 1-1 na Wolves wiki chache zilizopita, Pogba alisema angependa United wawe wakishambulia na kushambulia na kushambulia wakiwa nyumbani.

Hilo lilimfanya Mourinho kudai kwamba Mfaransa huyo hangekuwa nahodha msaidizi wa klabu hiyo tena.

Pogba alimjibu kwamba hahitaji kitambaa hicho cha nahodha.

Oktoba, zilitokea taarifa kwamba Mourinho huenda angefutwa kabla ya mechi yao dhidi ya Newcastle iwapo wangeshindwa.

Lakini baada yakuwa nyuma 2-0, walijikwamua na kushinda 3-2 na meneja huyo wa zamani wa Chelsea, Inter Milan na Real Madrid akapata muda zaidi.

Wakala wa Mourinho, Jorge Mendes alijaribu kutuliza wasiwasi mapema Desemba kwa kuchukua hatua isiyo ya kawaida ya kutoa taarifa rasmi kusema Mourinho ana furaha sana, na kwamba amejitolea kuendelea kuhudumu katika klabu hiyo.

Lakini hata licha ya kufuzu kwa hatua ya muondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambapo wamepangwa kucheza na Paris St-Germain ya Ufaransa, wameshinda mechi moja pekee ligini kati ya sita walizocheza karibuni.

Kufutwa kwa Mourinho kunaendeleza historia yake ya kutomaliza misimu mitatu mfululizo katika klabu moja.

Ni wakati mmoja tu ambapo alifanikiwa kuhudumu msimu wa nne, lakini aliondoka Chelsea 17 Desemba 2015 wakati wa kipindi chake cha pili Stamford Bridge.

Nani atamrithi Mourinho?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Pochettino, Simeone na Zidane

Manchester United wamedokeza kwamba watamteua meneja mpya wa muda.

Lakini hatakuwa meneja msaidizi Michael Carrick au meneja wa akademi Nicky Butt.

Atakuwa ni mtu kutoka nje ya klabu hiyo, lakini hatakuwa meneja wa zamani wa Arsenal Arsene Wenger.

Baadhi wanamzungumzia Zinedine Zidane aliyekuwa meneja wa Real Madrid.

Yupo pia meneja wa zamani wa Chelsea Mwitaliano Antonio Conte.

Yupo pia meneja wa Atletico Madrid Diego Simeone na meneja wa sasa wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino.

Mameneja wa awali Manchester United tangu 1980

Kipindi Meneja
01/07/2016 - 18/12/2018 José Mourinho
01/07/2014 - 23/05/2016 Louis van Gaal
22/04/2014 - 30/06/2014 Ryan Giggs
01/07/2013 - 21/04/2014 David Moyes
06/11/1986 - 30/06/2013 Alex Ferguson
01/06/1981 - 06/11/1986 Ron Atkinson

Rekodi ya mameneja Man Utd

Meneja Mechi Kushinda Sare Kushindwa Mabao waliyofunga Mabao waliyofungwa % ya ushindi
Jose Mourinho 144 84 32 28 243 117 58.33%
Alex Ferguson 1,500 895 338 267 2,769 1,365 59.67%
David Moyes 51 27 9 15 86 54 52.94%
Louis van Gaal 103 54 25 24 158 98 52.43%

Unaweza kusoma pia:

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii