Manchester United: Ole Gunnar Solskjaer ateuliwa kuongoza Mashetani Wekundu baada ya Mourinho kutimuliwa, kusaidiwa na Mike Phelan

Ole Gunnar Solskjaer Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ole Gunnar Solskjaer

Manchester United wamethibitisha kumteua nyota wao wa zamani Ole Gunnar Solskjaer kuwa kocha wa muda wa klabu hiyo mpaka mwisho wa msimu.

Taarifa rasmi imetolewa na klabu hiyo baada ya kuvuja mapema. Taarifa ya awali iliyokuwa imewekwa kwenye tovuti ya klabu hiyo ilikuwa imesema mshambuliaji huyo wa zamani wa United ni "kocha wetu wa muda". Taarifa hiyo hata hivyo ilifutwa baadae.

Lakini sasa taarifa rasmi imetolewa.

Raia huyo wa Norway atachukua mikoba ya Jose Mourinho ambaye alifutwa kazi jana Jumanne.

Manchester United wamesema Solskjær atachukua usukani kwenye timu kuu ya United mara moja.

"Ataendelea kuhudumu huku klau ikiendelea na mchakato wa kumtafuta meneja mpya wa kudumu. Atakuwa anafanya kazi na mkufunzi mpya wa timu kuu Mike Phelan, akisaidiana na Michael Carrick na Kieran McKenna."

"Manchester United wamo ndani ya moyo wangu na nafurahia sana kurejea katika wadhifa huu. Nasubiri kwa hamu kufanya kazi na kikosi cha wachezaji wenye vipaji tulio nao, wafanyakazi na kila mtu katika klabu hii," Solskjær amenukuliwa kwenye taarifa ya klabu hiyo.

Makamu mwenyekiti mtendaji wa Man Utd Ed Woodward amesema wana imani kwamba Solskjær na Mike Phelan watawaunganisha wachezaji na mashabiki klabu hiyo inapojiandaa kwa nusu iliyosalia ya msimu.

Solskjaer ni nani?

Solskjaer, mwenye miaka 45 sasa, ameifungia United magoli 126 katika misimu 11 chini ya kocha Sir Alex Ferguson.

Pia alishinda makombe sita ya ligi ya Premia, mawili ya FA na moja la Klabu Bingwa Ulaya.

Kwa sasa anafundisha klabu ya Norway ya Molde lakini msimu wao wa mwaka 2018 umesitishwa kupisha majira ya baridi kali na mechi zitarejea mwezi Machi mwakani.

Video inayomuonesha Solskjaer akifunga goli la ushindi katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich mwaka 1999, iliwekwa kwenye tovuti ya United na kuambatanishwa na maelezo kuwa: "Solskjaer anakuwa kocha wetu wa muda, misimu 20 baada ya kushinda makombe matatu kwa mpigo na lile goli lake katika (uwanja wa) Camp Nou..."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sir Alex Ferguson na Solskjaer baada ya kushinda fainali ya Klabu Bingwa Ulaya 1999 dhidi ya Bayern Munich

Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg alipokea taarifa hiyo kwa furaha na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter: "Siku njema kwa mpira wa Norway. Nakutakia mema katika kuongoza Mashetani Wekundu." Hata hivyo aliufuta ujumbe huo baadae.

Mechi ya kwanza ya Solskjaer itakuwa dhidi ya Cardiff City siku ya Jumamosi. Kocha huyo aliifundisha Cardiff hapo awali na kushuka nao daraja mwaka 2014.

United wanatarajiwa kumchagua kocha mpya mwisho wa msimu. Tayari majina matatu ya Zinedine Zidane na Waagerntina wawili Diego Simeone na Mauricio Pochettino yamekuwa yakipigiwa upatu.

Mada zinazohusiana