Callum Wilson: Bournemouth na Chelsea wavutania mchezaji anayechezea timu ya taifa ya England

Callum Wilson Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa England Callum Wilson anayechezea klabu ya Bournemouth amejipata akizozaniwa na klabu yake na klabu ya Chelsea kutokana na uchezaji wake mzuri.

Chelsea wamepungukiwa na washambuliaji na hawajawa na washambuliaji wa kutegemewa sana tangu kuondoka kwa Diego Costa.

Alvaro Morata alijiunga nao baada ya Costa kuondoka lakini amelaumiwa kwa kutomakinika vyema mbele ya lango. Morata kwa sasa anauguza jeraha na mshambuliaji pekee aliye sawa kucheza ni Mfaransa Oliver Giroud.

Wilson, 27, alicheza katika mechi ambayo walilazwa 1-0 na Chelsea katika robofainali ya Kombe la Carabao Jumatano.

Meneja wa klabu yake Eddie Howe amelazimika kujitokeza kusisitiza kwamba hatauzwa dirisha la kuhama wachezaji litakapofunguliwa Januari.

Kabla ya mechi kuanza, mkufunzi mkuu msaidizi wa Chelsea Gianfranco Zola alikuwa amesema kwamba Chelsea wanamfuatilia kwa karibu nyota huyo, sawa na "klabu nyingine nyingi".

"Callum ni mchezaji wetu, na amejitolea, tena sana kutuchezea. Nafikiri mngeweza kubaini hilo katika uchezaji wake," amesema Howe.

Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wowote wa Bournemouth kumuuza Januari, Howe aliongeza: "Sio kwa mtazamo wangu, hapana."

Wilson alikaribia sana kufunga katika mechi hiyo iliyochezewa Stamford Bridge lakini kombora lake la dakika ya 15 lilikosa goli kidogo tu.

Klabu yake ilipoteza nafasi ya kufika nusufainali ya michuano ya kushindania kombe kwa mara ya kwanza katika hisoria yao.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Callum Wilson alifunga mabao manane Ligi ya Premia msimu wa 2017-18 na msimu huu tayari amefikia idadi hiyo

Amefunga mabao tisa katika mechi 19 alizocheza mashindano yote msimu huu na pia alifunga alipochezea timu ya taifa ya England mara ya kwanza dhidi ya Marekani mwezi Novemba.

Zola anaamini kwamba mshambuliaji huyo aliyejiunga na Bournemouth kwa £3m kutoka Coventry City mwaka 2014, anaweza kufanikiwa sana katika soka.

"Ana nguvu sana, kasi na anaweza kujiweka sawa vyema kufunga," aliongeza Zola.

"Nampenda kwa sababu kwa mipira ya kichwa ni mzuri sana pia, jambo ambalo ni zuri sana [kwa mshambuliaji], lakini sitaki kumzungumzia sana."

"Anafanya vyema sana na nampongeza na kufurahia ufanisi huo wake.

Chelsea v Tottenham Hotspur, Manchester City v Burton Albion

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Meneja wa Burton Nigel Clough aliichezea Manchester City kati ya 1996 na 1998

Mabingwa watetezi Manchester City wamepangiwa kukutana na klabu ya League One ya Burton katika nusufainali ya Kombe la Carabao.

Tottenham watakutana na Chelsea, na mechi hizo zitachezwa wiki zinazoanza 7 na 21 Januari.

Kutakuwa na mechi ya kwanza na marudiano, ambapo City na Spurs wataanza kwa kucheza nyumbani.

Ni nusufainali ya kwanza kuu kwa Burton, ambao wamekuwa wakicheza Kombe la EFL kwa miaka 10 pekee.

Walishinda Ligi ya Taifa mwaka 2009.

Tottenham, ambao bado hawajashinda kombe chini ya Mauricio Pochettino, walifuzu kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Arsenal, Chelsea, nao na meneja wao Maurizio Sarri ambaye pia hajashinda kombe kubwa wakalaza Bournemouth 1-0.

Spurs walilaza Chelsea 3-1 Ligi ya Premia mwezi Novemba.

Mada zinazohusiana