Pep Guardiola: Liverpool huenda ndio bora zaidi duniani kwa sasa, asema mkufunzi wa Man City

Pep Guardiola

Pep Guardiola anasema kuwa Manchester City lazima ikubali kwamba wapinzani wake wakuu katika ligi ya Uingereza Liverpool wanaweza kuwa timu bora zaidi duniani kwa sasa.

Mabingwa watetezi City , ambao waliishinda Southampton , wanashiriki katika mechi ya siku ya Alhamisi dhidi ya Liverpool wakiwa alama saba nyuma ya viongozi hao wa ligi.

''Tofauti ni kwamba timu ile nyegine ni nzuri, Guardiola aliambia BBC Sport. ''Liverpool nadhani ndio timu bora zaidi Ulaya ama hata ulimwenguni kwa sasa na wako katika hali nzuri''.

Huku City ikiwa imeshindwa mara kadhaa dhidi ya Chelsea, Crystal Palace na Leicester mwezi Disemba , Liverpool imeshinda mechi zake zote saba za ligi walizocheza.

Walimaliza mwaka 2018 kwa bashasha baada ya kuifunga Arsenal 5-1 katika uwanja wa Anfield na hivyobasi kupanda kwa alama 10 dhidi ya City kwa muda.

Akizungumza kuhusu uwezo wa Liverpool, Guardiola aliongezea: ''Lazima ukubali. Kitu tunachoweza kufanya ni kuendelea na kazi yetu na baada ya hilo tutaona''.

Ikiongezea utawala wao katika ligi, Liverpool waliishinda City katika kombe la vilabu bingwa katika mkondo wa robo fainali msimu uliopita.

Iwapo Liverpool itashinda siku ya Alhamisi wataimarisha alama zao 10 juu ya jedwali la ligi na wanapigiwa upatu kushinda taji la ligi tangu 1990.

Nahodha wa City Vincent Kompany alisema kuwa mechi dhidi ya viongozi hao wa ligi ni baadhi ya mechi ''unazotaka kucheza''.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii