Jurgen Klopp: Vincent Kompany alifaa kadi nyekundu ushindi wa Man City dhidi ya Liverpool

Mohamed Salah Haki miliki ya picha Getty Images

Jurgen Klopp anaamini nahodha wa Manchester City Vincent Kompany alifaa kupewa kadi nyekundu wakati wa mechi ambayo Liverpool walilazwa 2-1 uwanjani Etihad.

Kompany alionyeshwa tu kadi ya manjano kwa kumchezea visivyo mshambuliaji wa Liverpool kutoka Misri Mohamed Salah dakika ya 32.

Mchezaji huyo wa Ubelgiji alimkaba Mo Salah kwa kuruka miguu yake yote ikiwa hewani kana kwamba anateleza. Alimgonga Salah kwenye kifundo chake cha mguu.

Leroy Sane alifunga bao la ushindi dakika ya 72 na kupunguza uongozi wa Liverpool hadi alama nne.

Kompany aliondolewa uwanjani dakika ya 88 na nafasi yake akaingia Nicolas Otamendi.

"Nampenda sana Vincent Kompany lakini inakuwaje kwamba hiyo si kadi nyekundu?" Klopp alishangaa baada ya mechi.

"Ndiye mtu wa mwisho safu ya ulinzi anapomkabili. Akamgonga Mo vyema, basi hataweza kucheza tena msimu huu. Sio rahisi kwa mwamuzi na huenda hakuona nilivyoona mimi."

Kompany alitofautiana na tathmini ya Klopp kuhusu tukio hilo lililotokea mambo yakiwa 0-0.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Kompany alionyeshwa kadi yake ya tano ya manjano akiwa na jezi ya Manchester City

"Nilifikiri nilikaba vyema, sivyo? Niliupata mpira, na kiasi kidogo nikampata yeye. Lakini hakukuwa na nia mbaya," Mbelgiji huyo alisema.

"Sikumuumiza. Ilikuwa ni nimkabili au nimwache aende akafunge."

Klopp alisema ni kweli timu yake haikucheza vyema sana lakini kwa kiasi fulani bahati haikusimama.

Haki miliki ya picha Getty Images

Sadio Mane wakati mmoja aliugonga mlingoti wa goli kwa kombora na John Stones akababaisha akijaribu kuuondoa mpira lakini akafanikiwa kuutoa kabla haujavuka mstari.

"Matarajio yetu yalikuwa makubwa. Tunaweza kucheza vyema zaidi. Ni lazima uichukulie mechi ilivyo. Hauwezi kutawala wakati wote," aliongeza.

"Kulikuwa na presha sana. Ilikuwa mechi kali na ya kasi. Tulikosa bahati nyakati muhimu za kutaka kufunga bao. Tulikosa bahati zaidi ya City, ninaweza kusema hivyo.

Haki miliki ya picha Reuters

Kushindwa kwa Liverpool mara ya kwanza Ligi ya Premia msimu huu kumefuta matumaini yao kwamba wangeweza kuiga ufanisi wa Arsenal wa kumaliza msimu bila kushindwa msimu wa 2004.

Image caption Liverpool wangekuwa alama 10 mbele ya Manchester City kama wangeshinda mechi hiyo Etihad

Lakini Klopp amesisitiza kwamba kuwa na alama nne mbele ya mabingwa hao watetezi ni nafasi nzuri sana, na bado wana matumaini ya kushinda taji lao la kwanza la ligi tangu 1990.

"Iwapo mtu angeniambia kwamba baada ya mechi zote mbili dhidi ya Man City tungekuwa alama nne juu, ningelipa pesa," alisema Klopp.

"Tunataka kumaliza msimu vyema kabisa iwezekanavyo na tuko katika nafasi nzuri.

"Tayari nimewaambia vijana wangu kwamba ni sawa. Tulishindwa, lakini hilo ni la kutarajiwa. Usiku huu haikuwa vyema lakini si kwamba ndilo tatizo kubwa zaidi."

Nini kinafuata

Ni mechi za Kombe la FA sasa Manchester City wakiwa wenyeji wa Rotherham Jumapili nao Liverpool wawe wageni wa Wolves Jumatatu.

Mada zinazohusiana