Dennis Oliech: Nahodha wa zamani wa Harambee Stars ya Kenya aeleza sababu ya kurejea kuchezea Gor Mahia

Auxerre's Kenyan forward Dennis Oliech runs with the ball during the French L1 football match Auxerre vs Caen, on September 17, 2011 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Dennis Oliech aliwahi kuichezea Auxerre ya Ufaransa

Mchezaji nyota wa kandanda wa Kenya Dennis Oliech ameeleza miongoni mwa sababu zilizochangia kurudi kwake uwanjani baada ya kutangaza amestaafu miaka mitatu iliyopita.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Oliech anasema amerudi mpirani kwa sababu anaupenda na umri wake unamruhusu acheze kandanda kwa miaka mingine minne na zaidi.

"Kuna wachezaji huendelea hadi miaka 37.Mimi hapa niko miaka 32 kwa hivyo nimeamua nina uwezo wa kucheza kandanda bado kwa miaka kama mitatu-minne hivi. Hali yangu kimwili ni nzuri maanake nimekua nacheza katika mechi za mtaani uwanja wa Woodley kila Jumatatu.

"Sikuwa nimeacha mpira kabisa ndio nikaona siwezi kustaafu kama wakati haujafika. Nilipomaliza kuichezea Dubai Sports Club mwaka wa 2015 nilitaka kurudi Ulaya lakini haikua rahisi ndio nikaenda kwa majaribio na Free State huko Afrika Kusini nikapita lakini walipobadilisha kocha mambo yakawa magumu. Hiyo ilikua mwezi Mei mwaka jana. Kutoka hapo nikaamua nijiunge na Gor Mahia.''

Oliech alirudi uwanjani rasmi wikendi iliyopita wakati Gor Mahia ilipoenda sare ya bao 1-1 na Mathare United. Aliingia dakika 15 za mwisho.

"Ndio mwanzo huo kisha mechi ijayo nitaanza nione kama naweza kucheza dakika arobaini na tano halafu dakika sitini na hatimaye nicheze dakika zote tisini. Nikipata kama wiki zingine mbili za mazoezi nitakua sawa kabisa. Nia yangu kubwa ni kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Kenya niiwezeshe Gor Mahia ihifadhi ubingwa wa ligi. Napanga kufunga mabao 25 ama zaidi yakiwa pamoja na ya penalti pia.''

Kwa nini Gor Mahia?

Mbona akaamua kujiunga na Gor Mahia, na sio kilabu nyingine nchini Kenya?

"Ndugu zangu wakubwa wamepitia Gor nami nimeonelea niichezee kilabu hii kabla sijastaafu kabisa. Sababu nyingine ni kwamba kuna wachezaji watano hapo nilikua nao timu ya taifa Harambee Stars baadhi yao ni George 'Blackberry' Odhiambo na Francis Kahata. Hawa wanaelewa mchezo wangu vizuri sana nitategemea wanipe mipira mizuri ya kufunga kama wachezaji wa kiungo cha kati.''

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Oliech akimwandama Tony Maweye wa Uganda mechi ya kufuzu kwa AFCON mwaka 2010

Oliech anasema amepokelewa vizuri na wachezaji wenzake, na wala hatajichukua kuwa spesheli zaidi ya wengine.

"Sote tukiwa kwa timu tuko sawa hakuna kujichukulia kwamba mimi ni wa maana zaidi ya wachezaji wengine,'' anasema Oliech, na kuongeza: "Kama ni kuoga tunaoga sote pamoja na kula pamoja na kucheka pamoja.''

Amerejea kutafuta pesa?

Oliech alianza kucheza kandanda ya kulipwa na kilabu ya Al Arabi kati ya mwaka 2003-2005 kisha akajiunga na Nantes, Auxerre na Ajaccio zote za Ufaransa na hatimaye akahamia Dubai Sports Club mwaka wa 2015.

Gor Mahia itakua inamlipa Oliech mshahara wa $3,500 (Shillingi 350,000 za Kenya) kila mwezi ambao ndio mshahari wa juu zadi katika ligi kuu ya kandanda ya Kenya.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Dennis Oliech akishindania mpira na beki wa Nantes Kevin Das Neves mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa mwaka 2008

Je, Oliech anasemaje kuhusu mshahara wake huo:``Kwanza nawashukuru maafisa wa Gor Mahia kwa kunikaribisha vizuri na kunilipa mshahara unaofaa. Napenda kusema wazi kwamba sikurudi mpirani kwa sababu ya pesa ila ni mapenzi yangu ya kusakata boli. Nikilinganisha na zile nimelipwa huko Ulaya hizi ni pesa ndogo sana. Nia yangu si pesa ni kucheza kandanda.

"Kupitia ndugu zangu wakubwa wamenisaidia nikawekeza kwenye biashara za vyakula, nikanunua ardhi na nyumba kadhaa kwa hivyo sina shida. Lakini nashukuru sana Gor Mahia kwa wanachonipa, kama ningetaka ningelipwa zaidi ya milioni moja kila mwezi lakini ninaelewa hali ya nyumbani."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii