Timu ya Mwaka 2018 ya Uefa chaguo la mashabiki: Kikosi cha wachezaji 11 bora zaidi Ulaya, Messi afunga bao la 400

Lionel Messi, Cristiano Ronaldo & Kylian Mbappe Haki miliki ya picha Getty Images

England walifika nusu fainali katika Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018, lakini hakuna mchezaji hata mmoja wa timu hiyo ya taifa aliyejumuishwa kwenye kikosi bora cha wachezaji 11 Ulaya, chaguo la mashabiki kwa mwaka huo.

Ingawa kuna wachezaji watatu wanaocheza Ligi ya Premia kwenye kikosi hicho, hata nahodha wa England Harry Kane aliyeshinda tuzo ya mfungaji bora zaidi Urusi, hajajumuishwa.

Kiungo wa Liverpool Virgil van Dijk na wachezaji wawili wa Chelsea N'Golo Kante na Eden Hazard wamo kwenye kikosi hicho cha wachezaji XI.

Cristiano Ronaldo ni miongoni mwao, ambapo amejumuishwa kwa mara ya 13 sasa, na kuwa mchezaji aliyejumuishwa mara nyingi zaidi.

Mshambuliaji huyo wa Ureno ambaye sasa huchezea Juventus ya Italia, aliisaidia klabu yake ya zamani Real Madrid kushinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia mjini Kiev, Ukraine mwezi Mei ambapo waliwalaza Liverpool.

Mchezaji mwenzake wa zamani Madrid, Luka Modric, ambaye alitamba sana akichezea Croatia na kuwasaidia kufika fainali Kombe la Dunia, ndiye mchezaji aliyepigiwa kura nyingi zaidi na mashabiki - kura 115,440.

Nyota wa Barcelona Lionel Messi amejumuishwa kwa mara ya kumi katika kikosi hicho.

Wageni wapya kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji wa Paris St-Germain Kylian Mbappe pamoja na Marc-Andre ter Stegen, Van Dijk, Raphael Varane, na Kante.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Harry Kane alikuwa mfungaji bora Kombe la Dunia 2018

Kikosi hicho, ambacho kina wachezaji watano kutoka Real Madrid, kiliandaliwa kwa kutumia kura milioni mbili za mashabiki waliojisajili na Uefa.

Uefa.com XI:

 1. Marc-Andre ter Stegen (FC Barcelona & Ujerumani)
 2. Sergio Ramos (Real Madrid CF & Uhispania)
 3. Virgil van Dijk (Liverpool FC & Uholanzi)
 4. Raphael Varane (Real Madrid CF & Ufaransa)
 5. Marcelo (Real Madrid CF & Brazil)
 6. N'Golo Kante (Chelsea FC & Ufaransa)
 7. Luka Modric (Real Madrid CF & Croatia)
 8. Eden Hazard (Chelsea FC & Ubelgiji)
 9. Kylian Mbappe (Paris Saint-Germain & Ufaransa)
 10. Cristiano Ronaldo (Real Madrid CF/Juventus & Ureno)
 11. Lionel Messi (FC Barcelona & Argentina)

Messi afunga bao lake la 400 La Liga

Hayo yakijiri, Lionel Messi alifunga bao lake la 400 La Liga na kuwasaidia Barcelona kuwalaza Eibar 3-0 uwanjani Nou Camp, na kurejesha mwanya wa alama tano kileleni.

Raia huyo wa Argentina ambaye ndiye mfungaji mabao mengi zaidi katika historia La Liga alifunga bao lake katika mechi yake ya 435.

Messi, ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao 400 katika moja ya ligi tano za Ulaya, na ndiye mchezaji wa pili kufunga mabao 400 katika mechi za ligi tano kuu Ulaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Messi alifungia Barcelona bao lao la pili mechi hiyo ambayo walishinda 3-0

Huyo mwingine ni Cristiano Ronaldo ambaye amefunga mabao 409 ligini baada ya kucheza mechi 507, lakini mabao yake ameyafunga England, Uhispania na Italia. Mabao ya Messi yote ni katika La Liga.

Bao hilo lake dhidi ya Eibar lina maana kuwa Messi amefikisha magoli 400 mechi 63 mapema kuliko Ronaldo.

Aidha, imefunguza zaidi mwanya kati yake na wafungaji wengine bora katika historia Uhispania, ambapo anafuatwa na Ronaldo mwenye mabao 311 kutoka mechi 292 akiwa Madrid lakini ambaye sasa anachezea Juventus.

Kuna pia Telmo Zarra, ambaye amefunga mabao 251 La Liga ambaye ndiye anayeshikilia nafasi ya tatu

Jedwali la msimamo wa ligi La Liga kufikia 14 Januari, 2019

Nambari Klabu Mechi Mabao Alama
1 Barcelona 19 33 43
2 Atl Madrid 19 14 38
3 Sevilla 19 11 33
4 Real Madrid 19 4 33
5 Alavés 19 3 32
6 Getafe 19 5 28
7 Real Betis 19 -1 26
8 Girona 19 -2 24
9 Espanyol 18 -5 24
10 Valencia 19 0 23
11 Levante 19 -5 23
12 Real Sociedad 18 0 22
13 Leganés 19 -4 22
14 Real Valladolid 19 -4 22
15 Ath Bilbao 19 -5 22
16 Eibar 19 -7 22
17 Celta Vigo 19 -1 21
18 Rayo Vallecano 19 -12 19
19 Villarreal 19 -5 17
20 Huesca 19 -19 11

Mada zinazohusiana