Kombe la SportPesa: Yanga na Singida zapoteza kwa Kariobangi Sharks na Bandari kutoka Kenya

Wachezaji wa timu ya Yanga kutoka Tanzania

Timu mbili za Kenya Bandari Fc na Kariobangi Sharks zimefuzu katika nusu fainali ya kombe la SportPesa baada ya kuwabwaga mabingwa wa ligi ya Tanzania Yanga pamoja na Singida United.

Duke Abuya alifunga magoli mawili huku klabu ya Kariobangi Sharks kutoka Kenya ikiwalaza mabingwa wa ligi ya Tanzania Yanga 3-1 katika robo fainali ya pili ya kombe la SportsPesa katika uwanja wa Kitaifa nchini humo.

George Abege pia aliifungia timu hiyo ya Kenya ambayo inashiriki katika mashindano hayo kwa mara ya pili.

Kulikuwa na vurugu awali baada ya Kipa wa kariobangi Sharks John Oyemba kushambuliwa na wachezaji wa Yanga baada ya kukataa kuwapatia mpira baada ya bao lao la pili.

Haki miliki ya picha Bandari FC

Sharks sasa watapambana na Wakenya wengine Bandari katika nusu fainali.

Bandari iliilaza timu ya nyumbani ya Singida United 1-0 katika nusu fainali ya kwanza.

Bao la mkwaju wa penalti la William Wadri kunako dakika ya 66 ndio lililoleta tofauti kati ya timu hizo mbili na wana Bandari hao ambao wanashiriki katika michuano hiyo kwa mara ya kwanza sasa watakabiliana na wapinzani wao wa nyumbani.

Wakenya hao walikabidhiwa mkwaju huo wa penalti baada ya beki wa siku nyingi wa timu ya Singida Boniface Maganga kuunawa mpira langoni kufuatia krosi iliopigwa na Moses Mudavadi.

''Nafurahia sana na nashkuru mungu kwa ushindi huu, lakini pia nataka kumwambia mkufunzi mwenzangu wa Singida kukubali kushindwa''.

''Lengo letu sasa ni kuangazia nusu fainali'', alisema kocha wa Bandari Bernard Mwalala.

Kipindi cha kwanza cha mechi kiliisha kwa sare tasa, lakini haikuwa kutoshindwa kwa timu hizo mbili kufanya mashambulizi.

Dhidi ya timu inayoorodheshwa ya 15 katika ligi ya Premia ya Tanzania, Washambuliaji wa Bandari Wycliffe Ochomo na Darius Msagha walitekeleza mashambulizi mengi lakini hawakuwa na bahati .

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii