Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) lawatoa kifungoni wanamuziki Diamond Platnumz na Rayvany

Diamond Platnumz na Rayvanny Haki miliki ya picha DiamondPlatnumz Instagram

Mamlaka nchini Tanzania zimewafungulia wasanii nyota wawili wa muziki Diamond Platnumz na Rayvany ambao walifungiwa kwa muda usiojulikana kwa kutumbuiza kibao kilichofungiwa.

Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) limetangaza jana kuwa wasanii hao ambao walifungiwa mwishoni mwa mwaka jana wapo huru kuendelea na kazi zao za sanaa. Uamuzi wa Basata ulifuatia kitendo cha wasanii hao kutumbuiza jukwaani kibao kilichopigwa marufuku na mamlaka cha Mwanza.

Kwa mujibu wa Basata, kibao cha Mwanza "kinaenda kinyume cha maadili na kuhamasisha ngono". Mwimbo huo ulifungiwa rasmi Novemba 12 lakini wasanii hao wakautumbuiza kwenye tamasha la Wasafi Festival Jijini Mwanza mwezi uliopita. Tamasha hilo pia lilipigwa marufuku.

Taarifa iliyotolewa Jumanne jioni na Basata imeeleza kuwa wawili hao wametolewa kifungoni baada ya "kupokea maombi kadhaa ya kukiri kosa na kuomba msamaha kutoka kwa wasanii tajwa na kampuni ya Wasafi Company Limited (WCB)."

Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji wa Basata,Godfrey Mngereza, baada ya kupokea maombi hayo na kuzingatia jukumu la baraza hilo la "kusimamia, kuendeleza na kukuza kazi za wasaniina sekta ya sanaa nchini, Baraza limeamua kuwaruhusu wasanii tajwa kuendelea na shughuli za sanaa."

Hata hivyo, Basata imetahadharisha kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa wasanii hao na WCB kwa ujumla ili kuhakikisha wanazingatia maadili, sheria na kanuni.

Wasnii hao wameandika kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii kulishukuru baraza hilo: "Sanaa ni kazi, tuipende, tuilinde na Kuithamini...HAPPY INDEPENDECE VANNY BOY," ameandika Diamond Platnumz.

Mwezi Disemba wakati Basata ikiwaangushia rungu wasanii hao ilidai kuwa: "Baraza limefikia maamuzi ya kuwafungia rasmi kutokana na wasanii hawa kuendelea kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili uliokithiri unaofanywa na waandaaji wa Tamasha la Wasafi 2018, chini ya uongozi wake Diamond Platnumz," taarifa ya Basata ambayo ilitiwa saini na Onesmo Kayanda kwa niaba ya Katibu Mtendaji ilisema.

Wasanaii hao pia waliomba mamlaka radhi na kuahidi kuwa hawatarudia tena: "...Ni kweli tulikosea kwa kuperform mwimbo ambao umefungiwa. Tunaahidi kutorudia tena kosa lilotokea. Lakini pia kwa kutumia kazi za sanaa kuwasihi wasanii wenzetu na mashabiki kuwa mabalozi bora wa tamaduni za Tanzania," alisema Diamond kwenye video iliyopakiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Basata ililegeza msimamo kidogo kwa kuwaruhusu wasanii hao kwenda kufanya matamasha yao ya nje ya nchi tu kutokana kuwa tayari walishauza tiketi. Matamasha hayo yalikuwa nchini Kenya na visiwani Komoro.

Mada zinazohusiana