Mwili waonekana chini ya bahari kwenye mabaki ya ndege iliyodondoka na mchezaji Emiliano Sala

Wreckage from the Piper Malibu Haki miliki ya picha AAIB

Mwili mmoja umeonekana chini ya bahari kwenye mabaki ya ndege ambayo alikuwa amepanda mchezaji mpira Emiliano Sala na rubani David Ibbotson.

Msako wa chini ya bahari siku ya Jumapili ulibaini mabaki ya ndege aina Piper Malibu nje kidogo ya mji wa Guernsey,Uingereza takriban wiki mbili tangu ilivyopotea.

Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege Uingereza (AAIB) ilithibitisha leo Jumatatu kuonekana kwa mabaki hayo na kuwa mwili wa mtu mmoja umeonekana.

Ndege hiyo ilipotea Januari 21 ikiwa na imembeba mshambuliaji huyo raia wa Argentia mwenye miaka 28. Sala alikuwa anatoka Ufaransa kwenda Wales baada ya kukamilisha usajili wa pauni milioni 15 kutoka Nantes kwenda Cardiff City.

Haki miliki ya picha Getty Images/David Ibbotson
Image caption Emiliano Sala (kushoto) aliabiri ndege hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na rubaniDavid Ibbotson

"Kifaa kinachofanya uchunguzi (ROV) kimebaini mabaki hayo, na kwa masikitiko mwakubwa kuna mwili mmoja ambao unaonekana kwenye picha tuliyoinasa. Sasa tunachukua hatua za ziada za kuongea na familia za abiria na rubani pamoja na polisi," taarifa ya AAIB imesema.

AAIB pia imesema inatarajia kutoa taarifa ya awali juu ya ajali hiyo ndani ya mwezi mmoja toka kutokea kwa ajali.

Bado maamuzi hayajafanyika iwapo mabaki hayo yaliyopo mita 63 chini ya bahari (sawa na futi 207) kuwa yatolewe mpaka ardhini ama la.

Msako wa ndege hiyo ulisitishwa siku chache toka ilipotokea ajali, hata hivyo mchango wa kwenye mtandao ulioanzishwa na ajenti wa Salla ulikusanya pauni 324,000 (371,000 euros) ambazo zimetumika kufadhili msako uliogundua mabaki ya ndege hiyo.

Haki miliki ya picha Marine Traffic
Image caption Eneo ambalo mabaki ya ndege hiyo yalipobainika, mita zaidi ya 60 chini ya bahari.
Haki miliki ya picha Rich Watson / Geoxyz
Image caption Meli ya Geo Ocean III ambayo imeongoza msako wa ndege hiyo baharini

Mito inayoaminika kutoka kwenye ndege hiyo ilipatikana ufukweni katika eneo la Surtainville, nchini Ufaransa wiki iliyopita.

Huzuni ilitanda na salamu za rambi rambi kutumwa kwa wingi jumamosi wakati Cardiff walipocheza mchezo wao wa kwanza nyumbani toka mchezaji huyo alipopotea.

Kocha wa timu hiyo, Neil Warnock, amesema alihisi kuwa Salla alikuwa pamoja nao wakati wakiifunga Bournemouth 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Premia.