Mourinho ahukumiwa mwaka mmoja jela Uhispania kwa kukwepa kodi

Jose Mourinho drives away after leaving his job as Manchester United manager in December Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mourinho alitimuliwa kazi na Machester United mwezi Disemba

Kocha wa zamani wa Mancester United Jose Mourinho amekubali adhabu ya kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la ukwepaji kodi nchini Uhispania.

Uhispania hata hivyo huwa haiwafungi jela wahalifu ambao wamehukumiwa kifungo cha chini ya miaka miwili na wale ambao hawajatumia mabavu kwenye kutenda uhalifu wao.

Mourinho ambaye amekiri makosa yake, anatarajiwa kulipa faini ya Euro 182,500 (£160,160) ili kujihakikishia kuwa hatupwi jela.

Kwa ujumla Mourinho ametozwa faini ya Euro milioni 2 kama adhabu ya kukwepa kodi.

Wendesha mashtaka walimtuhumu kocha huyo kukwepa kodi ya Euro milioni 3.3m (£2.9m) katika kipindi ambacho alikinoa kikosi cha Real Madrid Real Madrid kati ya 2011-2012.

Mourinho anatuhumiwa kuanzisha makampuni kadhaa visiwani British Virgin Islands ili kusimamia mapato yake yatokanayo na picha.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa makampuni hayo yaliundwa ili kuficha mapato halisi ya mkufunzi huyo na kuathiri kiasi cha kodi alichotakiwa kulipa.

Makubaliano ya adhabu hiyo yalifikiwa na Mourinho na maafisa kodi hapo awali, na leo walienda mahakamani ili kuyapa uhalali wa kisheria.

Image caption Mwezi Januari Cristiano Ronaldo alikubali kulipa faini ya Euro milioni 18 kuepuka kifungo cha miezi 23

Kocha huyo ni nyota mpya wa mchezo wa soka kufikia makubaliano na watoza kodi wa Uhispania kwa tuhuma za ukwepaji wa kodi.

Mwezi Januari Cristiano Ronaldo alikubali kulipa faini ya Euro milioni 18 kuepuka kifungo cha miezi 23, katika kesi ya mapato ya picha pia.

Ronaldo alitenda makosa hayo mwaka 201 mpaka 2014 kipindi ambacho Mourinho alikuwa akikinoa kikosi hicho.

Mchezaji mwenza wa zamani wa Ronaldo kikosini Madrid Xabi Alonso, pia anakabiliwa na mashtaka ya ukwepaji kodi wa kiasi cha Euro milioni 2, lakini anakanusha mashtaka hayo.

Marcelo Vieira amekubali kifungo cha nje cha miezi minne kwa kutumia makampuni ya ughaibuni kushughulikia mapato yake ya Euro nusu milioni.

Wachezaji wa Barcelona Lionel Messi na Neymar (sasa yupo PSG) pia wameshawahi kujikuta matatani na mamlaka za kodi za Uhispania hapo awali.

Mada zinazohusiana