Real Madrid 1-2 Girona: Sergio Ramos apewa kadi nyekundu

Cristhian Stuani Haki miliki ya picha EPA
Image caption Cristhian Stuani aliichezea Middlesbrough kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kujiunga na Girona 2017

Real Madrid ilikosa fursa ya kupanda hadi nafasi ya pili katika jedwali la ligi ya La Liga baada ya Girona kutoka nyuma na kuwalaza mabingwa hao wa Ulaya uwanjani Bernabeu.

Casemiro alifunga bao la kwanza kupitia krosi iliopigwa na Toni Kroos kutoka wingi ya kulia na kuwapatia wenyeji hao uongozi.

Hatahivyo Penalti ya Cristhian Stuani ilifanya mambo kuwa 1-1 baada ya Sergio Ramos kushika mpira katika lango na mchezaji wa Girona akapiga mwamba wa goli.

Portu baadaye alifunga bao la ushindi kwa kichwa alichoruka baada ya mkwaju wa Anthony Lozano kupanguliwa, kabla ya Ramos kutolewa nje katika muda wa majeruhi kwa kupewa kadi mbili za manjano.

Beki huyo alikuwa tayari amepewa kadi ya manjano wakati aliposababisha penalti na akapewa onyo wakati alipojaribu kupiga 'bicycle kick' lakini akamuumiza mchezaji wa Girona Pedro Alcala.

Kadi hiyo nyekundu ilikuwa ya 19 ya Ramos tangu aanze kucheza katika lligi ya la Liga, ikiwa ni zaidi ya mchezaji mwengine yeyote yule katika ligi hiyo ya Uhispania.

Ulikuwa muda mwengine mbaya kwa nahodha huyo wa Real Madrid ambaye anakabiliwa na uchunguzi wa Uefa kuhusu iwapo kwa makusudi alitaka kupewa kadi siku ya Jumatano kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Ajax katika mkondo wa kwanza wa mechi ya vilabu bingwa Ulaya ili kuweza kupata marufuku wakati huu na sio baadaye katika shindano hilo.

Ramos alinukuliwa akiwaambia maripota kwamba atakuwa anadanganya akisema kwamba hakulazimisha adhabu hiyo, lakini baadaye alichapisha katika mitandao ya kijamii kwamba hakulazimisha kupewa kadi hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sergio Ramos akipewa kandi nyekundu

Mabadiliko yashindwa kufua dafu

Real, ambaye alianza wikendi katika nafasi ya pili katika jedwali sasa wako nafasi ya tatu , wakiwa na pointi tisa nyuma ya viongozi Barcelona ambao walishinda 1-0 dhidi ya Real Valladolid siku ya Jumamosi.

Atletico Madrid sasa iko katika nafasi ya pili ikiwa pointi mbili juu ya wapinzani wao Real kufuatia ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano.

Mkufunzi wa Real Santiago Solari alifanya mabadiliko sita dhidi ya Girona, huku mshambuliaji wa Wales Gareth Bale akiwa miongoni mwa wachezaji hao huku kiungo wa kati Luka Modric akiwa anahudumia marufuku yake.

Mkufunzi wa Real MadridSantiago Solari alisema: "Girona walionyesha mchezo mzuri katika kipindi cha pili kwa sababu walitusumbua sana. Tumekuwa tukicheza vizuri lakini leo haikuwa siku yetu.

Tulijaribu kuimarisha viwango vya nguvu zetu lakini hatukufanikiwa -Tuna kikosi kikubwa na wachezaji wazuri. Hatukutumia fursa tulizopata na ilikuwa vigumu kwetu katika dakika 25 za kwanza.

Mkufunzi wa Girona Eusebio Sacristan alisema: "Ni muhimu kwetu kupata ushindi katika mji wa Bernabeu - kwa mashabiki wetu, na timu yetu.

Pengine walidhania watapata bao la pili, lakini tulikuwa polepole tunazidi kuwazuia na kusonga mbele. Mwisho wa mechi nadhani yalikuwa matokeo ya sawa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii