UEFA: Juventus yalazwa na Atletico Madrid huku Man City ikiishinda Schalke Ujerumani

Bao la Diego Godin lilikuwa la kwanza la vilabu bingwa Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images

Atletico Madrid ilijipatia ushindi mkubwa dhidi ya Juventus katika mechi ya kuwania robo fainli ya vilabu bingwa Ulaya raundi ya kwanza baada ya kusakamwa magoli mawili kwa nunge.

Kikosi cha Diego Simione kilinyimwa penalti na goli la Alvaro Morata na refa msaidizi VAR kabla ya kupata magoli hayo mawili.

Jose Maria Gimenez alifunga bao la kwanza baada ya kichwa cha Morata kuzuiliwa na Mario Mandzukic

Diego Godin baadaye alifunga goli la pili baada ya msukosuko katika safu ya ulinzi ya Juventus.

Wachezaji watakaokosa mechi ya mkondo wa pili

Mshambuliaji Diego Costa na kiungo wa kati Thomas Partey wa Atletico Madrid na beki wa kushoto wa Juventus Alex Sandro wote watakosa mechi ya mkondo wa pili siku ya Jumanne, mwezi Machi baada ya kupewa kadi zao za tatu katika michuano hiyo.

Chanzo cha picha, EPA

Wakati huohuo Klabu ya Manchester City haiko tayari kujizatiti zaidi katika mkondo wa mwisho wa kombe la vilabu bingwa , kulingana na mkufunzi wake Pep Guardiola baada ya kikosi chake kutoka nyuma dakika za mwisho na kuishinda Schalke ya Ujerumani katika awamu ya kwanza ya mechi ya kufuzu katika robo fainali ya kombe hilo.

Mshambuliaji wa Uingereza Raheem Sterling alifunga bao hilo la dakika za mwisho.

Mabingwa hao wa ligi ya Uingereza walianza mechi hiyo wakipigiwa upatu na wakapata bao la kwanza kunako dakika ya 18 kupitia Sergio Aguero.

Usaidizi wa VAR

Lakini mechi ilitawaliwa na Schalke kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika baada ya uamuzi wa utata wa VAR na penalti mbili za Nabil Bentaleb.

Penalti ya kwanza ya Schalke ilijiri kufuatia uamuzi wa VAR, ambao ulimuadhibu beki wa City Nicolas Otamendi kwa kunawa mpira katika lango baada ya mpira kumgusa kwenye mkono alipokuwa akiurudisha nyuma.

Penalti ya pili ilitolewa kufuatia fauli ya Fernandinho aliyomfanyia Salif Sane huku refa akisisitiza uamuzi wake baada ya kushirikiana na VAR.

Baada ya kupewa kadi ya manjano kwa kuunawa mpira huo, Otamendi alionyeshwa kadi nyengine ya manjano kwa kumchezea visivyo Guido Burgstaller katika kipindi cha pili-ikimaanisha kwamba yeye na Fernandinho hawatashiriki katika mechi ya mkondo wa pili wa kombe hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Naye Ronaldo ambaye analenga kushinda kombe la sita la michuano ya vilabu bingwa na la nne mfululizo alikuwa na nafasi bora zaidi za kuiweka kifua mbele klabu yake baada ya mkwaju wake wa adhabu kupanguliwa na kipa Jan Oblak.

Atletico hawako katika hali yao ya kuonyesha mchezo mzuri msimu huu lakini walihitaji kupata ushindi huo kwa timu ambayo imepoteza fainali nne kati ya fainali tano za vilabu bingwa Ulaya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Walikosa penalti ya kipindi cha kwanza ambayo ilitolewa baada ya Mattia de Sciglio kumuangusha Costa ambaye alikuwa anaanza kwa mara ya kwanza tangu tarehe 2 mwezi Disemba kufuatia jeraha.

Refa alibadilisha uamuzi baada ya maafisa wa VAR kumwambia kwamba makosa hayo yalifnyika nje ya eneo hatari.