Claude Puel: Afutwa kazi na Leicester

Mkufunzi Claude Puel

Chanzo cha picha, Getty Images

Leicester City imemfuta kazi mkufunzi wake Claude Puel baada ya miezi 16 kutokana na msururu mbaya wa matokeo.

City ilishindwa 4-1 nyumbani na klabu ya Crystal Palace siku ya Jumamosi katika kile kilichoonekana kuwa mechi ya mwisho ya Puel.

Puel, 57 anaondoka katika klabu hiyo ikiwa katika nafasi ya 12 katika jedwali la ligi katika msimu wake wa kwanza na sasa klabu hiyo inamsaka meneja wake wa nne wa kudumu katika kipindi cha miezi 23.

Kushindwa kwa siku ya Jumamosi kunamaanisha kwamba Leicester imeshindwa mechi nne mfululizo katika ligi ya Uingereza kwa mara ya kwanza tangu mwezi Januari 2000 na kufungwa bao la haraka zaidi katika mechi 19 za EPL msimu huu-ikiwa ni zaidi ya timu nyengine yeyote ile.

Naibu mkufunzi Jacky Bonnevay pia ataondoka katika klabu hiyo pamoja na mkufunzi wa kwanza Mike Stowell huku Adam Sadler akitarajiwa kuchukua usimamizi wa timu hiyo kwa muda.

Mechi ya Leicester inayofuata itakuwa nyumbani dhidi ya Brighton siku ya Jumanne.

Puel aliajiriwa kwa mkataba wa miaka mitatu mnamo mwezi Octoba 2017, akichukua mahala pake Craig Shakespeare ambaye alikua amemrithi mshindi wa taji la ligi ya EPL Claudio Ranieri katika usimamizi wa klabu hiyo.

Mkufunzi huyo wa zamani wa klabu ya Lyon alikuwa amefutwa kazi na Southampton mwezi Juni 2017 na kuwasili Leicester miezi minne baadaye klabu hiyo ikiwa ya tatu kutoka chini.

Aliingoza kufika katika nafasi ya tisa katika jedwali la ligi , ikiwa ni mara ya pili kumaliza wakiwa katika nafasi 10 bora tangu 2000.

Chanzo cha picha, Getty Images

Je mbinu yake ndio iliomchongea kupigwa kalamu?

Msimu huu, Leicester imeshinda mechi tisa kati ya 27 za EPL , ikiwemo ushindi dhidi ya Manchester City na Chelsea mwezi Disemba.

Lakini mbinu ya mchezo wa Puel na wachezaji anaochagua wamekabiliwa na pingamizi kubwa kutoka kwa mashabiki wa Foxes.

Puel iliwakasirisha baadhi ya mashabiki kwa kuweka timu iliodhoofika dhidi ya Manchester City katika robo fainali ya kombe la Carabao huku James Maddison na Marc Albrighton wakicheza kama wachezaji wa ziada , huku Jamie Vardy naye akitochezeshwa kabisa.

Kushindwa 2-1 kwa Foxes katika uwanja wa Newport kunajiri baada ya Puel kufanyia kikosi chake mabadiliko saba katika kikosi chake huku Mardisson na Vardy wakiwekwa benchi licha ya kuwachagua washindi hao wa ligi ya Uingereza katika kikosi cha wachezaji 11.

Mshambuliaji Vardy ambaye ana magoli 8 na ndio mchezaji mwenye mabao mengi msimu huu hivi majuzi alikiri kwamba mbinu inayotumiwa na Puel haimfurahishi.