Kwanini Marekani imewawekea vikwazo vya usafiri viongozi wa DRC?

Rais wa tume huru ya uchaguzi nchini DR Congo (CENI) Corneille Nangaa Yobeluo akitangaza matokeo ya muda ya uchaguzi wa urais mjini Kinshasa on Januari 10, 2019

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa tume huru ya uchaguzi nchini DR Congo (CENI) Corneille Nangaa Yobeluo

Hatua ya Marekani ya kuwawekea vikwazo vya usafiri maafisa wakuu wa tume ya uchaguzi pamoja na viongozi wengine nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya DRC imeendelea kuzua hisia mbalimbali.

Serikali ya Marekani ilichukua hatua hiyo mwishoni mwa wiki kwa madai kwamba viongozi hao walijipatia utajiri kwa njia za rushwa.

Msemaji wa Tume huru ya uchaguzi Jean Pierre Kalamba, kupitia barua iliyotiwa saini na tume hiyo amekanusha tuhuma hizo za rushwa na kuongeza kuwa ilifanya kazi nzuri ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia ya amani.

Hali ambayo ilisaidia marais wawili wa Congo kupokezana madaraka kwa njia ya amani.

Bwana Kalamba ameahidi kutoa ripoti ya maandalizi ya uchaguzi kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka huu.

Kwa upande wake Lambert Mende ambaye alikuwa msemaji wa serikali ya Joseph Kabila amesema vikwazo hivyo havitakuwa na mafanikio yoyote.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Lambert Mende

''Marekani inasimama na watu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufuatia historia waliyoweka kwa kufanikisha mchakato wa viongozi kupokezana madaraka kwa amani. Uchaguzi ulionesha ari ya wakongo ya kutaka mabadiliko ya serikali na taasisi zinazowajibika. Hatahivyo, kuna madai kwamba hapakuwa na uwazi katika machakato wa uchaguzi.'' ilisema taarifa iliyotolewa na Marekani.

Viongozi waliyowekewa vikwazo ni pamoja na mwenyekiti wa tume ya huru ya uchaguzi ya Congo DRC (CENI), Corneille Nangaa, naibu wake Norbert Basengezi Katintima.

Wengine ni mshauri wa mkuu wa CENI Marcellin Mukolo Basengezi, kiongozi wa bunge la kitaifa Aubin Minaku Ndjalandjoko pamoja na rais wa mahakama ya kikatiba bwana Benoit Lwamba Bindu.

Marekani pia imewawekea vikwazo vya usafiri maafisa wa kijeshi na maafisa wa serikali wanaoamnikia kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhujumu mchakato wa uchaguzi nchini D.R.C.

''Maafisa hawa walinufaika kutokana na ufasadi, au kuwazuia watu kuandamana na kuwanyima uhuru wa kujieleza.''iliongeza taarifa hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mgombea wa upinzani Martin Fayulu amepinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa urais

Je uchaguzi wa Disemba 30 ulikuwaje?

Tume ya uchaguzi awali ilikuwa imetangaza kwamba felix Tshisekedi alikuwa amepata asilimia 38.5 ya kura hiyo huku Fayulu akijpatia asilimia 34.7.

Mgombea wa chama tawala Emmanuel Shadary alipata asilimia 23.8.

Hatahivyo Fayulu alihoji kwamba bwana Tshisekedi alifanya makubaliano na Bwana Kabila ambaye amekuwa uongozini kwa miaka 18.

Bwana Kabila alikuwa haruhusiwi kuwania muhula mwengine kikatiba.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Martin Fayulu anasisitiza kuwa yeye ndiye aliyechaguliwa rai

Kabla ya uchaguzi, kulitokea utata baada ya uchaguzi kuahirishwa katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola yakiwemo miji ya Beni na Butembo mashariki mwa nchi hiyo, na pia katika jiji la Yumbi magharibi mwa nchi hiyo.

Hatua hiyo iliathiri takriban wapiga kura 1.26 milioni kati ya jumla ya wapiga kura 40 milioni.

Uchaguzi katika maeneo hayo uliahirishwa hadi mwezi Machi mwaka huu.