Simba SC 2-1 AS Vita: Miamba ya soka ya Tanzania yatinga robo fainali Klabu Bingwa Afrika

mashabiki wa Simba SC wakiwa uwanjani katika mechi yao na AS Vita
Image caption Mashabiki wa Simba hawakuchoka kuishangilia timu yao wakati wa mchuano na Vita Club

Klabu ya soka ya Simba kutoka Tanzania imetinga hatua ya robo fainali ya Michuano ya Kabu Bingwa Afrika baada ya kusubiri kwa miaka 25.

Mara ya mwisho kwa Simba kufikia hatua kama hiyo ilikuwa mwaka 1994, ambapo walitolewa na klabu ya Nkana ya Zambia kwa jumla ya magoli 4-3 baada ya kucheza michezo miwili.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Simba kufika robo fainali, mara ya kwanza ilikuwa miaka 45 iliyopita mnamo 1974 ambapo walisonga mpaka kufikia hatua ya nusu fainali na kutolewa na Ghazl Al-Mahalla ya Misri kwa mikwaju ya penati 3-0.

Jumamosi Simba ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, iliitungua Vita Club ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa goli 2-1, ushindi uliowapatia alama 9 baada ya kucheza mechi sita.

Katika mchezo huo, AS Vita iliitangulia Simba katika dakika ya 13' kwa kuandika goli liliofungwa na Kasendu Kazadi baada ya kuwazidi maarifa walinzi wa Simba.

Simba ilirudi mchezoni katika dakika ya 36' kwa goli la mlinzi wa kushoto Mohammed Hussein. Baada ya hapo mchezo huo ulitawaliwa na kosa kosa hususan kwa upande wa safu ya ushambuliaji ya Simba.

Furaha ya Simba ilitimia katika dakika ya 90' baada ya kiungo nguli Clatous Chota Chama kufunga bao safi, akipokea pasi kutoka kwa nahodha John Bocco na 'kususwa' na Haruna Niyonzima na kisha kuunganisha mpaka nyavu ndogo za lango la Vita.

Kwa ushindi huo, Simba imemaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi D na kungana na Al Ahly ya Misri iliyomaliza kileleni kwa alama 10 kufuzu katika hatua ya robo fainali.

Klabu 'nane bora' Afrika 2018/19

  • Simba (Tanzania)
  • TP Mazembe (DRC)
  • Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
  • Horoya (Guinea, Conakry)
  • Al Ahly (Misri)
  • CS Constantine (Algeria)
  • Esperance (Tunisia)
  • Wydad Athletic Club (Morocco)

Simba wakali nyumbani

Kufuzu kwa Simba kwenda robo fainali ni matokeo ya kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani. Kwani wamefungwa mechi zote tau walizocheza ugenini.

Kabla ya hatua ya makundi Simba ilicheza mechi nne, mbili nyumbani na mbili ugenini. Timu pekee ambayo Simba imeifunga nyumbani (4-1) na ugenini (0-4) ni Mbabane Swallows ya eSwatini katika raundi ya kwanza kwa jumla ya goli 8-1.

Image caption Kikosi cha Simba kilichocheza na Vita Club

Raundi ya pili Simba ilicheza na Nkana ya Zambia na kufungwa ugenini 2-1 kabla ya kuwatoa kwa ushindi wa nyumbani wa magoli 3-1.

Kwenye makundi Simba ilifungwa goli 5 mara mbili nchini DRC na Vita na nchini Misri na Al Ahly. Simba pia ilifungwa 2-0 na JS Soura nchini Algeria.

Nyumbani Simba ikaifunga JS Soura 3-0, Al Ahly 1-0 na Vita 2-1.

Moja ya chachu ya ushindi kwa Simba wakiwa nyumbani ni nguvu kubwa ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiujaza Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki 60,000.

Tayari kocha wa Simba raia wa Ubelgiji Patrick Aussems anapanga mipango ya kutinga nusu fainali: "Asante kwa wachezaji, viongozi pamoja na Mo (Mohammed Dewji)…Asante kwa mashabiki waliotushangilia kwa nguvu. Tumefuzu robo fainali, sasa twende nusu fainali."

Hata hivyo, kocha huyo pamoja na benchi zima la ufundi litabidi lipitie upya aina yao ya uchezaji wanapokuwa nje ya Tanzania kama kweli wanataka kufanya vizuri katika hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali kama ilivyofanya mwaka 1974.

Kwa sasa, mashabiki wa Simba wanasubiria kupangwa kwa droo ya hatua inayofuatia ili kumjua mpinzani wao katika hatua ya robo fainali.

Huwezi kusikiliza tena
Shabiki wa Yanga aliyemweka rehani mkewe

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii