AFCON 2019: Taifa Stars yaifunga Uganda na kumaliza mkosi wa miaka 39

Taifa Stars
Image caption Kikosi cha Taifa Stars kilichoandika historia ya kufuzu AFCON baada ya miaka 39.

Timu ya Taifa Tanzania imefuzu katika michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mara ya pili baada ya kusubiri kwa miaka 39.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo maarufu kama Taifa Stars ilikuwa 1980, ambapo hakuna hata mchezaji mmoja katika kikosi cha sasa ambaye alikuwa amezaliwa, na kocha wao Mnigeria Emmanuel Amunike alikuwa mtoto wa miaka 10.

Baada ya safari yao kupitia milima na mabonde, Taifa Stars wamefuzu katika siku ya mwisho kabisa ya mchuano wa makundi jana Jumapili baada ya kuifunga Uganda 3-0. Ushindi huo uliwafanya Stars kufikisha alama 8 na kujikatia tiketi ya kwenda Misri baadae mwaka huu.

Katika mchezo mwengine wa kundi lao, Cape Verde walitoka sare tasa na Lesotho, hivyo timu hizo kufikisha alama 5 na 6 mtawalia. Kwa matokeo hayo Stars imejiunga na vinara Uganda ambao walifuzu awali baada ya kufikisha alama 13.

Stars waliunza mchezo huo kwa kasi, huku wakipata hamasa kutoka kwa mashabiki zaidi ya 60,000 walioujaza uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Goli la kwanza la stars lilifungwa na mshambuliaji Simon Msuva baada ya kupokea pasi kutoka kwa John Bocco. Mpaka mapumziko matokeo yalikuwa 1-0.

Dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza, Stars walipata penati baada ya mpira uliopigwa na nahodha Mbwana Samatta kutua kwenye mkono wa mlinzi wa Uganda Cranes Kirizistom Ntambi kwenye eneo la hatari.

Mkwaju wa penati hiyo ulisukumwa nyavuni na mlinzi Erasto Nyoni na kuiandikia Stars bao la pili.

Ushindi mnono kwa Stars ulihitimishwa katika dakika ya 57 mara baada ya beki Agrey Morris kufungwa kwa ustadi goli la kichwa akiunganisha krosi maridhawa iliyochongwa na John Bocco.

Matokeo hayo yamepokelewa kwa mikono miwili na Watanzania wakiongozwa na rais John Magufuli ambaye amewamwagiwa sifa kem kem wachezaji: "kwa kweli leo nimefurahi sana. Taifa Stars oye, Tanzania oye... yani yale magoli, leo nimeuona mpira, sio ule wa siku za nyuma."

Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete kwa kutumia mtandao wake wa Twitter pia ametuma pongezi zake kwa Stars.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cook naye ametuma saqlamu zake za hongera kwa ushindi huo uliosubiriwa kwa miaka 39.

Afrika Mashariki yang'ara

Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Wachezaji wa Harambee Stars wakisherehekea kufunga bao katika uga wa Kasarani 14 Oktoba, 2018

Kufuzu kwa Stars kunakamilisha moja ya historia kubwa ya mafanikio ya mpira katika kanda ya Afrika Mashariki ambapo kwa mara ya kwanza mataifa manne ya ukanda huo yamefuzu kuelekea Misri.

Uganda wao walitangulia kufuzu mwezi Novemba 2018, na michuano ya mwaka huu itakuwa ya saba kwa taifa hilo kushiriki.

Kenya ilikuwa ya pili kwa kufuzu katika ukanda huu kwa kufanya hivyo Disimba 2018., na wataenda Misri ikiwa ni mara yao ya sita kushiriki michuano hiyo.

Burundi wao walifuzu siku moja kabla ya Tanzania kwa kutoka sare na Gabon. Hii ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kushiriki michuano ya AFCON.

Kwa ujumla, michuano ya mwaka huu yatashirikisha mataifa 24, ikiwa ni ongezeko la timu 8 kutoka awali ambapo zilikuwa zikishiriki timu 16.