Klabu Bingwa Ulaya: Liverpool 2-0 Porto, Tottenham 1-0 Manchester City

Son Heung-min
Maelezo ya picha,

Licha ya ushindi wa goli moja la Son Heung-min, Spurs watakuwa na kibarua kigumu kulinda ushindi wao dhidi ya City watakaporudiana wiki ijayo.

Mechi ya kwanza ya robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya inayowakutanisha vilabu vikubwa vya Uingereza imekamilika kwa Tottenham kupata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Manchester City.

Mshambuliaji wa Spurs, Son Heung-min aliamsha furaha za mashabiki wa timu yake katika uwanja wao mpya kwa kufunga goli muruwa katika dakika ya 78.

Hata hivyo, ushindi wa Spurs umekuja na machungu pia baada ya mshambuliaji wao tegemezi Harry Kane kutolewa baada ya kuumia mchezoni, na kuna uwezekano asiweze kurejea tena dimbani msimu huu.

Manchester City walipoteza nafasi ya wazi ya kupata goli baada ya penati ya Sergio Aguero kutolewa na kipa wa Spurs Hugo Lloris.

Mashabiki wa City bado wanaamini kuwa ushindi mwembamba wa Spurs unaweza kupinduliwa na wachezaji wao kwenye mechi ya marudiano wiki ijayo watakapokuwa nyumbani dimba la Etihad.

Man City wamekuwa wakiangaliwa kwa makini msimu huu iwapo wataweza kuandikisha historia ya kuchukua vikombe vyote vinne wanavyoshiriki msimu huu; Klabu Bingwa Ulaya, Ligi ya Premia, Kombe la FA na Kombe la Ligi.

Kocha wa Spurs Mauricio Pochettino kwa sasa akili yake yote ipo kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo: "Ulikuwa ni mchezo mkali na mgumu. Lakini wapinzani wetu ni Manchester City na kuna mchezo wa marejeano. Tuna furaha kuwa tumeonesha kiwango cha juu. Bado kuna dakika 90 za kucheza."

Maelezo ya picha,

Mshambuliaji tegemezi wa Spurs, Harry Kane huenda akakosa echi zote zilizosalia msimu huu baada ya kuumia jana usiku.

Kwa upande wake kocha wa City Pep Guardiola amesema matokeo ya Klabu Bingwa kwa kawaida ni magumu lakini kwa sasa mipango yao yote ipo kwenye mchezo wao unaofuata wa Ligi ya Premia dhidi ya Crystal Palace. City na Liverpool awanaminyana vikali kuwania ubingwa wa Premia.

"...Sasa inatupasa tujipange dhidi ya mchezo na Crystal Palace. Hatuna muda wa kuwafikiria Tottenham," amesema Guardiola. Katika mechi ya kwanza mwezi Disemba, Palace waliwafunga city 3-2.

Liverpool waitangulia Porto

Liverpool wamechukua hatamu ya mchuano wao wa robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kuwatangulia Porto goli 2-0.

Katika mechi hiyo ambayo Liverpool walikuwa nyumbani Anfield, Majogoo hao wa jiji walipata goli la uongozi katika dakika ya tano kupitia Naby Keita.

Maelezo ya picha,

Naby Keita amefunga bao lake la pili kwa Livepool dhidi ya Porto.

Dakika 20 baadae winga Roberto Firmino akapachika goli la pili akimalizia kazi nzuri na pasi safi baina ya Trent Alexander-Arnold na Jordan Henderson kwenye eneo la kiungo.

Porto pia walitengeneza nafasi kadhaa lakini wakashindwa kuzitumia.

Mshambuliaji wa Porto Moussa Marega alipata nafasi kadhaa lakini akashindwa kucheka na nyavu, na kuikosesha timu yake walau goli moja muhimu la ugenini.

Mlinda mlango wa Liverpool Alisson alifanya kazi nzuri kuzuia shambulio kali la mshambuliaji huyo katika dakika ya 30 na muda mfupi baadae raia huyo wa Mali.

Kwa ujumla, Marega alipata nafasi tatu za wazi ambazo angeweza kuzitumia kuwaumiza Liverpool.

Maelezo ya picha,

Mshambuliaji wa Porto Moussa Marega alipata nafasi tatu za wazi ambazo angeweza kuzitumia kuwaumiza Liverpool.

Japo Liverpool wanaendelea kupigiwa chapuo la kusonga katika hatua ya nusu fainali, bado wana kazi ya kufanya watakapokua ugenini nchini Ureno wiki ijayo kwenye mechi ya marudiano.

Hata hiyo kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amefurahia matokeo ya jana usiku.

"Tuna furaha, ni mechi ya kwanza na mambo yatakuwa magumu kwenye mchezo wa pili. Tumefunga magoli mawili, na kuutawala mchezo kwa muda mrefu, japo hatukutulia katika kipindi cha pili. Mpambano bado haujaisha, sasa inabidi twende ugenini na kupambana tena," amesema Klopp.

Usiku wa leo Jumatano, michuano hiyo itaendelea kwa Mancester United kuwakaribisha Barcelona dimbani Old Trafford, huku Ajax ikiwakaribisha Juventus.