TP Mazembe yaifunga Simba 4-1 na kuwango'a Klabu Bingwa Afrika

Kikosi cha TP Mazembe Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kikosi cha TP Mazembe

Klabu ya Simba ya Tanzania imekubali kichapo cha goli 4-1 kutoka kwa TP Mazembe ya DRC na kung'olewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Mchezo huo wa robo fainali umepigwa jijini Lubumbashi nchini Congo ulikuwa ni wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza kuchezwa jijini Dar es Salaam wikendi iliyopita.

Simba walishindwa kufurukuta wiki iliyopita wakiwa nyumbani na kulazimishwa sare tasa.

Awali Simba walionekana kama wanaenda kuvunja mwuko wao wa unyonge ugenini kwa kuuanza mchezo wa leo vyema.

Straika wa Simba Emmanuel Okwi aliwanyamazisha mashabiki wa Mazembe kwa kuitanguliza timu yake katika dakika ya pili ya mchezo.

Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo walusawazisha katika dakika ya 23 ya mchezo kupitia beki Kobaso Chongo.

Meshack Elia ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba aliwaandikia Mazembe goli la pili katika dakika ya 38.

Image caption Kikosi cha wachezaji wa Simba

Kipindi cha pili kilianza kwa Mazembe kuendelea kujiamini na walifunga bao lao la tatu kupitia kiungo fundi Tresor Mputu katika dakika ya 62.

Msumari wa mwisho kwenye jeneza la Simba uligongelewa na Jacob Muleka katika dakika ya 74.

Matokeo ya leo ni muendelezo wa kiwango hafifu ambacho Simba imekuwa ikikionesha wanapokuwa ugenini.

Kufuzu kwa Simba kwenda robo fainali ni matokeo ya kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani.

Simba wamefungwa mechi tano kati ya sita za ugenini walizocheza kwenye michuano hiyo.

Na katika mechi sita walizocheza nyumbani wameshinda tano na kutoka sare mmoja.

Timu pekee ambayo Simba imeifunga nyumbani (4-1) na ugenini (0-4) ni Mbabane Swallows ya eSwatini katika raundi ya kwanza kwa jumla ya goli 8-1.

Raundi ya pili Simba ilicheza na Nkana ya Zambia na kufungwa ugenini 2-1 kabla ya kuwatoa kwa ushindi wa nyumbani wa magoli 3-1.

Kwenye makundi Simba ilifungwa goli 5 mara mbili nchini DRC na Vita na nchini Misri na Al Ahly. Simba pia ilifungwa 2-0 na JS Soura nchini Algeria.

Mara ya mwisho kwa Simba kufikia hatua ya robo fainali ilikuwa mwaka 1994, ambapo walitolewa na klabu ya Nkana ya Zambia kwa jumla ya magoli 4-3 baada ya kucheza michezo miwili.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Simba kufika robo fainali, mara ya kwanza ilikuwa miaka 45 iliyopita mnamo 1974 ambapo walisonga mpaka kufikia hatua ya nusu fainali na kutolewa na Ghazl Al-Mahalla ya Misri kwa mikwaju ya penati 3-0.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii