Messi azima ndoto za United Ulaya Ajax yatinga nusu fainali baada ya kuilaza Juventus nyumbani

Chanzo cha picha, Getty Images
Lionel Messi
Mabao mawili ya kipindi cha kwanza ya Lionel Messi yameisaidia Barcelona kuitandika Manchester United 3-0 na kutinga hatua ya nusu fainali ya Klabu bingwa Ulaya, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015.
Barcelona imeiondosha Manchester United kwa jumla ya mabao 4-0, kufuatia ushindi wake wa 1-0 iliyoupata wiki iliyopita katika uwanja wa Old Trafford.
Kabla ya mabao hayo ya Messi katika dakika za 16 na 20, United ilianza vyema mchezo huo, Marcus Rashford akigongesha mwamba mwanzoni kabisa mwa mchezo huo.
Lakini ndoto za kikosi hicho cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer kufuzu nusu fainali zilizimwa na bao la Philippe Coutinho katika dakika ya 61.
Kipigo hicho kinaifanya Manchester kukumbana na kipigo kikubwa zaidi katika michezo miwili ya mtoano inayohusisha matokeo ya ujumla kwenye michuano ya Ulaya.
Chanzo cha picha, Reuters
Barca itavaana na mshindi wa mechi ya jumatano hii kati ya Liverpool na Porto, ambapo katika mchezo wa awali Liverpool ilishinda 2-0, wakati United sasa macho yao itabidi wayaelekeze kwenye ligi kuu ya England, kusaka nafasi ya nne, ambapo jumapili hii wanakipiga na Everton.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amemsifu Messi kwa kiwango alichoonyesha.
"Hakuna shaka kwamba Messi ni mchezaji bora, na ndiye aliyeleta tofauti ya matokeo ya mchezo, baada ya mabao yake mawili, ilikuwa ngumu, mchezo ulikwishamaliza. Tunaijenga timu upya msimu ujao, lazima tusajili vizuri."
Chanzo cha picha, Reuters
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer alimsifu Messi kwa kiwango alichoonyesha.
Kiungo wa Manchester United Jesse Lingard: "Hupaswi kufanya makosa katika aina hii ya mechi.
Tulitawala dakika 15 za kwanza, tulipata nafasi, tungezitumia mambo yangekuwa tofauti".
Nayo timu ya Ajax imetinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika miaka 22, baada ya kutoka nyuma kwa goli 1, na kushinda 2-1 dhidi ya Juventus ugenini katika uwanja wa Allianz. Mchezo wa kwanza timu hizo zilikwenda sare ya 1-1, hivyo Ajax wanafuzu kwa jumla ya magoli 3-2.
Chanzo cha picha, Reuters
Wajezaji wa Ajax washerehekea kufuzu wa Nusu fainali ya Klabu Bingwa Ulaya
Cristiano Ronaldo alifunga bao lake la 126 katika mashindano hayo, dakika 28 tu baada ya kuanza kwa mchezo huo, kabla ya Donny van de Beek kuisawazishia Ajax dakika 6 baadae.
Juventus hawatamsahau Matthijs de Ligt, aliyezamisha jahazi lao vigogo hao wa Turin, katika dakika ya 67.
Ajax inasubiri mshindi wa mechi ya Manchester City dhidi ya Tottenham, wanaokipiga jumatano hii, City ikiingia katika mchezo huo ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Chanzo cha picha, Reuters
Cristiano Ronaldo
Kocha wa Juventus Massimiliano Allegri: "Wametupa shida sana kipindi cha pili, na kuruhusu bao,"Ajax wanastahili matokeo haya na kufuzu nusu fainali.
"Nimemueleza Rais kwamba nabaki, sitajiuzulu na rais pia anataka nibaki. Tutakaa chini na kuzungumza kuhusu mustakabali wa timu hii."

Solksjaer: Bahati haitatusaidia dhidi ya Barcelona, kivumbi hii leo Camp Nou
Manchester United kuvaana na Barcelona usiku wa leo.