Tottenham yailaza ManCity Liverpool yaibwaga Porto kutinga nusu fainali Champions League

Wachezaji wa Spurs washangilia ushindi wao dhidi ya Manchester City

Chanzo cha picha, Reuters

Tottenham Hotspur imetinga hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia, ikibebwa na kanuni ya magoli ya ugenini kwenye mchezo wa marejeano baina ya timu hiyo na Manchester City usiku wa jumatano.

Licha ya kufungwa na Manchester City 4-3, ushindi wa goli 1-0 iliyoupata Spurs kwenye mchezo wa awali, umeisaidia timu hiyo kuiondosha City iliyohitaji ushindi wowote wa tofauti ya magoli mawili.

Katika mchezo huo, magoli matano yalifungwa ndani ya dakika 21, yakiweka rekodi ya magoli matano yaliyofungwa kwa haraka zaidi kwenye historia ya michuano ya Klabu bingwa Ulaya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sterling alifunga mabao mawili (4, 21) na Bernardo Silva goli moja (11) kwa upande wa City, huku Heung-Min Son akiifungia Spurs mabao mawili (7, 10).

Aguero alileta matumaini kwa City (59), kabla Fernando Llorente kufunga bao muhimu akiunganisha kona ya Kieran Trippier.

Nusura historia hiyo ya Spurs izimwe katika dakika ya mwisho ya mchezo kama si mfumo wa usaidizi wa video (VAR), kukataa goli la Sterling ambalo kama lingekubalika, lingezima ndoto za Spurs.

Chanzo cha picha, Reuters

Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino anasema: "Ni kama maajabu vile namna mambo yalivyokwenda. Nina furaha sana, wachezaji wangu ni mashujaa. Nina furaha kwa ajili yao na mashabiki pia".

Pochettino sasa anafikia rekodi ya Bill Nicholson ambaye aliiwezesha Tottenham Hotspur kutinga nusu nusu fainali ya kombe la Ulaya katika msimu wa 1961-62.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola: "Tulikosa penati katika wa kwanza, tulitengeneza nafasi nyingi sawia dhidi ya timu ngumu… Tumefanya makosa katika magoli yao mawili ya kwanza. Tulipambana mpaka hatua ya mwisho."

Chanzo cha picha, Reuters

Kwa ushindi huo Spurs sasa itavaana na Ajax ambayo iliondosha Juventus kwa kuifunga mabao 2-1 usiku wa Jumanne hii.

Nayo Liverpool itavaana na Barcelona baada ya ushindi mnono wa mabao 4-1 iliyoupata dhidi ya Porto na kufuzu nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 6-1.

Kikosi hicho cha Jurgen Klopp hakikupata ushindani mkali sana katika uwanja wa Estadio do Dragao, Sadio Mane akiitanguliza Liverpool kwa bao lake la dakika ya 26 akiunganisha krosi ya Mohamed Salah.

Chanzo cha picha, Reuters

Mabao mengine ya Liverpool yalifungwa na Salah (65), Roberto Firmino (77) na Virgil van Dijk (84), wakati bao pekee la Porto katika mchezo huo lilifungwa na Eder Militao.

Winga wa Liverpool Sadio Mane: "Mwanzoni mchezo ulikuwa mgumu. Tulijawa na hofu lakini morali ilikua juu, tulipambana na kufanikiwa kufunga."