EUROPA LEAGUE: Arsenal na Chelsea zatinga nusu fainali

Arsenal imeiondosha Napoli kwa jumla ya mabao 3-0

Chanzo cha picha, Getty Images

Mkwaju wa adhabu wa Alexandre Lacazette katika kipindi cha kwanza umeipa ushindi wa ugenini wa bao 1-0 Arsenal na kuisaidia kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Europa League, kwa kuiondosha Napoli.

Arsenal imeiondosha Napoli kwa jumla ya mabao 3-0, kufatia ushindi wake wa bao 2-0 iliyoupata kweye mchezo wa kwanza uliopigwa Emirates wiki iliyopita.

Pamoja na Napoli kuruhusu mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani San Paolo mapema, masaa matatu kabla ya mchezo kuanza, badala ya kuongeza molari ya wachezaji, mashabiki hao walionekana kulowa muda ulivyozidi kuyoyoma.

Katika mchezo huo Arkadiusz Milik nusura afufue matumaini ya Napoli baada ya kufunga goli lililokataliwa kutokana na kuonekana kuzidi, huku mlinda mlango mkongwe, Petr Cech akifanya kazi ya ziada kuchomoa mchomo wa Jose Callejon.

Kiungo wa Arsenal, Aaron Ramsey alitolewa mapema kwenye mchezo huo baada ya kupata majeraha, ambayo kwa mujibu wa kocha wa Arsenal, Unai Emery, huenda nyota huyo akakaa nje kwa majuma kadhaa.

Emery: "Aaron Ramsey amepata majeraha ya misuli, majeraha ya aina hii kawaida atakaa nje kwa majuma kadhaa .

Lakini tuna wachezaji wengine watacheza kusaidia timu kufanya vyema. Najivunia wachezaji wangu, tulianza vyema. Kuifunga Napoli kwenye mechi mbili, tunapaswa kuwa na furaha."

Nayo Chelsea imeitandika Slavia Pragua na kufuzu nusu fainali Ulaya, Pedro akiifungia Chelsea mabao mawili, katika mchezo ambao Chelse aimeitandika Slavia Prague 4-3 na hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao (5-3).

Mhispania huyo aliipa uongozi wa mapema Chelsea katika dakika ya (5) tu ya mchezo, kabla ya Simon Deli kujifunga katika dakika ya 9).

Chanzo cha picha, Reuters

Olivier Giroud aliifungia Chelsea bao la tatu na lake la kumi katika michuano hiyo ya Europa League msimu huu (117) kabla ya Pedro kuongeza la nne (27).

Mabao mawili ya harakaharaka ya Sevcik (51, 54) nusura yatie mchanga kitumbua cha Chelsea, ambao walipambana kuhakikisha wanaziba njia zote za Prague.

Ushindi wa Chelsea unaifanya kuwa klabu ya kwanza England kushinda michezo 11 katika michuano ya Ulaya kwenye msimu mmoja, lakini kocha wa Chelsea itabidi afanye kazi ya ziada kuhakikisha timu hiyo inapata kombe la Ulaya la kwanza tangu mwaka 2013 na kufuzu mashindano ya Klabu bingwa Ulaya mwakani.

Katika michezo mingine, Valencia imeitandika Villareal 2-0, Frankfurt ikaizaba Benfica 2-0, timu hizo zinaungana na Chelsea na Arsenal kucheza nusu fainali ya Europa.

Chelsea sasa itavaana Frankfurt, Arsenal itawakaribisha Valencia katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali hiyo itakayopigwa Alhamisi ya Mei 2 mwaka huu.