Bondia Mkenya Veronica Mbithe aliyepitia maisha magumu kuwa mwanajeshi

  • John Nene
  • BBC Swahili, Nairobi
Mbithe akifanya mazoezi

Veronica Mbithe alikabiliwa na upinzani mkali alipoanza kujifunza ndondi mwaka wa 2014 katika kilabu ya Dallas iliyoko mtaa wa Muthurwa mjini Nairobi nchini Kenya.

Mama yake Mbithe, Eunice Nziva, alikua hataki kabisa msichana wake ajihusishe na ndondi.

``Nilishangaa sana kwa nini mama yangu alikua hataki nicheze ndondi, mpaka siku moja akaficha nguo zangu za mazoezi,'' anakumbuka Mbithe.

Kutokana na upinzani huo wa mamake, ilibidi Mbithe amjulishe kocha wa kilabu ya Dallas Charles Mukula ambaye alizungumza naye na kumueleza umuhimu wa msichana wake kucheza ndondi.

``Hili ni tatizo kubwa ninalokabiliana nalo. Wazazi wengine wanasema wasichana wao wakicheza ndondi watakua wajeuri na wengine nao wanaogopa mimba za mapema kwa mabinti zao,'' anaeleza Mukula.

``Kama kocha nilienda kwa kina Mbithe nyumbani nikamueleza mamake manufaa ya msichana wake kucheza ndondi kama vile kujikinga dhidi ya majambazi na hata kupata kazi ndiposa akakubali lakini shingo upande.''

Mama Mbithe anatueleza ni kwanini hakutaka msichana wake ajihusishe na ndondi..

``Nilikua nimeona mabondia wengi wamecheza lakini ndondi haikuwapeleka popote. Hata hiyo ya Mbithe akicheza mara nyingi nililazimika kutoa pesa zangu mwenyewe kumsaidia, sasa nikashindwa hii ndondi ina maana gani.''

Lakini tangu msichana wake Mbithe aandikwe kazi na Jeshi la Kenya mwaka jana mwezi wa nne, mama Mbithe amebadilishwa mtazamo wake wa ndondi.

``Ni furaha kubwa sana hata sijui niseme nini. Sikutarajia siku moja msichana wangu ataandikwa kazi na Jeshi. Nawashukuru sana watu wa Jeshi kwa kumpa Mbithe kazi.

``Naona siku hizi maisha kwangu yamekua mazuri zaidi kwa sababu tunasaidiana na Mbithe kwa masuala ya kujiendeleza nyumbani. Hata kwa biashara yangu ya saluni ananisaidia kuiendeleza kwani yeye mwenyewe pia anajua sana kazi hii ya saluni.''

Furaha ilioje pia kwa marafiki mabondia wa Mbithe ambao alikua nao kilabu ya Dallas pamoja na kocha wake. Miongoni mwao niliozungumza nao nilipowatembelea wakiwa mazoezini wanasema nao pia wana hamu ya kuingia Jeshi.

``Vile Mbithe amepata kazi kupitia nbondi, tumejua huu mchezo utatupeleka mbali sana hata hisi tupate kazi pia,'' anasema Senewa John, mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya SSD.

``Shida kubwa niliyo nayo ni babangu hataki nicheze ndondi lakini mama hana neno ananipa morali sana, natumai Mbithe kupata kazi kutasaidia kumbadilisha mawazo,'' anasema Senewa.

Maelezo ya picha,

Mbithe akiwa na mabondia wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya

Sheila Jepkemoi, kama mabondia wenzake wa kike, ana morali ndondi itamsaidia kubadilisha maisha yake.

``Tangu Mbithe apate kazi Jeshi la Kenya, sote tumefurahia sana na kumpongeza mwenzetu. Tunajua ndondi yaweza kubadilisha maisha yetu,'' anasema Jepkemoi ambaye alimaliza kidato cha nne mwaka jana katika shule ya Temple Road.

Mbithe anasema ana hamu sana kuona wenzake wa Dallas wanajiunga naye kwani kwa sasa ni yeye tu bondia mwanamke katika timu ya Jeshi.

Ama kwa hakika Mbithe ameweka historia kuwa bondia wa kwanza mwanamke nchini Kenya kujiunga na Jeshi.

``Nimefurahi kuwa bondia wa kwanza mwanamke kuchukuliwa Jeshi la Kenya,'' anasema Mbithe.

Je, ana ushauri upi kwa mabondia wenzake wa Dallas?

``Kile ninachowaambia mabondia wenzangu pale Dallas ni wafanye bidii na wawe na nidhamu bila hivyo si rahisi kufanikiwa. Lazima wajitolee na wafanye mazoezi zaidi ya muda wa kawaida kama wana nia ya kusonga juu.

``Mimi nilipoanza kucheza ndondi mambo hayakua rahisi, shida kubwa ilikua ukosefu wa vifaa vya kutosha hata gloves zilikua chache lakini nilijikakamua vilivyo mpaka nikafanikiwa.''

Mbithe, mwenye umri wa miaka 24, alijiunga na Jeshi mwaka jana wakati alitakiwa kusafiri na timu ya Kenya ya ndondi kuelekea Gold Coast, Australia kwa michezo ya Jumuiya ya Madola.

``Nilipopata barua ya kazi niingie Jeshi tulikua kambi ya mazoezi mjini Nakuru. Kusema kweli nilichanganyikiwa sana hata usiku huo sikulala. Ndio nikapata mawaidha kutoka kwa mabondia wenzangu, mamangu na marafiki wakanishauri niingie Jeshi badala ya kusafiri Gold Coast.

``Nilichukua ushauri wao kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikubali kazi ina umuhimu zaidi wakati huo. Kutoka hapo nikaelekea Eldoret kwa mafunzo ya Jeshi miezi tisa. Mafunzo yalikua mazuri lakini magumu kweli, nikajiondoa ule umtaa wangu nikawa mwanajeshi mwenye nidhamu ya hali ya juu. Hata bunduki sasa naweza kuibeba na nikafyatua risasi bila tatizo. Nawashukuru sana wakuu wa Jeshi kwa kunipa kazi.''

Maelezo ya picha,

Mamake Mbithe , Eunice Nziva, awali hakupendezwa na kipaji cha binti yake

Mbithe ni wa kwanza kwa familia ya watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume. Hamna yeyote anacheza ndondi kama yeye lakini ndugu yake Job Munyaka anacheza kandanda..

Miongoni mwa mabondia wa kike walio changia pakubwa kwake kujiunga na ndondi ni Rebah Matanda na bingwa wa dunia uzani wa super-bantam chama cha WBC Fatuma Zarika.

``Zarika amenisadia kwa mawaidha, na nilipokua nampigia simu anachukua bila tatizo hata akiwa mazoezini, ni bondia na utu na maulana amuongezee,'' anasema Mbithe.

Kocha Mukula anakumbuka jinsi Matanda alivyomvutia Mbithe mpaka akasema siku moja atafikia kiwango chake.

``Matanda alikua bondia wangu hapa Dallas, kisha akaandikwa kazi na polisi. Hii ilimpendeza Mbithe sana, hasa waliposafiri ng'ambo kuiwakilisha Kenya. Nafurahi Mbithe ametimiza ndoto yake. Ndio raha ya kocha hii.

``Nawashukuru Jeshi kwa kumpa kazi lakini naomba wasinisahau hapa kilabu yangu ya Dallas. Ninahitaji vifaa vya kisasa vya mazoezi. Natumai Jeshi watanisaidia kwa vifaa hivyo nami niendelee kukuza vipaji vya mabondia wengine nikiwa hapa mashinani.''

Mabondia wengine wa kike ambao huenda wakajiunga na Jeshi mwaka huu ni mabondia wa kimataifa Christine Ongare ambaye alijishindia shaba kule Gold Coast, Lorna Kusa na Elizabeth Akinyi.

``Haki nitafurahi sana kama hawa wenzangu nao watapata kazi Jeshi, angalau nisiwe na upweke wa mwanamke pekee wa timu ya Jeshi,'' anasema Mbithe ambaye nia yake kubwa kwa sasa ni kushiriki michezo ya mataifa ya Afrika mwezi Agosti mwaka huu nchini Morocco na michezo ya Olimpiki mwakani mjini Tokyo endapo atafuzu.

``Nishaanza mazoezi na timu ya wanaume. Najifunza mengi sana kutoka kwao,'' anasema Mbithe.

``Mamangu ana hamu sana kuniona nikicheza, hutajua ni yule aliyenipinga vikali nicheze ndondi.

``Sasa amekua kama kocha wangu kila mara anataka kujua nitarudi lini ulingoni.Naelewa sana kwanini hapo mwanzo hakutaka nicheze ndondi. Ni mamangu nampenda sana, na nitamsaidia niwezavyo.''