Sterling, van Dijik washinda tuzo za EPL

PFA Haki miliki ya picha PA
Image caption Virgil van Dijk na Vivianne Miedema ni wachezaji wa kwanza kutoka nchi moja kushinda tuzo ya PFA pamoja. Wote ni raia wa Uholanzi.

Raheem Sterling na Virgil van Dijik wameibuka wachezaji bora wa msimu Ligi ya Primia kwa 2018/19 wa ambao upo ukingoni.

Sterling, 24, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu inayotelwa na chama cha Waandishi wa Kandanda (FWA). Tuzo hiyo kwa upande wa wachezaji wanawake imenyakuliwa Nikita Parris, wote wawili wanatokea Manchester City.

Van Dijik ambaye ni beki kisiki wa Liverpool kwa upande wake ameshinda tuzo inayotolewa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa (PFA) nchini humo. Kwa wanawake tuzo hiyo imenyakuliwa na Vivianne Miedema anayekipiga klabu ya Arsenal.

Beki huyo amekuwa wa kwanza kushinda tuzo ya PFA toka iliponyakuliwa na John Terry katika msimu wa 2004/05 alipokuwa akikipiga na Chelsea. Van Dijik pia amemrithi mshambuliaji wa klabu yake ya Liverpool Mohammed Salaah amhaye alishinda tuzo hiyo msimu uliopita.

Klabu ya Liverpool inaendelea kuminyana vikali na Manchester City kuwania ubingwa wa Primia. Timu hizo zinatofautiana alama moja tu na City wameketi kileleni kukiwa na mechi mbili za kucheza kabla msimu kuisha.

Van Dijik ambaye amejiunga na Liverpool Januari 2018 anatajwa kuwa mwamba kwenye safu ya ulinzi wa klabu hiyo.

Liverpool wamecheza michezo 19 bila kuruhusu nyavu zao kuguswa katika mechi 36 walizocheza mpaka sasa msimu huu huku van Dijik akiongoza safu ya ulinzi.

Beki huyo amefunga magoli matatu na kutengeneza magoli mawili kwa timu yake.

"Hii ni tuzo kubwa kwa mchezaji, kuchaguliwa kuwa wewe ni bora na wachezaji wenzako unaocheza dhidi yao kila wiki," amesema van Dijik na kuongeza, "ni kitu cha kipekee na ninajivunia kukipokea."

Katika mbio za ushindi van Dijik amewapiku Raheem Sterling, Bernardo Silva, Sergio Aguero, Sadio Mane na Eden Hazard.

Hata hivyo Sterling pia ameshinda tuzo za PFA kwenye kipengele cha mchezaji kinda.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Raheem Sterling na Nikita Parris wameng'ara na Manchester City msimu huu

Nyota ya Sterling imeendelea kung'ara msimu huu japo amekumbwa na visa kadhaa vya kubaguliwa kwenye ligi ya Primia na hata kwenye ligi ya klabu bingwa Ulaya.

Zaidi ya waandishi 400 ambao ni wanachama wa FWA walipiga kura huku Sterling akimshinda Van Dijik kwa zaidi ya kura 100.

Wachezaji wengine ambao walipata kura japo hawakushinda ni pamoja na Harry Kane, Eden Hazard, Alexandre Lacazette, Bernardo Silva na David Silva.

Sterling anakuwa mchezaji wa kwanza wa City kushinda tuzo hiyo kwa miaka 50 toka iliponyakuliwa na Tony Book mwaka 1969.

"Sterling ni mfano bora wa mchezaji kwenye kipaji ambaye waanzilishi wa tuzo hii walitaka kumtuza walioianzisha mwaka 1947," amaesema mwenyekiti wa FWA Carrie Brown.

"... tuzo hii pia ni kielelezo cha kuthamini ujasiri alionao Sterling katika kupambana na ubaguzi wa rangi, jambo ambalo litaacha alama kwa vizazi vijavyo kwenye mpira na jamii kwa ujumla," amesema Bi Brown.

Mada zinazohusiana