Afcon 2019: Emmanuel Amuneke amjumuisha Kelvin John Pius au 'Mbappe' kuichezea Taifa Stars ya Tanzania

Kinda wa miaka 15 Kelvin John au 'Mbappe' aliifungia timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17

Mkufunzi wa timu ya Taifa Stars nchini Tanzania na raia wa Nigeria Emmanuel Amuneke amemshirikisha kinda wa miaka 15 Kelvin John Pius katika kikosi chake cha watu 39 kitakachoshiriki katika Kombe la mataifa ya Afrika.

John ambaye amepewa jina la utani la mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe aliwafurahisha maskauti katika michuano ya Afrika ya wachezaji wasiozdi umri wa miaka 17 ambalo Tanzania walikuwa mwenyeji.

Kinda mwengine Claryo Boniface kutoka kikosi cha wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20 pia ameorodheshwa katika kikosi hicho.

''Ninaamini ni wakati tuanze kujenga timu na kufikiria siku zijazo'', alisema Amunike.

Tunahitaji kuanza kufikiria kuhusu vijana na kuona iwapo tunaweza kuanza kuwashirikisha katika mfumo wetu''.

John alifunga katika mechi ya ufunguzi ya Tanzania wakati walipopoteza 5-4 kwa Nigeria na kupoteza tena kwa Uganda na Angola huku waandalizi hao wakishindwa kufuzu katika nusu fainali ya michuano hiyo.

Amuneke pia amesema kuwa Tanzania wana mechi ya kufuzu ya CHAN dhidi ya Sudan wiki moja tu baada ya dimba hilo la mataifa ya Afrika.

Mbali na vijana hao , timu hiyo pia inashirikisha wachezaji wanaosakata dimba ugenini pamoja na wale kutoka kwa ligi ya Tanzania.

''Timu hii sio tu ya Afcon bali pia ya CHAN baadaye'', alielezea.

''Hivyobasi kama timu ya kiufundi tunajiandaa vile tutakavyoingiana na CHAN baada ya Afcon''.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii