Champions League: Miujiza ya Tottenham yatoka nyuma na kuilaza Ajax ugenini na kutinga fainali klabu bingwa dhidi ya Liverpool

Spurs ilifunga magoli matatu katika kipindi cha pili kutinga fainali ya klabu bingwa Haki miliki ya picha Getty Images

Klabu ya Tottenham imetoka nyuma na kuwashangaza wenyeji wao Ajax katika mechi ya pili ya nusu fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya.

Lucas Moura alifunga bao la ushindi katika dakika ya 96 na kuisaidia timu yake kutoka nyuma na kuilza miamba ya Uholanzi Ajax Amsterdam 3-2 na kutinga fainali dhidi ya Liverpool.

Wakiwa nyuma 1-0 kutoka mkondo wa kwanza, Spurs ilianza na mkosi mbaya mjini Amsterdam baada ya nahodha Matthijs de Ligt kuruka juu na kufunga kichwa kizuri kufuatia kona .

Hatahivyo Tottenham iligonga mwamba wa goli kupitia Son Heung kabla ya Hakim Ziyeck kufunga goli la pili na hivyobasi kuiweka Ajax kifua mbele baada ya pasi nzuri kutoka kwa mchezaji wa zamani wa Southampton Dusan Tadic.

Bao hilo lilivunja matumaini ya Spurs katika nusu fainali nyengine , lakini katika kipindi cha pili kikosi hicho cha Mauricio Pochettino kilifunga magoli mawili katika muda wa dakika tano.

Moura alipunguza pengo hilo kupitia bao zuri kabla ya mchezaji huyo wa Brazil kusawazisha katika usiku ulioiwacha Tottenham ikitafuta bao moja la ushindi ili kutinga fainali.

Na katika mashambulizi ya mara kwa mara ya Tottenham, Vertonghen alipiga kichwa kilichogonga mwamba wa goli kabla ya Moura kufunga goli lake la tatu kwa kutumia guu lake la kushoto akiwa maguu 16 kutoka kwa goli katika dakika ya sita ya lala salama.

Itakuwa fainali ya pili inayoshirikisha timu za Uingereza baada ya Manchester United kuilza Chelsea katika mikwaju ya penalti katika fainali iliochezewa mjini Moscow 2008.

Ni usiku usio sahaulika kwa Tottenham

Haki miliki ya picha Getty Images

Kocha wa Tottenham Maurico Pochettino hakuweza kuzuia hisia zake baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa ambapo alidondokwa na machozi huku akionekana kusherehekea bila kujali na wachezaji wake.

Raia huyo wa Argentina ambaye ataadhimisha mwaka wake wa tano akiifunza Tottenham baadaye mwezi huu alikuwa katika magoti baada ya usiku kama ule ambao Liverpool ilitoka nyuma na kuilaza Barcelona siku ya Jumanne.

Harry Kane ambaye anaendelea kuuguza jeraha , alijiunga na wenzake uwanjani kusherehekea mbele ya mashabiki wao 2500.

Spurs ilionekana kana kwamba imevunjika nguvu wakati Ziyeck alipounga goli lao la tatu kwa jumla kabla ya kipindi cha kwanza lakini walijikusanya na kutinga fainali ya kombe la klabu bingwa.

Hatahivyo ni mchezaji Lucas Moura aliyerudisha matumaini ya mashabiki wa Tottenham , akitoa pasi tatu nzuri , ya tatu baada ya kichwa cha mchezaji wa zamani wa Ajax Vertonghen kugonga mwamba wa goli kutoka maguu manne huku ikiwa zimesalia dakika nne za muda wa kawaida.

Bao la tatu ambalo ndilo lililobainisha mbivu na mbichi lilijiri wakati alipochukua mpira kufuatia shambulio la Delle Ali ambalo lilipanguliwa na kipa Onana.

Kilikuwa kiunzi muhimu kwa Tottenham kuruka

Walikuwa wamepoteza mechi tatu za nusu fainali ikiwemo mikwaju ya penalti dhidi ya Chelsea katika kombe la Carabao.

Baada ya kuwasili katika uwanja mpya uliogharimu £1bn mwezi uliopita , huu ni wakati muhimu wa Spurs wanaowania kushinda kombe la kwanza katika kipindi cha miaka 11.

Na huku akiwa tayari wamefanikiwa kutinga nne bora katika ligi ya EPL wamesalia na ushindi mmoja pekee kutawazwa mabingwa wa Ulaya.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mtumaini ya Ajax Ulaya yasitishwa ghafla

Ajax imekuwa timu nzuri kuitazama ikicheza katika michuano yote ya klabu bingwa ilioanza tarene 25 mwezi Julai katika raundi ya pili ya muondoano dhidi ya timu ya Austria Sturm Graz.

Wamepata mashabiki wengi wapya wakati wa michuano hiyo ambayo iliondoa miamba ya La Liga Real Madrid na ile ya Seria A Juventus ili kutinga nusu fainali.

Ijapokuwa mabingwa hao mara nne wa Ulaya watahitajika kujipa moyo baadaye baada ya kunyimwa fainali yao ya kwanza tangu 1996 katika dakika za mwisho.

Wakiwa kifua mbele kwa magoli matatu kufikia kipindi cha kwanza , mashabiki wao walikuwa wakisherehekea kabla ya miujiza ya Tottenham kufanyika.

Bao la mapema la nahodha mwenye umri wa miaka 19 De Ligt kutoka kona muda mfupi baada ya kipa Hugo Lloris kuzuia shambulio la Tadic lilifuatiliwa na bao jingine la Ziyeck na hivyobasi kuipatia Tottenham mlima wa kupanda.

Lakini hawakujua kitakachowapata baada ya Spurs wakiongozwa na Moura kubadilisha mambo.

Mchezaji bora -Luca Moura Tottenham

Haki miliki ya picha Reuters

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii