Ander Herrera kuachana na Man United baada ya msimu kuisha leo

Ander Herrera Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Herrera amefunga magoli 20 goals katika mechi 189 alizochezea Man United

Ander Herrera ataachana rasmi na klabu ya Manchester United baada ya mechi ya leo kutokana na mkataba wake kufikia tamati.

Hii leo ndiyo mwisho wa msimu wa Ligi ya Primia 2018/19 na pia ndiyo mwisho wa mkataba wa kiungo huyo raia wa Uhispania na Mashetani Wekundu.

Taarifa juu ya kuondoka kwake zimethibitishwa rasmi jana Jumamosi baada ya kipindi kirefu cha tetesi juu ya mustakabali wa mchezaji huyo klabuni hapo.

Kiungo huyo mwenye miaka 29, alijiunga na United mwaka 2014 kipindi klabu hiyo ikinolewa na kocha Mholanzi Louis van Gaal.

Herrera alijiunga na United akitokea Athletic Bilbao ya Uhispania, na inaelezwa kuwa ataelekea kujiunga na miamba ya Ufaransa klabu ya Paris St-Germain kama mchezaji huru.

United walijaribu kumbakiza Herrera lakini hawakuafikiana na mahitaji aliyokuwa akiyataka Herrera.

Inaarifiwa kuwa mchezaji huyo alighadhibishwa na klabu hiyo kuchukua muda mrefu mpaka kukaa naye kwenye meza ya mazungumzo. Pia inaarifiwa kuwa alitaka aongezewe mshahara na kulingana na wachezaji ambao wanapokea donge kubwa la mishahara.

Uongozi wa klabu ya United uliona kuwa matakwa hayo ya Herrera ni makubwa, na kushindwa kuafikiana naye.

Katika miaka yake mitano Old Trafford, amefunga magoli 20 katika michezo 189 na kutwaa mataji ya kombe la FA, Ligi ya Euoropa na Kombe la Ligi.

Herrera, ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora wa United mwaka 2017 baada kupigiwa kura na mashabiki amesema, "kuna wekundu ndani ya moyo wangu."

"Kuchezea klabu kubwa zaidi England imekuwa ni heshima kubwa sana kwangu. Kila wakati nilipoiwakilisha klabu hii, katika kila mechi, katika ushindi na kufungwa, hata pale nilipokuwa nipo benchi, nilikuwa najua fika uzito wa klabu hii."

Valencia pia aaga

Mechi ya leo dhidi ya Cardiff pia itakuwa ya mwisho kwa nahodha Antonio Valencia, 33, ambaye anaachana na United baada ya kuchezea timu hiyo kwa miaka 10.

Beki huyo wa kulia na winga alijiunga na United mwaka 2009 na ameshinda mataji mawili ya Primia, kombe la FA, makombe mawili ya ligi na kombe la Ligi ya Europa. nd

Mchezaji huyo kutoka Ecuador ameichezea Unite mechi tisa tu msimu huu amesema anataka aendelee kusakata kabumbu kwa walau miaka miwili au mitatu zaidi.

"Uamuzi huu unamaanisha kila kitu kwangu. Ni mchanganyiko wa huzuni na furaha," Valencia ameliambia shirika la habari la kimataifa la Pres Association.

"Huzuni sababu nimeshinda kila taji kama mchezaji kwenye klabu hii, na nitazikumbuka sana zama hizo.

"Ni huzuni pia sababu tumepokea vipigo vikali kama timu, lakini shukrani kwa kuungwa mkono na amashabiki tumeweza kujiinusuru na ninaamini hivi karibuni watapata mafanikio wanayoystahili."

Kuhusu BBC

Mitandao inayohusiana

BBC haina haihusiki vyovyote na taarifa za mitandao ya kujitegemea