EPL 2018: Jinsi Liverpool ilivyopoteza ubingwa wa EPL

wachezaji wa Man City na kocha wao Pep Guadiola Haki miliki ya picha Getty Images

Manchester City wamehifadhi taji la ligi ya Primia baada ya kuifunga Brighton mabao 4-1 na kujipatia alama 98.

Ushindi huo unamaanisha ngoja ngoja ya Liverpool ya miaka 29 kushinda taji hilo inaendelea, licha ya ushinda 2-0 dhidi ya Wolves katika uwanja wa Anfield.

Wachezaji wengi wa Liverpool walionekana kuwa na uchovu kipenga cha mwisho kilipopulizwa, lakini timu ya Jurgen Klopp ilishangiliwa kwa vifijo na nderemo.

Ni vigumu kuamini kuwa wakati mwaka 2018 unaisha, Liverpool walikuwa wanaongoza msimamo wa ligi wakiwaacha Manchester City kwa alama tisa.

Kilichotokea baada ya hapo ni hadithi ya Mikasa na kusikitisha kwa Liverpool.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mohamed Salah na Sadio Mane

City na Liverpool zilikutana Januari 3 huku Liverpool ikiwa inaongoza ligi kwa alama saba na kuwa na uwezekano wa kujikita kileleni kwa alama 10.

Liverpool hata hivyo walipoteza mchezo huo kwa goli 2-1 na kufanya pengo lipunguwe na kufikia alama nne.

Januari 29, City walifungwa na Newcaste goli 2-1. Liveroop walikuwa na wasaa wa kutanua pengo kwa alama 7 laiti wangeliwafunga Leicester City siku moja mbele.

Hata hivyo Liverpool ilitoka sare ya 1-1 katika mchezo huo uliopigwa Januari 30, na kufanya pengo liwe alama tano.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mohamed Salah

Februari 2, Manchester City iliwabamiza Arsenal goli 3-1, magoli yote ya City yakifungwa na Sergio Kun Aguero.

Siku mbili baadae, yaani Februari 4, Liverpool ilirejea tena dimbani dhidi ya West Ham ambapo walitoka sare ya 1-1.

Tofauti ya alama baina ya miamba hiyo ikaendelea kupungua na kufikia alama nne, na kufanya joto liendelee kupanda.

Mwezi Februari uliendelea kuwa mbaya kwa Liverpool kwani tarehe 24 walitoka sare ya bila kufungana na Mancester United.

City wao waliwafunga Chelsea 6-0 wiki moja kabla. Timu hizo zilifikisha michezo 27 na tofauti ya alama ikawa ni moja tu.

Mwezi Machi ndipo Livepool walipigwa kikumbo na City na kuachia uongozi wa ligi.

Ilikuwa Machi 3, ambapo Liverpool walishindwa kutamba mbele ya jirani zao na mahasimu wao wakuu klabu ya Everton kwa kutoka sare ya bila kufungana.

Siku moja kabla, City waliwafunga AFC Bournemouth kwa goli moja bila.

City ikaongoza ligi kwa alama moja, na toka hapo wameendelea kushikilia usikani wa ligi kwa tofauti ya alama moja mpaka wanakabidhiwa ubingwa leo.

Je, Liverpool ina mkosi?

Liverpool, maarufu kama majogoo wa jiji hawajanyanyua ubingwa wa Ligi ya England toka mwaka 1990.

Historia inaonekana kutokuwa upande wa Liverpool katika mbio za kuwania ubingwa wa EPL.

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa timu ambayo inaongoza EPL wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya kuchukua ubingwa.

Katika misimu 11 iliyopita ya EPL, ubingwa ulienda kwa klabu iliyokuwa ikiongoza ligi kwenye msimu wa siku kuu hizo mara nane, na katika mara tatu pekee ambazo haikuwa hivyo yaani msimu wa 2008-09, 2013-14 na 2018-19 ni Liverpool ndiyo ilikuwa kwenye usukani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii