Je, Simba kukabidhiwa kombe mbele ya Sevilla FC?

Simba Haki miliki ya picha Simba SC

Miamba ya soka Tanzania klabu ya Simba SC imetetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.

Simba imenyakuwa ubingwa ikiwa bado ina michezo miwili mkononi baada ya kuichapa Singida United goli 2 bila majibu.

Klabu hiyo yenye maskani yake Kariakoo, Dar es Salaam imefikisha alama 91 baada ya kucheza mechi 36. Alama hizo haziwezi kufikiwa na timu nyengine yeyote kwenye ligi.

Yanga, ambao ni watani wa jadi wa Simba wana alama 83, na hata wakishinda michezo miwili iliyosalia wataishia kuwa na alama 89.

Safu ya ushambuliaji ya Simba imekuwa hatari katika kipindi chote cha msimu, huku wastani wa tofauti ya magoli ya kufungwa na kufungwa klabu hiyo mpaka sasa ni magoli 62. Yanga ni magoli 30 na Azam 29.

Hivyo ukiunganisha wastani Yanga na Azam bado utakuwa nyuma kwa goli moja ukilinganisha na Simba.

Washambuliaji watatu wa Simba wamefunga 54 peke yao mpaka sasa na namba hiyo inaweza kuendelea kupanda katika mechi mbili zijazo. Meddie Kagere aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea Gor Mahia ya Kenya anaongoza kwa magoli 23, John Bocco anafuatia kwa magoli 16, sawia na kinara kwa upande wa Yanga Hartier Makambo na kufuatiwa na Emmanuel Okwi mwenye magoli 15.

Simba kukabidhiwa ubingwa mbele ya Sevilla?

Haki miliki ya picha Tale, Sport Pesa
Image caption Wachezaji wa Sevilla wakiburudishwa baada ya kuwasili Tanzania

Kumekuwa na maombi kwa majuma kadhaa sasa kutoka kwa msemaji machachari wa klabu ya Simba, Haji Manara kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la kukabidhiwa kikombe baada ya mechi dhidi ya Sevilla FC kutoka Uhispania.

Timu ya Sevilla imemaliza katika nafasi ya sita kwenye La Liga, na tayari imeshawasili Tanzania kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Simba.

Haki miliki ya picha Tale, Sports Pesa

Simba inaomba kanuni za ligi 'zilegezwe' ili waweze kukabidhiwa kombe lao kwenye mchezo huo ambao si wa ligi.

Timu ya Sevilla kwa kutumia mitandao yake ya kijamii wamekwishaipongeza Simba kwa kunyakuwa ubingwa.

TFF bado haijatoa majibu hadharani juu ya maombi hayo ya Simba.

Sevilla FC ni klabu ya kwanza ya Uhispania kuizuru Tanzania kucheza mechi ya kirafiki na ni ya pili Ulaya baada ya Everton kushuka pia mnamo 2017 ilipochuana na timu bingwa Gor Mahia kutoka Kenya katika mashindano ya Sport Pesa.

Msimu bora kwa Simba

Ubingwa wa Simba umekamilisha msimu bora wa klabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni. Huu ni ubingwa wa 20 kwa Simba, lakini bado wako nyuma ya wapinzani wao Yanga ambao wameshanyanyua ubingwa huo mara 27.

Ukiacha kutetea mafanikio yake katika mashindano ya nyumbani, Simba msimu huu ilitinga robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 25.

Simba walitolewa kwenye mashindano hayo baada ya kukubali kichapo cha goli 4-1 mbele ya TP Mazembe jijini Lubumbashi, katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya kutokufungana.

Mafanikio ya Simba katika michuano hiyo kwa msimu huu yametokana na kuutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani, katika mechi sita walizocheza nyumbani walishinda tano na kutoka sare moja dhidi ya Mazembe.

Moja ya chachu ya ushindi kwa Simba wakiwa nyumbani ni nguvu kubwa ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiujaza Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki 60,000.

Kwa kuulinda ubingwa wao Simba imejihakikishia nafasi ya kurejea tena katika mashindano ya klabu bingwa Afrika kwa msimu ujao. Changamoto kubwa mbele ya benchi la ufundi ni kuhakikisha hawatakuwa na matokeo mabaya wanapocheza nje ya nchi kama ilivyotokea katika msimu uliopita.