Tanzania na Kenya zinaongoza kwa uvutaji wa bangi Afrika mashariki

Mmea wa bangi

Taifa la Tanzania linaongoza kwa idadi ya watu wanaovuta bangi katika eneo la Afrika mashiriki.

Kulingana na utafiti wa watumizi wa marijuana uliofanywa na shirika la New Frontier Data kutoka Uingereza, Tanzania ambayo iko katika nafasi ya tano kwa idadi ya watumizi wa mmea huo barani Afrika, inaongoza eneo la Afrika mashariki ikiwa na watu milioni 3.6 wanaotumia bangi ikifuatiwa na Kenya ambayo iko nafasi ya sita na watu milioni 3.3 na Uganda katika nafasi ya nane ikiwa na watumizi milioni 2.6.

Mataifa yanayoongoza kwa uvutaji wa bangi barani Afrika ni Nigeria ilio na watumiaji milioni 20.8, ikifuatiwa na Ethiopia yenye watu milioni 7.1, Misri watu milioni 5.9 huku taifa la DR Congo likiwa la 4 na watu milioni 5.

Mataifa ya Burundi na Sudan Kusini hayakuorodheshwa.

Lakini taifa la Sudan linashikilia nafasi ya 7, ilikiwa na watumizi milioni 2.7, likifuatiwa na Madagascar lenye watu milioni 2.1, Ghana milioni 2, Msumbiji watu milioni 1.9, na Angola watu milioni 1.8.

Mataifa ya Afrika yalio na watumizi wa wachache wa bangi kulingana na ripoti hiyo ya 2019 ni pamoja na Zimbabwe ilio na watu milioni 1.1, Malawi watu milioni 1.2, Niger watu milioni 1.2 na Zambia watu milioni 1.4

Ripoti hiyo inajiri siku chache tu baada ya Mbunge wa Kahama mjini nchini Tanzania, Jumanne Kishimba kutoa wito kwa serikali kuhalalisha matumizi ya mmea huo kwa mautumizi ya dawa.

Akizungumza bungeni aliyataja mataifa mengine manne ya Afrika ambayo tayari yemahalalisha Marijuana kutumiwa kutengeneza dawa.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania mbunge huyo anasema kuwa ni vyema kama taifa kuanza kufikiria kuhusu fursa hiyo mapema.

Hivi majuzi rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alinukuliwa akimtaka waziri wa maji na umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa kuwa mkali kusimamia miradi ambayo imekusudiwa na serikali.

''Zinazungumzwa fedha zimeenda kwenye miradi lakini hazikwenda, kuna wakati nilienda kanda ya ziwa ninauliza mradi wa maji uko wapi zimetumika milioni 400 zilikua milioni 800 lakini maji hayapo''

''Sasa nikuombe waziri na watendaji wako mkawe wakali kweli kweli kama una uwezo wa kuvuta bangi ya njombe ili uwe mkali kaivute, kaivute kisirisiri ili wasikuone ukiivuta ili ukienda kwenye mradi hawa mainjinia wa maji wakafanye kazi''.Alisema Rais Magufuli

Nchini Tanzania ni haramu kuvuta bangi na ukiukaji wa sheria hiyo inavutia hukumu kali jela na faini kubwa.

Serikali ya Tanzania imepinga uwezekano wowote wa kuhalalishwa kwa mmea huo katika taifa hilo.

Hatahivyo takwimu mpya za Shirika la New Frontier Data zinakadiria jumla ya masoko ya bangi yalio halali na yasiokuwa halali yanayaouza bangi barani Afrika kuwa dola 37.3b (juu ya Shs139.2 trilioni), na kushuka kwa wastani kati ya $ 18.99b na $ 63.7b.

Bangi hutumika sana barani Afrika huku kukiwa na kiwango cha wastani cha kila mwaka cha asilimia 11.4 kati ya watu wazima wenye umri wa kati ya 15-64, ikikaribia kuwa mara mbili ya kiwango kinachotumika duniani cha asilimia sita ,ripoti hiyo inasema.

Makadirio hayo ya utumizi wa mihadarati yanatokana na data zilizopo kutoka kwa vitengo vya serikali na mashirika ya afya ya umma duniani.

Hatahivyo makadirio hayo hubadilika kila data mpya zinazpopatikana.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mataifa mengine yamehalalisha utumizi wa bangi kwa namna fulani huku mataifa mengine kama Uganda yakiwa katika awamu ya kwanza kutengeneza kanuni zao za masoko.

Huku serikali, wafanyabiashara, maafisa wa afya, na wataalam wa kisheria wakifanya kazi ya kuweka misingi ya masoko mapya ya kisheria kote ulimwenguni, ripoti hiyo inasema kuwa ni muhimu kuelewa ukubwa wa fursa za soko na wanaoshawishi ukuaji wa sekta hiyo.

Mahitaji ya kila mwaka ya bangi duniani yanakadiriwa kuwa $334.4b katika kipindi chote cha mwaka 2018.

Makadirio ya thamani ya mahitaji ya mmea huo hutegemea kiwango kinachotumiwa na kila nchi kwa kila mtumizi na bei yake.

Mwaka wa 2015, Uganda ilianzisha sheria ya mihadarati na Dawa za Kisaikolojia ambayo inaruhusu kilimo, uzalishaji na usafirishaji wa bangi inayotumika kwa matibabu.

Serikali ya taifa hilo imetoa leseni kwa kampuni ya Industrial Hemp (U) Ltd kukuza na kuuza nje bangi ya matibabu kwa madhumuni ya matibabu.

Kampuni ya Hemp (U) Ltd ilianzishwa mwaka 2012 na kwa sasa hufanya kazi ikishirikiana na kampuni ya Pharma Limited, mojawapo ya makampuni makubwa ya marijuana nchini Israeli kwenye soko la hisa la Tel Aviv

Wamewekeza $ 360m katika sekta ya bangi na kuanzisha mashamba ya bangi katika Wilaya ya Hima, Kasese.

Kwa nini mataifa mengi yameanza kuidhinisha matumizi ya bangi?

Haki miliki ya picha Getty Images

Sehemu mbalimbali duniani mtazamo kuhusiana na matumizi ya mmea wa cannabis yaani bangi unabadilika kwa kasi.

Serikali mpya ya Mexico ina mpango wa kuhalalisha matumizi ya bangi kama njia ya kujiburudisha, sawa na ilivyofanya utawala mpya wa Luxembourg. Wakati huo huo, viongozi wakuu nchini New Zealand, wanakusudia kuandaa kura ya maoni ya namna watakavyoshughulikia swala hilo.

Jinsi maoni ya umma - na yale ya serikali- yanavyobadilika, ni dhahiri kuwa mataifa mengi yatafuata mkondo huo. Maswali yanayoibuka ni kwa namna gani nchi hizo zitadhibiti matumizi na usambazaji wa mmea huo?

Ni nini hasa kinachopelekea mataifa mbalimbali katika kulegeza kamba kwenye sheria zake, au hata kuamua kuidhinisha ,matumizi ya bangi moja kwa moja?

Vita dhidi ya mihadarati

Ilikuwa mwaka 2012 ambapo Uruguay, ilipoandika historia kwa kuwa taifa la kwanza duniani kuruhusu matumizi ya bangi kwa minajili ya kujiburudisha. Hatua hiyo, kwa uhalisia, ilikuwa na nia ya kuiwezehsa serikali kushughulikia biashara haramu na magenge ya wahalifu waliokuwa wanaiongoza biashara hiyo.

Baadaye mwaka huo, wapiga kura katika majimbo mawili ya Washington na Colorado, wakawa wa kwanza kabisa nchini Marekani kuunga mkono uidhinishwaji wa matumizi ya bangi ambayo si ya kimatibabu.

Chini ya utawala wa Barack Obama, msisitizo uliwekwa kwenye majimbo kuwa huru katika kubadili sheria zake za kuratibu matumizi ya bangi.

Majimbo manane mengine kwa pamoja na Washington DC, yameunga mkono uhalalishwaji wa bangi kwa njia ya kujiburudisha huku hukumu ya kupatikana au kutumia kama dawa ikilegezwa kwingineko.

Matumizi ya bangi kwa minajili ya dawa, sasa yanakubaliwa katika majimbo 33 kati ya majimbo 50 nchini Marekani.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Uruguay na Canada wanaruhusu uvutwaji wa bangi hadharani

Sasa wimbi hilo limetanda kote Marekani na linakwenda kwa kasi mno, huku Canada ikihalalisha uuzaji, umiliki na matumizi ya bangi kwa njia ya kujiburudisha kote nchini humo mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa Mexico kuhalalisha bangi bila shaka ni jambo la hakika. Serikali mpya ya Andrés Manuel López Obrador imewasilisha muswada bungeni, ambao utahalalisha matumizi yake kama dawa na burudani, ilihali mahakama ya juu zaidi nchini humo, hivi majuzi iliamua kuwepo kwa marufuku ya matumizi ya bangi kwa njia ya burudani, kwamba ni kinyume cha sheria.

Mataifa mengine yanaongeza shinikizo. Ingawa uuzaji wa bangi unasalia kuwa haramu, kupatikana na kiwango kidogo sio tena uvunjaji wa sheria katika mataifa ya Brazil, Jamaica na Ureno.

Nchini Uhispania ni ruhusa kuvuta bangi japo kwa siri, ilihali dawa hizo zinauzwa wazi katika maduka yenye majina Coffee Shops nchini Uholanzi. Bado mataifa mengi yanakubalia matumizi ya cannabis kwa matibabu.

Nchini Uingereza, madaktari wamekubaliwa kuwapa wagonjwa bidhaa za cannabis tangu mwezi Novemba.Korea Kusini wamehalalisha matumizi ya bangi kama dawa lakini chini ya mazingira yenye sheria kali, licha ya kuwahukumu wakaazi wanaotumia dawa hizo hata nje ya nchi.

Haki miliki ya picha Reuters

Hukumu ya kifo kwa mvulana mmoja aliyepatikana akiuza mafuta ya bangi, imesababisha mjadala mkali wa uhalalishaji wa bangi nchini Malaysia. Lebanon inadhamiria kuhalalisha uzalishaji wa cannabis kwa matibabu, na pia kusaidia kuboresha uchumi wa taifa.

Lesotho ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuruhusu kilimo na matumizi ya bangi kwa sababu za kiafya tu. Tayari wakulima wamegeukia zao hilo na wanapata pesa maradufu.

Mwezi Aprili mwaka huu, Zimbabwe ilikuwa nchi ya pili Afrika kuhalalisha uzalishaji wa bagi kwa matumizi ya kiafya na kisayansi.

Septemba mwaka huu Mahakama ya Kikatiba nchini Afrika Kusini ilihalalisha utumiaji wa bangi kwa watu wazima katika maeneo faragha.

Watoto wagonjwa

Mwanzo wa kuhalalisha bangi umekuwa ni huruma ya jamii. Nchini Marekani na Canada, picha za watoto ambao ni wagonjwa na uzima wao ni dawa zenye vimelea vya bangi zilitumika kufanya kampeni ya kuhalalisha bangi.

Canada iliruhusu matumizi ya bangi kimatibabu mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kuruhusu kuwa kiburudisho mwaka huu.

Mtazamo kama huo pia umeshuhudiwa nchini Uingereza.

Mwezi Juni, Billy Gladwell mwenye umri wa miaka 12, aliyekuwa akiugua kifafa, alilazwa hospitalini, baada ya dawa yake mafuta ya bangi ilipokamatwa. Mwezi mmoja baadaye, leseni maalum ya kutumia mafuta ya bangi ikatolewa kwa Alfie Dingley mwenye umri wa miaka 7, aliyekuwa akiugua pia kifafa.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mamake Alfie Dingley anasema mafuta ya cannabis imemsaidia mwanawe dhidi ya kifafa

Mwezi Juni, Billy Gladwell mwenye umri wa miaka 12, aliyekuwa akiugua kifafa, alilazwa hospitalini, baada ya dawa yake mafuta ya bangi ilipokamatwa. Mwezi mmoja baadaye, leseni maalum ya kutumia mafuta ya bangi ikatolewa kwa Alfie Dingley mwenye umri wa miaka 7, aliyekuwa akiugua pia kifafa.

Kufuatia kampeni ya nguvu, serikali ya Uingereza iliamua kubadilisha sheria ili kuwakubalia madaktari kuwapa wagonjwa matibabu yanayotokana na bidhaa za bangi.

Lakini nchini Uingereza, Wizara ya mambo ya ndani, inasema matumizi ya bangi kwa njia ya burudani, itasalia kupigwa marufuku, hata ingawa maafisa wakuu, akiwemo kiongozi mmoja mkuu wa chama cha Conservative, William Hague, akipendekeza hatua hiyo ifikiriwe upya.

Mexico pia ina kesi ya watoto wanaokatazwa kupewa bangi kwa matibabu, lakini pia inakabiliwa na changamoto ya ghasia zinazohusishwa na vita vya ulanguzi wa mihadarati.

Hata ingawa bangi ni sehemu ndogo mno ya asilimia kubwa ya magenge yanayojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya, marufuku dhidi yake inaonekana kuchochea zaidi kuongezeka kwake kuliko hali ilivyo.

Wanadiplomasia wa Mexico, wanaionya Marekani kuwa, ni vigumu mno kukabiliana na bangi huku jimbo jirani la California limeidhinisha matumizi yake.

Masoko ya Bangi

Haki miliki ya picha Getty Images

Huku mataifa mengi duniani yakielekea katika hali ya kuleta mabadiliko ya uhalalishaji wa bangi, ni wazi soko la zao hilo litazidi kupanuka.

Serikali za nchi za Amerika ya Kusini zinataka wakulima wao kuyafikia masoko hayo ya biashara kubwa ya ukulima wa bangi kwa minajili ya matibabu, ambayo yanaszidi kukua kila uchao.

Nchini Lesotho, wakulima tayari wameanza kuvuna faida ya kilimo hicho.

Mashirika makubwa pia yameonyesha hitaji la kujiunga nayo. Kampuni ya Altria, ambayo ni wazalishaji wa chapa maarufu ya sigara za Marlboro wapo katika mazungumzo na kampuni moja ya kuzalisha bangi nchini Canada ili wawekeze mtaji wao wa dola bilioni 1.86.

Wazalishaji wa bia ya Corona, kampuni ya Constellation Brands imesema itawekeza dola bilioni 4 kwenye kampuni kubwa zaidi ya uzalishaji bangi nchini Cananda, Canopy Growth. Uwekezaji huo ndio mkubwa zaidi mpaka sasa katika biashara ya bangi duniani.

Kampuni maarufu ya vinywaji ya Coca-Cola ni maarufu zaidi kwa kutengeneza soda, lakini sasa inapanga kufanyia majaribio aina mpya ya kinywaji ambacho kitakuwa na bangi.

Changamoto kubwa kwa sasa, ni matumizi ya cannabis kwa burudani, haiwezi kuwa biashara kutoka taifa moja hadi nyingine. Mataifa tu yatanunua bidhaa hiyo kutoka nje au kuuza nje ya nchi kama tiba chini ya mfumo wa leseni inayopigiwa msasa na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Mihadarati.

Wakulima katika mataifa kama vile Morocco na Jamaica, wanasifika kwa kuzalisha bangi nzuri lakini hawataweza kuyafikia masoko ambayo wakulima wake wa ndani si wazuri kama ilivyotokea nchini Canada mara tu baada ya kuhalalisha.

Madhara ya Bangi

  • Unaweza kusababisha kuchanganyikiwa na wasiwasi usio wa kawaida
  • Ikivutwa na tumbaku, inaweza kuongeza hatari ya ugonjwa kama vile saratani ya mapafu
  • Matumizi ya mara kwa mara yamehusishwa na hatari ya kupatwa na magonjwa ya kiakili
  • Upungufu wa kudumu wa kiwango cha mtu kufikiria na kufahamu mambo, baada ya kutumia kwa muda mrefu