Harry Kane: Mshambuliaji wa Tottenham asema amepona na yupo tayari kumenyana na Liverpool

Harry Kane Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji tegemezi na nahodha wa klabu ya Tottenham Harry Kane amesema yupo tayari kuvaana na Liverpool kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya Jumapili ijayo.

Kane, 25, alipata majeraha makubwa ya kifundo cha mguu baada ya kuteleza na kuanguka kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe hilo dhidi ya Man City Aprili 9.

Kocha wa Spurs Mauricio Pochettino awali alisema nahodha huyo wa Uingereza angelikuwa nje ya uwanjwa kwa mechi zote zilizosalia.

"Najisia vyema sana sasa. Sina shida tena," amesema Kane.

"Nilianza kurudi kwenye kikosi toka mwishoni mwa wiki iliyopita. Wiki hii narejesha nguvu na ukakamavu wa mwili kwa kadri ya uwezo wangu," amesema.

"Baada ya hapo itakuwa juu ya kocha kuamua. Yeye ndiye atafanya tathmini yake na kufanya maamuzi ya kunujumisha kikosini ama la. Lakini mpaka sasa mimi majisikia vizuri na nipo tayari kwa mchezo.

Kane ameifungia Tottenham magoli 24 msimu huu kwenye michuano yote licha ya kuwa nje ya uwanja kwa wiki sita baina ya Januari na Februari baada ya kuumia kifundo cha mguu huo huo alioumia mwezi uliopita.

Pia alikaa benchi mwezi mmoja msimu uliopita kwa jeraha hilohilo.

Kuhusu uwezekano wa Kane kucheza, Pochettino amesema : "Siwezi sema kuwa yupo sawa kwa 100%, ama iwapo atakuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba ama la. Lakini tuna furaha kuona napona kwa kasi."

Haki miliki ya picha Reuters

"Ni jambo la muhimu sana kwake kuona kama anajisikia nafuu. Mimi naombea heri zaidi. Tuna wiki moja zaid ya kuendelea kufuatilia maendeleo yake.

Kocha huyo amesema japo Keane ni mtu muhimu, lakini wanaelekeza nguvu yote kwenye timu kwa ujumla.

"Mpira ni mchezo unaohusisha timu nzima, umoja na imanani thabiti. Tazama namna ambavyo tumefika fainali. Pale Harry (Kane) alipoumia kwenye robo fainali, nini kilitokea," amesema Pochettino.

"Hilo halimaanishi kwamba yeye si moja ya wachezaji bora wa kikosi chetu. Kwangu yeye ni moja ya washambuliaji mahiri kabisa duniani - yupo kwenye tatu bora.

"Inatubidi tuwafunge Liverpool na kama atakuwepo, litakuwa jambo jema zaidi."

Mada zinazohusiana