Mchezaji nyota wa Brazil Neymar akanusha madai ya ubakaji jijini Paris

Neymar kwa sasa anashiriki mazoezi na timu ya taifa Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Neymar kwa sasa anashiriki mazoezi na timu ya taifa

Nyota wa kandanda wa Brazil amekanusha tuhuma za kumbaka mwanamke mmoja jijini Paris.

Kulingana na ripoti ya polisi iliowasilishwa mjini Sao Paulo , mwanamke huyo amedai kwamba shambulio hilo lilfanyika katika hoteli moja katika mji huo ambapo Neymar anaichezea klabu ya Paris St Germain PSG.

Neymar ameamua kutoa utetetezi wake kwa kurekodi video na kuonesha kile alichokiita mfululizo wa ujumbe wa Whatsapp baina yake na mwanamke huyo.

Neymar kwa sasa yuko nchini Brazil kwenye kambi ya timu ya taifa katika maandalizi ya kombe la Copa America.

Je anakabiliwa na madai gani?

Kulingana na ushaidi wa polisi , mwanamke huyo ambaye jina lake halijatajwa alijuana na Neymar kupitia mtandao wa Instagram na Neymar akashauri wakutane Paris.

Alimtumia tiketi ya ndege kutoka Brazil kuelekea Ufaransa mbali na kumlipia chumba cha kulala katika hoteli ya kifahari ya Sofitel Paris arc Du Triomp.

Mnamo tarehe 15 mwezi Mei mwanamke huyo amedai kuwa Neymar alitokea akiwa ni mlevi.

Baada ya mazungumzo Neymar na kukumbatiana, "ikafika hatua Neymar akawa analazimisha mambo, na kwa kutumia nguvu akamuingilia mwanamke huyo bila ridhaa yake," kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Mwanamke huyo alirejea Brazil siku mbili baadaye, bila kuripoti tukio hilo kwa maafisa wa polisi wa Ufaransa, kwa kuwa "alikuwa amejawa na hofu kuwasilisha malalamishi yake katika taifa geni," taarifa ya inaendelea kueleza.

Je Neymar amesema nini?

Taarifa iyotolewa na uongozi wa mchezaji huo, imekemea vikali kile ilichokiita madai yasiyo na msingi wala haki.

Taarifa hiyo imedai kuwa Neymar ndiye amekuwa "mhanga wa jaribio la kulazimishwa kutoa pesa" na "ushahidi wa jaribio hilo na kutokutokea kwa ubakaji utawasilishwa polisi."

Neymar,27, amechapisha video yake ya kujitenga na tuhuma hizo katika ukurasa wake wa Instagram.

Mchezaji huyo ambaye hajaoa ameambatanisha video hiyo na maelezo kuwa: "kutokana na kulazimishwa kutoa fedha, nalazimika kuanika maisha yangu na ya familia yangu.."

"Kilichotokea siku ile kilikuwa na faragha ya wapenzi wawili, yalikuwa ni mahusiano ya mwanaume na mwanamke ndani ya kuta nne. Siku ya pili hakukuwa na mengi yaliyotokea. Tuliendelea kutumiana ujumbe kwenye simu, akaniomba nimtumie zawadi (ya mtoto wake)," amesema Neymar.

Katika video hiyo Neymar ameonesha msururu wa kile alichokiita ujumbe wa simu baina yao na mpaka picha za msichana huyo akiwa amevalia nguo zake za ndani tu.

Baba wa mchezaji huyo dos Santos pia aliambia runinga ya Band nchini Brazil siku ya Jumamosi kwamba ilikuwa wazi kwamba mwanawe alikuwa amewekewa mtego.

''Iwapo umma hautaambiwa ukweli kuhusu kisa hiki na iwapo hatuwezi kuonesha ukweli kwa haraka tuhuma hizo zitakuwa kubwa. Iwapo tutalazimika kuonesha mawasiliano ya Neymar ya Whatsapp na msichana huyu tutayaonesha'', aliongezea.

Je Neymar yuko tayari kushiriki katika kombe la Copa America?

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amepokonywa unahodha wa Brazil kutokana na madai ya utovu wa nidhamu wa hivi karibuni.

Shirikisho la a soka nchini Ufaransa lilimpiga marufuku Neymar kwa mechi tatu baada ya kumshambulia shabiki mmoja kufuatia kushindwa kwa PSG na timu ya Rennes katika mchuano wa kuwania taji la Coupe De France mwezi uliopita.

Pia amedaiwa kuhusika katika makabiliano na mchezaji mwenza.

Kombe la Copa America linaloshirikisha timu za America kusini linafanyika nchini Brazil kutoka tarehe 14 mwezi Juni hadi tarehe 7 mwezi Julai huku wenyeji wakicheza dhidi ya Bolivia , Venezuela na Peru katika kundi A.

Neymar alilazimika kuwacha mazoezi siku ya Jumanne wakati alipopata jeraha la goti , ijapokuwa jeraha hilo halikuwa baya sana.

Mada zinazohusiana