Najila Trindade: Mwanamke aliyemshutumu Neymar kwa ubakaji ahojiwa na runinga ya Brazil

Neymar amekana madai kamba alimbaka Najila Trindade mjini Paris Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Neymar amekana madai kamba alimbaka Najila Trindade mjini Paris

Mwanamke aliyedai kubakwa na mchezaji wa soka nchini Brazil Neymar amejitokeza hadharani na kumshtumu mchezaji huyo katika runinga moja ya Brazil

Najila Trindade aliambia runinga ya SBT nchini Brazil kwamba kisa hicho katika hoteli moja ya Paris mnamo tarehe 15 mwezi Mei kilikuwa cha unyanyasaji pamoja na ubakaji.

Neymar amekana madai hayo , akituma ujumbe wa Whats App ili kujaribu kuonyesha kwamba hana hatia.

Aliichezea kwa muda mfupi timu yake ya Brazil siku ya Jumatano katika mechi aliyodai kuwa ngumu katika kipindi chote che uchezaji wake.

Neymar alipata jeraha baada ya dakika 20 ya mechi hiyo dhidi ya Qatar mjini Brasilia na sasa atakosa kushiriki katika michuano ya kombe la Copa America 2019 nchini Brazil akiwa na jeraha la mguu.

Ni nini kilichosemwa katika mahojiano?

Bi Trindade anasema kuwa alivutiwa na mchezaji huyo wa PSG na Brazil na alitaka kushiriki ngono naye. Anasema alisafarishwa kwa ndege hadi mjini Paris na kulipiwa katika hoteli ,moja ya mjini Paris.

Bi Trindade alikuwa mtu wa kawaida- mwanamitindo na mwananfunzi wa mitindo , mtoto na mama.

Aliyekuwa akimuhoji alimuuliza Bi Trindade iwapo kile kilichotokea ulikuwa ubakaji na bi Trindade alimjibu kwamba ulikuwa unyanyasaji wa kingono na ubakaji.

Anasema kwamba wakati walipokutana na Neymar alikuwa mtu wa fujo ''mtu tofauti na yule niliyemjua katika ujumbe''.

Bi Trindade alikua amejiandaa kushiriki ngono lakini akataka watumie mipira ya kondomu. Anadai kwamba Neymar alikataa akaleta fujo na kumbaka.

Anasema kwamba alimwambia kuacha kufanya hivyo lakini akakataa.

SBT ilichapisha baadhi ya mahojiano hayo katika mtandao wa Twitter { kwa Kireno).

Video imepatikana.Je inaonyesha nini?

Kanda ya Video inaonyesha mtafaruku kati ya bi Trindade katika chumba kimoja cha hoteli-ikidaiwa kuchukuliwa na bi Trindade.

Wawili hao wanaonekana wakiwa wamelala katika kitanda ambapo baadaye mwanamke huyo anasimama na kuanza kumpiga mwanamume aliyelala kitandani ambaye anajikinga na miguu yake.

Mwanamke huyo anasema nitakupiga, unajua kwa nini kwasababu umenipiga , mtafaruku huo ukionekana kuwa mkutano wao wa pili .

Neymar amesema kuwa yeye na bi Trindade walikutana mara mbili.

Katika mahojiano hayo ya Runinga ya SBT , Bi Trindade alisema kuwa alianza kuelewa kila kitu kilichofanyika baada ya mkutano wao wa kwanza ulipokamilika na kwamba alirudi ili kuthibitisha kitendo kilichofanyika huku akitaka haki kufanyika.

Kanda hiyo ya Video ilionyeshwa katika kituo hicho cha Brazil.

Je Neymar amesema nini?

Neymar hajatoa tamko lolote kufikia sasa kuhusu mahojiano hayo ya runinga.

Babake Neymar dos Santos , alihojiwa na TV Record kuhusu kanda hiyo ya video iliochukuliwa katika chumba cha hoteli na alisema kuwa ,mwanawe alikuwa ametegwa na kwamba Neymar alikuwa hana hatia.

Katika taarifa ya mapema , Usimamizi wa Neymar uliziita shutuma hizo kuwa zisizo na haki na kusema kuwa mchezaji huyo alikua mwathiriwa wa jaribio la kumlaghai. Neymar alirudia madai hayo ya ulaghai katika ukurasa wake wa Instagram kwa dakiika saba.

Akizungumza kwa lugha ya Kireno , mchezaji huyo alisema: Kile kilichotokea siku ile ni mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamume na mwanamke ndani ya chumba kama inavyokuwa kati ya wapenzi wawili.

Na siku iliofuatia hakuna kubwa lililotokea. Tuliendelea kutumiana ujumbe . Aliniomba zawadi ya mtoto wake .

Katika kanda hiyo ya video , mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alionyesha kile alichokitaja kuwa msururu wa ujumbe wa WhatsApp kati yake na Trindade , ikiwemo picha za kimapenzi naye."

Anasema kwamba alilazimika kuziweka wazi ili kuonyesha kwamba kulikuwa hakuna na mno. katika mahojiano hayo bi Trindade alikana kujaribu kumlaghai bi Trindade akisema kuwa . Nataka haki na sio kulipwa fidia ya kifedha.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro alimtembelea Neymar hospitalini baada ya mchezaji huyo wa kandanda kupata jeraha siku ya Jumatano ''akimtakia kupona kwa haraka'' ,bwana Bolsonaro alisema awali.

''Yuko katika hali ngumu lakini namuamini''.

Je hali ya kisheria ikoje?

Mawakili waliomwakilisha bi Trindade wanasema kuwa malalamishi yake ya kwanza yalikuwa ya uchokozi ama kupigwa na Neymar.

Wanasema kwamba walikuwa wamekubaliana jinsi ya kutatau swala hilo na mawakili wa Neymar lakini baadaye mawakili hao walikataa.

Mawakili wa pande zote mbili walitofautiana kuhusu ni nani haswa aliyeitisha kikao hicho.

Baadaye Trindade aliwasilisha mahakamani madai yake siku ya Ijumaa mjini Sao Paulo.

Neymar pia huenda akakabiliwa na uchunguzi kuhusu kuchapisha picha za Trindade bila ruhusa yake ka kuwa kitendo hicho huenda kikakiuka sheria za kulinda faragha ya mtu.