Paul Pogba asema anahitaji changamoto mpya sehemu nyengine

Pogba Haki miliki ya picha Getty Images

Kiungo wa Manchester United Paul Pogba amesema "muda huu unaweza kuwa ni muafaka kwake kuhamia sehemu nyengine."

Kiungo huyo kinara wa timu ya taifa ya Ufaransa, anahusishwa na kutaka kuhamia katika klabu kongwe na tajiri ya nchini Uhispania, Real Madrid.

Pia klabu yake ya zamani, miamba ya Italia, Juventus, pia inahusishwa na mipango ya kuta kumsajili.

Hata hivyo, kiungo huyo mwenye miaka 26, ambaye alikuwa pekee kutoka Man United kujumuishwa kwenye kikosi bora cha ligi kwa msimu ulioisha wa 2018/19, yungali na mkataba na United mpaka mwaka 2021.

"Ninalifikiria suala hili: Kupata changamoto mpya sehemu nyengine," ameeleza Pogba.

"Nimekuwa Manchester kwa miaka mitatu sasa, na nimekuwa na Maisha mazuri; nimekuwa na nyakati nzuri na mbaya pia, kama ilivyo kwa watu wengine pia. Kama sehemu nyengine pia.

"Baada ya msimu huu, na kila kilichotokea… Nafikiri kwangu itakuwa ni jambo jema kupata changamoto mpya."

Japo kuna uwezekano wa kupata fedha nyingi, inaonekana kuwa uongozi wa Man United unaamini Pogba ataendelea kusalia katika uga wa Old Trafford msimu ujao.

Haki miliki ya picha Getty Images

Pogba alirejea Manchester United baada ya kuchezea klabu ya Juventus kwa misimu minne.

Uhamisho huo ulifanyika mwaka 2016, kwa dau la pauni 89.3 milioni, ambayo kwa kipindi hiko lilikuwa ndio dau kubwa zaidi.

Pogba aliibukia kwenye kituo cha kukuzia wachezaji wachanga cha klabu ya Man United.

Toka arejee kutoka Juventus Pogba amecheza mechi 89 za ligi ya Primia na kufunga magoli 24.

Mwezi Aprili, kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer alisema kuwa anataraji kiungo huyo ataendelea kusalia klabuni hapo msimu ujao.

Je, Pogba ataondoka?

Muda utaongea.

Mada zinazohusiana