AFCON 2019: Lifahamu kundi gumu zaidi katika michuano ya mwaka huu

kOMBE Haki miliki ya picha Getty Images

Zimesalia siku tatu pekee kabla ya michuano ya kandanda ya Mataifa ya Afrika kuanza nchini Misri - lakini swali swali ni, lipi kundi gumu zaidi kati ya sita yaliyopo?

Kwa mashabiki wa mpira Afrika Mashariki, kundi lilolomo midomoni wao zaidi ni C, na wengi yamkini wakilitazama kundi hilo kama gumu zaidi kwenye micguano hiyo.

Kundi hilo linaundwa na timu jirani na hasimu za Tanzania na Kenya pamoja na timu zenye uzoefu na wachezaji wakubwa kimataifa za Senegal na Morocco.

Lakini je, kundi hilo ni gumu kiuhalisia ama ni hisia tu za wapenzi wa kandanda wa Kenya na Tanzania?

Kwa wafuatiliaji wa kandanda na wachambuzi, kundi hilo linaonekana kuwa ni la kawaida, huku Senehal yenye wachezaji wakubwa kama Sadio Mane na Khalidou Koulibaly na Algeria yenye wachezaji kama Riyad Mahrez zikipigiwa upatu kusonga mbele.

Iwapo Tanzania na Kenya itaifunga timu yoyote kati ya hizo matokeo hayo yatachukuliwa kama ya kushangaza kwenye ulimwengu wa kandanda.

Kama kundi C siyo gumu, basi kundi lipi ni gumu ama kundi la kifo kama ifahamikavyo kwenye lugha za kimichezo?

Image caption Mauritania wamefuzu kwa mara ya kwanza michuano hiyo

Wachambuzi wanaamini kuwa kundi D lenye timu za Ivory Coast, Morocco, Afrika Kusini na Namibia.

Timu tatu katika hizo ukiacha Namibia washawahi kunyakua ubingwa wa Afcon hapo kabla. Na ukiangalia uhalisia timu ya Namibia haipigiwi upatu kupenya kwenye kundi hilo.

Swali ni timu zipi mbili katika mabingwa hao wa zamani watafuzu kwa hatua ya mtoano ya michuano hiyo?

Kwa mujibu wa takwimu za ubora wa timu zinazotolewa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni Fifa, Morocco ndiyo timu yenye kiwango cha juu zaidi kwenye kundi hilo ikishika nafasi ya 47 duniani, ikifuatiwa na Ivory Coast katika nafasi ya 62, Afrika Kusini nafasi ya 72 huku Namibia ikiachwa mbali katika nafasi ya 113.

Haki miliki ya picha TFF/Twitter
Image caption Je Mbwana Samatta atawika mbele ya Senegal na Algeria?

Ni vyema kuwa na tahadhari lakini kuwa, si mara zote takwimu za nje ya uwanja huwa na uhalisia uwanjani.

Mwaka 2012, timu ya taifa ya Zambia ambayo haikuwa wachezaji wenye majina makubwa iliushangaza ulimwengu wa kandanda kwa kuchukua kombe hilo ikiifunga kwa mikwaju ya penati timu ya Ivory Coast ambayo inatajwa kuwa ni kizazi cha dhahabu cha taifa hilo.

Ivory Coast ya wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Didier Drogba, pamoja na nyota wengine kama ndungu Yaya na Kolo Toure, Solomon Kalou, Didier Zokora na Gervinho. Lakini walishindwa kuwafunga Zambia ya akina Stophira Sunzu, Christopher Katongo, Rainford Kalaba, Emmanuel Mayuka na wengineo.

Kundi ambalo linaonekana kufuatia kwa ugumu ni F lenye timu za Benin, Cameroon, Ghana na Guinea Bisau.

Kwa macho ya kawaida, Cameroon na Ghana wanapigiwa upatu kupita kwenye kundi hilo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Cameroon ndio mabingwa watetezi wa kombe la Afcon

Cameroon ni mabingwa mara tano wa michuano huku Ghana wameshinda mara nne kombe hilo.

Hata hivyo timu zote za kundi hilozinatokea katika ukanda wa Afrika Magharibi na zinajuana vilivyo katika sampuli zao za uchezaji.

Kundi A pia linaonekana jepesi kwa mwenyeji wa michuano hiyo timu ya Taifa ya Misri ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo.

Hata hivyo kutakuwa na kipute kigumu si haba baina ya mataifa ya DRC, Zimbabwe na Uganda.

Yote kwa yote, hesabu za makundi zitatimia pale michezo hiyo itakapoanza kutimua vumbi Ijumaa.

Si ajabu Kenya ama Tanzania zikafuata nyayo za Zambia katika kuangusha timu kubwa kama ilivyotokea mwaka 2012.