Makamu wa rais wa Barcelona FC: Neymar anataka kurudi Barcelona kutoka PSG

Former Barcelona striker Neymar Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alijiunga na PSG kutoka Barcelona kwa dau lililovunja rekodi la £200m 2017

Mshambuliaji wa Paris St-Germain Neymar anataka kurudi Barcelona kulingana na naibu rais wa klabu hiyo .

Hatahivyo Jordi Cardoner amesisitiza kuwa hakuna mawasiliano yoyote yaliofanyika kati yao na mchezaji huyo ambaye alihudumu miaka minne katika klabu hiyo ya Nou Camp.

Mchezaji huyo wa Brazil ametaabika katika klabu ya PSG tangu aliposajiliwa kwa dau lililovunja rekodi la dunia 2017.

''Kile ninachoamini ni kwamba Neymar anataka kurudi, Cardoner alisema''. ''lakini kusema kwamba tumeanza mikakati ya kutaka kumsajili hicho ni kitu ambacho sitakubaliana nacho''.

Kumekuwa na uvumi kuhusu ni klabu gani Neymar atahamia iwapo ataondoka PSG , swala ambalo Cardoner aliulizwa katika mkutano na vyombo vya habari siku ya Alhamisi.

Alikiri kwamba ni wazi alikuwa anataka kurudi Barca, lakini akaongezea kwamba klabu yake haijaamua kuhusu kumrudisha tena mchezaji huyo ama hata kufanya mazungumzo naye.

''Hatusajili mtu yeyote kwa sasa husan mchezaji huyu ambaye hatujawasiliana naye'', alisema.

Uhamisho wa Neymar wa kuelekea PSG 2017 ulivunja rekodi ya dunia huku klabu hiyo hiyo ya ligue 1 ikilipa dau la £200m).

Aliisaidia timu hiyo kushinda mataji kadhaa ya ligi hiyo na kufunga magoli 34 katika mechi 36, lakini kipindi chake katika uwanja huo wa Parc des Princes kiligubikwa na uvumi wa makabiliano katika chumba cha maandalizi mbali na mafuruku mbili za kumpiga shabiki na kumtusi afisa mmoja wa mechi.

Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Uhispania , amejitolea kupunguziwa mshahara kwa Yuro milioni 12 kila mwaka ili kuweza kurudi katika klabu hiyo.

Antoine Griezmann anatarajiwa kujiunga na klabu hiyo ya Catalan kutoka Atletico Madrid kwa dau la Yuro milioni 120 huku Frenkie de Jong akisaini kwa Yuro milioni 75 kutoka Ajax.